Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 13 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 7...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyo onekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa wote walio hai,Mungu  wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Mungu mwenye huruma
Baba mwenye kusamehe,Baba wa yatima,Mume wa wajane,Muweza
wa yote,Alfa na Omega...!!


Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.”

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwa akili zetu
si kwa nguvu zetu na si kwamba sisi ni wazuri mno..
Nikwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!!



Yahweh tazama jana imepita leo ni siku mpya na kesho ni siku
nyingine..
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea...
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Yahweh utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za 
mpinga Kristo zikashindwe katika jina la Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo...
Jehovah tunaomba ukatutakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu ukatufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona,kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...


Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako’. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja. Mwenye masikio na asikie! “Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: ‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkuomboleza!’ Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: ‘Amepagawa na pepo’. Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: ‘Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji...

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu
tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwanao
mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo...
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha yetu,Mungu wetu tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti
yako na kuitii,Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia
zako Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku
zote za maisha yetu,Yahweh ukatupe neema ya kutambua
mema na mabaya,Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha 
yetu,Baba wa Mbinguni ukatufanye barua njema nasi tukasomeke
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”

Yahweh tazama wenye shida/tabu,Wagonjwa,wenye njaa,
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,
walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,walio katika vifungo vya
yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walioanguka/potea
waliokwenda kinyume nawe,wote walio elemewa na mizito mizito,
walioumizwa rohoni,walio kwama kibiashara,wanaotafuta kazi,
wenye kutafuta watoto na wengine wote kila mmoja na hitaji lake..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kiroho na kimwili pia
Jehovah tunaomba ukawavushe salama,Mungu wetu ukawaoke
na kuwalinda,Baba wa Mbinguni haki ikatendeke
Yahweh tunaomba ukabariki mashamba yao,vyanzo vyao
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea na kufuata
njia zako,Jehovah tunaomba ukawasamehe na kuwasimamisha tena
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni ukawafute
machozi yao,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze,Neema/rehema zikawe nao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu

Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Mungu wetu ukawatendee sawaswa na mapenzi yako
Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina....!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami/kunisoma
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye...
Amani ya Kristo Yesu ikawe nayi daima....
Nawapenda.

Ikulu ya Solomoni

1Solomoni alijijengea ikulu, nayo ilimchukua miaka kumi na mitatu kumalizika. 2Kisha, akajenga jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Urefu wake ulikuwa mita 44.5, upana wake mita 22.25, na kimo chake mita 13.5. Ilikuwa imejengwa juu ya safu 3 za nguzo za mierezi, nguzo ambazo zilishikilia boriti za mierezi kwa upande wa juu. 3Kila safu ilikuwa na nguzo 15; basi zote pamoja zilikuwa nguzo 45. Vyumba vilivyojengwa juu ya nguzo hizo, alivitilia dari ya mbao za mierezi. 4Kulikuwa na safu tatu za madirisha yaliyoelekeana. 5Milango yote ilikuwa ya mraba, na miimo ya madirisha hayo yaliyoelekeana ilikuwa pia ya mraba.
6Alijenga ukumbi wa nguzo, ambao urefu wake ulikuwa mita 22.25, na upana wake mita 13.5. Kwenye sehemu ya mbele ya jengo hilo kulikuwa na sebule. Mbele ya sebule kulikuwa na nguzo; na mbele ya nguzo kulitokeza paa dogo.
7Solomoni alijenga ukumbi wa kiti cha enzi ambamo aliamulia kesi za watu. Huu uliitwa pia Ukumbi wa Hukumu. Ulikuwa umepambwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafu mpaka dari.
8Nyumba yake ya kukaa mwenyewe, iliyokuwa nyuma ya Ukumbi wa Hukumu, ilikuwa imejengwa kama zile nyingine. Solomoni pia alijenga nyumba kama ukumbi huo kwa ajili ya binti Farao, ambaye alikuwa amemwoa.
9Majengo hayo yote yalijengwa kwa mawe ya thamani kutoka msingi mpaka juu, mawe ambayo yalikuwa yamechongwa kwa vipimo maalumu, na kukatwa kwa msumeno upande wa ndani na wa nje. 10Msingi ulikuwa wa mawe ya thamani na makubwa yenye urefu wa mita 3.5, na upana mita 4.5. 11Sehemu za juu zilijengwa kwa mawe mengine yaliyochongwa kwa vipimo maalumu, na kwa mbao za mierezi.
12Ua wa nyumba ya mfalme ulikuwa na kuta zenye safu moja ya mbao za mierezi na safu tatu za mawe ya kuchongwa kila moja; ndivyo ilivyokuwa hata kwa ua wa ndani wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kwa ukumbi wa nyumba.

Kazi za Hiramu

13Kisha mfalme Solomoni alimwita Hiramu kutoka Tiro. 14Huyo, alikuwa mwana wa mjane wa kabila la Naftali, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro, mfua shaba. Hiramu alikuwa na hekima nyingi na akili, na fundi stadi wa kazi yoyote ya shaba. Basi, alikuja kwa mfalme Solomoni, akamfanyia kazi yake yote.

Nguzo mbili za shaba za hekalu

(2Nya 3:15-17)

15Hiramu alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa mita 54, na mzingo wa mita 5.5. Ndani zilikuwa na tundu ambalo unene wa pande zake ulikuwa sentimita 2. 16Akatengeneza pia taji mbili za shaba, kila moja ikiwa na kimo cha mita 2.25; akaziweka juu ya nguzo hizo. 17Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo. 18Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo. 19Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75. 20Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji.
21Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi. 22Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika.

Tangi la shaba

(2Nya 4:2-5)

23Hiramu alitengeneza Birika liitwalo Bahari. Lilikuwa la mviringo lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, na urefu wa mita 2.25 na mzingo wa mita 13.5. 24Chini ya ukingo wake, kulizunguka tangi hilo, kulikuwa na safu mbili za vibuyu, kila kimoja mita 13.5. Vibuyu hivyo vilikuwa vimetengenezwa wakati huohuo tangi hilo lilipofanywa. 25Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili; tatu zikielekea upande wa kaskazini, tatu zikielekea magharibi, tatu kusini, na nyingine tatu mashariki. Tangi liliwekwa juu ya mafahali hao, sehemu zao za nyuma zikiwa ndani. 26Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5; nao ulikuwa ukifanana na ukingo wa kikombe na kama ua la yungiyungi. Tangi liliweza kujaa maji kiasi cha lita 40,000.

Magari ya shaba

27Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25. 28Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo, 29kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri. 30Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa. 31Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo. 32Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66. 33Hayo magurudumu yalikuwa kama magurudumu ya magari ya kukokotwa; na vyuma vyake vya katikati, duara zake, mataruma yake na vikombe vyake: Hivyo vyote vilikuwa vya kusubu. 34Chini ya kila gari kulikuwa na mihimili minne kwenye pembe zake, nayo ilishikamanishwa na gari. 35Na juu ya kila gari palikuwa na utepe uliofanyiza duara ya kimo cha sentimita 22; na vishikio na mabamba yaliyokuwa upande wa juu yalishikamana na gari lenyewe. 36Kwenye nafasi wazi iliyopatikana katika vishikio na mabamba ya kila gari, Hiramu alichonga michoro ya viumbe wenye mabawa, simba na miti ya mitende, akazungushia na mashada ya mapambo. 37Mifano hiyo yote kumi ya magari ilifanana, ikiwa na kimo kimoja na muundo uleule.
38Hiramu, pia alitengeneza mabirika kumi ya shaba, moja kwa kila gari. Kila birika ilikuwa na upana wa mita 1.75, na iliweza kuchukua maji kadiri ya lita 880. 39Akaweka magari matano upande wa kusini wa nyumba, na matano upande wa kaskazini; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba.

Vifaa vya hekalu

(2Nya 4:11–5:1)

40Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: 41Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili, 42mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo. 43Hali kadhalika, alitengeneza magari kumi, na vishikio kumi katika magari hayo; 44na tangi lile moja na sanamu za mafahali kumi na wawili, chini ya hilo tangi. 45Halafu vile vyungu, sepetu na mabirika, vyombo hivyo vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Hiramu alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. 46Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sarethani. 47Solomoni hakupima uzani wa vifaa hivi vyote kwa kuwa vilikuwa vingi sana, na kwa sababu uzani wa shaba haukujulikana.
48Solomoni alitengeneza vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Madhabahu ya dhahabu, meza ya dhahabu kwa ajili ya mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, 49vinara vya taa vya dhahabu safi vilivyowekwa mbele ya mahali patakatifu sana, vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini; maua, taa, koleo, vyote vikiwa vya dhahabu; 50vikombe, makasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, vyetezo vya kuwekea ubani, miiko ya kuchukulia moto, vyote vya dhahabu safi; bawaba za milango ya sehemu ya ndani kabisa ya nyumba – pale mahali patakatifu sana – na bawaba za milango ya ukumbi wa ibada wa hekalu bawaba zote za dhahabu.
51Basi, mfalme Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote ambayo baba yake Daudi, alikuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.



1Wafalme7;1-51


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 12 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 6....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote

Asante Mungu wetu  kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa 
majukukumu yetu...
Utukuzwe ee Mungu wetu,Mungu mwenye Nguvu,Mungu wa
walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo
Baba wa yatima,Mume wa Wajane,Baba wa Upendo
Jehovah Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Shammah..!
Jehovah Raah..!Jehovah Rapha..!Jehovah Shalom..!
Emanueli-Mungu pamoja nasi....!!!


Kulikuwa na mtu mmoja mjini Rama katika nchi ya milima ya Efraimu aitwaye Elkana wa kabila la Efraimu. Yeye alikuwa mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu. Elkana alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na wa pili Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Kila mwaka Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kuabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi kule Shilo. Huko, watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Kila wakati Elkana alipotoa tambiko alimpa mkewe Penina fungu moja la nyama ya tambiko na fungu mojamoja kwa watoto wake wa kiume na wa kike. Lakini Elkana alimpa Hana fungu moja ingawa alikuwa anampenda sana, na Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto. Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto. Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?”

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu
zote tulizo zifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,
kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu wetu usitutie katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehova tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona...


Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.” Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake. Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa. Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.” Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu. Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.” Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena.



Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa
katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema
ya kuwabariki wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
Watoto,wazazi wetu,Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba 
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Jehovah ukatupe 
macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha,Mungu wetu neema yako na Nuru yako ikaangaze 
katika maisha yetu Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya 
kutambua mema na mabaya Yahweh tunaomba ukatupe
neema ya kufuata njia zako Jehovah tukasimamie Neno
lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo Yahweh
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi......

Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.” Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri. Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.” Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya. Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu. Walipokwisha kumchinja yule fahali, walimpeleka mtoto kwa kuhani Eli. Hana akamwambia, “Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyekuwa anasimama mbele yako akimwomba Mwenyezi-Mungu. Nilimwomba anipe mtoto huyu, na yeye alinipa kile nilichomwomba. Kwa sababu hiyo, mimi ninampa Mwenyezi-Mungu mtoto huyu; wakati wote atakapokuwa hai, ametolewa kwa Mwenyezi-Mungu.” Halafu, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu hapo.




Mungu wetu tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba
kwa bidii na imani Yahweh tunaomba ukawaguse na mkono
wako wenye nguvu,Mungu wetu tunaomba ukawatendee kila
mmoja kwa hitaji/shida zake Yahweh ukatende kama 
inavyokupendeza wewe..Mungu wetu tunaomba ukawasamehe
wale wote waliokwenda kinyme nawe Baba wa Mbinguni ukawape
neema ya kujiombea na kufuata njia zako Jehovah ukawape macho
ya rohoni Baba wa Mbinguni ukawaponye kiroho na kimwili
pia,Mungu wetu ukawe tumaini lao Baba wa Minguni ukaonekane
katika mapito yao...
Jehovah tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba
ukawafute machozi ya watoto wako..
Ee Baba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukapokee sala/maombi
yetu nawe ukajibu sawasawa na mapenzi yako..
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu wetu mwenye nguvu akaguse maisha yenu..
Baraka na amani vikawafuate,Msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.



Solomoni ajenga hekalu

1Solomoni alianza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka Misri. Huo ulikuwa mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni juu ya Israeli, katika mwezi wa Zifu,6:1 Zifu: Ni mwezi wa pili katika kalenda ya Waisraeli. yaani mwezi wa pili. 2Nyumba hiyo ambayo mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na urefu wa mita 27, upana wa mita 9, na kimo cha mita 13.5. 3Ukumbi wa sebule ya nyumba ulikuwa na upana wa mita 4.5 toka upande mmoja wa nyumba mpaka upande mwingine. Na kina chake mbele ya hiyo nyumba kilikuwa mita 9. 4Aliiwekea nyumba hiyo madirisha mapana kwa ndani na membamba kwa nje. 5Pia alijenga nguzo kuzunguka, ili kutegemeza ukuta wa nje; akatengeneza na vyumba vya pembeni kila upande. 6Vyumba vya chini, katika hivyo vyumba vya nyongeza, vilikuwa na upana wa mita 2.25, na ghorofa iliyofuata ilikuwa na upana wa mita 2.75, na ghorofa ya juu kabisa ilikuwa na upana wa mita 3. Ghorofa hizo zilikuwa zimetofautiana kwa upana, kwa sababu Solomoni alikuwa amepunguza kiasi ukuta wa nje kuzunguka nyumba, ili boriti za kutegemeza jengo zisishikamane na kuta.
7Wakati nyumba ilipokuwa inajengwa, hapakusikika ndani ya nyumba mlio wa nyundo, wala wa chombo chochote cha chuma, maana ilijengwa kwa mawe yaliyokuwa yamechongwa na kutayarishwa kabisa huko yalikochukuliwa. 8Mlango wa kuingilia sehemu ya chini ya jengo lililoongezwa ubavuni mwa nyumba, ulikuwa upande wa kusini. Ndani, mlikuwa na ngazi ambayo watu waliweza kupanda ili kwenda ghorofa ya katikati na ya mwisho. 9Hivyo, Solomoni aliijenga nyumba, ikamalizika. Dari ya nyumba alikuwa ameitengeneza kwa boriti na mbao za mierezi. 10Kuuzunguka ukuta wa nje wa nyumba hiyo, alijenga vyumba vya ghorofa vyenye kimo cha mita 2.25; navyo vilikuwa vimeunganishwa na nyumba kwa boriti za mierezi. 11Wakati huo, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Solomoni, 12“Kuhusu nyumba hii unayoijenga, kama ukifuata maongozi yangu, ukayatii maagizo yangu na amri zangu, nitakutimizia mambo yote niliyomwahidi baba yako Daudi. 13Mimi nitakaa miongoni mwa wazawa wa Israeli, na sitawaacha kamwe watu wangu, Israeli.” 14Hivyo, Solomoni akaijenga nyumba na kuimaliza.

Mapambo ya ndani ya hekalu

(2Nya 3:8-14)

15Upande wa ndani wa kuta za nyumba aliufunika kwa mbao za mierezi, kutoka sakafuni mpaka kwenye boriti za dari; na sakafu akaitandika mbao za miberoshi. 16Chumba cha ndani, kilichoitwa mahali patakatifu sana, kilijengwa katika sehemu ya nyuma ya nyumba. Kilikuwa kimejengwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafuni hadi darini, na urefu wake ulikuwa mita 9. 17Nyumba ile iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu sana, ilikuwa na urefu wa mita 18. 18Mbao za mierezi zilizotanda ukuta wa nyumba kwa ndani zilikuwa zimepambwa kwa michoro ya mibuyu na maua yaliyochanua. Kila sehemu ilikuwa imefunikwa kwa mbao za mierezi, wala hapana jiwe lililoonekana.
19Katika sehemu ya ndani kabisa ya jengo hilo, Solomoni alitayarisha chumba cha pekee ambamo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwekwa. 20Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 9, upana wa mita 9, na kimo cha mita 9; nacho kilipambwa kwa dhahabu safi. Pia, alitengeneza madhabahu kwa mbao za mierezi. 21Solomoni aliipamba kwa dhahabu safi sehemu ya ndani ya nyumba, na mbele ya hicho chumba cha ndani akaweka minyororo ya dhahabu kutoka upande mmoja mpaka upande wa pili, aliipamba kwa dhahabu. 22Nyumba yote aliipamba kwa dhahabu, na madhabahu iliyokuwa katika chumba cha ndani kabisa.
23Alitengeneza kwa mbao za mizeituni sanamu za viumbe wawili wenye mabawa, kila sanamu ikiwa na kimo cha mita 4.5, akaziweka katika chumba cha ndani kabisa. 24Kila bawa lilikuwa na urefu wa mita 2.5; kwa hiyo urefu kutoka ncha ya bawa moja mpaka ncha ya bawa lingine ulikuwa mita 4.5. 25Kiumbe mwingine alikuwa na urefu wa mita 4.5; viumbe wote wawili walikuwa na vipimo vilevile na umbo lilelile. 26Urefu wa kiumbe mmoja ulikuwa mita 4.5; pia urefu wa kiumbe mwingine ulikuwa uleule. 27Sanamu hizo zilikuwa sambamba, zikiwa na mabawa yaliyokunjuliwa: Bawa la mmoja likigusa ukuta mmoja, na bawa la mwingine likigusa ukuta wa pili, huku yale mengine yaligusana katikati ya chumba. 28Nazo sanamu hizo alizipamba kwa dhahabu.
29Kuta za kila chumba alizipamba kwa kuchongwa michoro ya viumbe wenye mabawa, mitende na michoro ya maua yaliyochanua. 30Aliipaka dhahabu sakafu ya vyumba vya ndani na vya nje.
31Kwa kuingia chumba cha ndani kabisa alitengeneza milango kwa mbao za mizeituni. Vizingiti na miimo ya milango vilifanya umbo la pembe tano. 32Katika milango hiyo miwili ya mizeituni, alichora viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba michoro hiyo kwa dhahabu. 33Hali kadhalika, alitengeneza mlango wa mraba wa kuingia sebuleni. Miimo ya mlango huo ilikuwa ya mizeituni, 34na mabamba yake mawili yalikuwa ya miberoshi; kila bamba liliweza kukunjwa mara moja. 35Juu ya mabamba hayo ya mlango, kulichorwa viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba vizuri michoro hiyo kwa dhahabu. 36Alijenga ukumbi wa ndani ambao kuta zake zilikuwa za tabaka tatu za mawe yaliyochongwa, na tabaka moja la boriti za mwerezi. 37Msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ulijengwa mnamo mwezi wa Zifu6:37 mwezi wa Zifu: Mwezi wa pili. katika mwaka wa nne. 38Na katika mwezi wa Buli,6:38 Buli: Ni mwezi wa nane katika kalenda ya Waisraeli. yaani mwezi wa nane, katika mwaka wa kumi na mmoja, ujenzi wa nyumba ulimalizika, na kazi ilikuwa imekamilika kama ilivyopangwa. Ujenzi huo ulimchukua Solomoni miaka saba.


1Wafalme6;1-38


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday 9 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 5....




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwamba sisi
ni wazuri mno,si kwa uwezo wetu wala nguvu zetu,
si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii ni 
kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu.....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Muumba wetu Muumba wa vyote vilivyomo
vinavyoonekana na visivyoonekana,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,
Mungu wenye kusamehe,hakuna kama wewe,hakuna lililogumu mbele zako
wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega....!!

Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako.’ Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”


Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye alitesekakwanza ili sisi tupate kupona...

Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu baba wa Mbinguni
ukatupe sawasawa na mapenzi yako...


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
Yahweh tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu
na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
vilivyo ndani na vilivyo nje Baba wa Mbinguni ukatubariki 
tuingiapo/tutokapo Yahweh  ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama moyoni Mfalme wa amani
amani yako ikatawale katika maisha yetu,Neema na Nuru
yako ikaangaze katika maisha yetu,Yahweh ukatupe neema ya 
kufuata njia zako Mungu wetu tukasimamiE Neno lako
amri na sheria zako siku zote za maisha yetu...
Jehovah ukatupe macho ya kuona na amasikio ya kusikia
sauti yako na kuitii Mungu wetu ukaonekane popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Yahweh ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike
 kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!” Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.

Baba wa Mbinguni tazama watoto wako wanaokutafuta/
kukuhitaji kwa bidii na imani,Mungu wetu tunaomba
ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh kila mmoja kwa mahitaji/maombi yake... Mungu wetu
ukaonekane katika maisha yao Jehovah ukawape neeema
ya kujiombea,Mungu wetu ukawape neema ya kufuata njia
zako na kusimamia Neno lako Yahweh wakasikie sauti yako
Mungu wetu ukawape macho ya  rohoni Yahweh ukawaponye
kimwili na kiroho pia.....


Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha. Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.” Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya.

 Baba wa Mbinguni ukawasamehe
pale walipokwenda kinyume nawe Yahweh ukawasimamishe
na kuwaongoza Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika
maisha yao ee Baba tunaomba ukasikie na ukapokee
sala/maombi yetu Mungu wetu tunaomba ukatende
sawaswa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!


Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza
yeye,
Baraka na amani vikatawale katika maisha yenu
Nawapenda.

Solomoni ajitayarisha kujenga hekalu

(2Nya 2:1-18)

1 5:1 Kiebrania ni 5:15. Naye mfalme Hiramu wa Tiro, aliyekuwa rafiki ya Daudi, alipopata habari kwamba Solomoni amekuwa mfalme mahali pa baba yake, alituma watumishi kwake. 2Ndipo Solomoni akampelekea Hiramu ujumbe huu: 3“Wajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, hekalu la kumwabudia, kwa sababu ya kukumbana na vita vingi dhidi ya maadui wa nchi jirani mpaka hapo Mwenyezi-Mungu alipompatia ushindi. 4Lakini sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, amenijalia amani pande zote. Sina adui wala taabu. 5Basi, nimeamua kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nyumba ya kumwabudia. Na hii ni sawa kabisa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwahidi baba yangu akisema: ‘Mwanao ambaye nitamfanya aketi katika kiti chako cha enzi, atanijengea nyumba!’ 6Sasa basi, uwaamuru watu wako wanikatie mierezi ya Lebanoni. Watu wangu watajiunga na watu wako katika kazi hiyo, nami nitawalipa watumishi wako kadiri utakavyosema; kwani kama ujuavyo, hakuna yeyote mwenye ujuzi wa kukata miti kama nyinyi Wasidoni.”
7Hiramu alifurahi sana alipopata ujumbe huu wa Solomoni, akasema, “Mwenyezi-Mungu asifiwe wakati huu, kwa kumpa Daudi mwana mwenye hekima atawale taifa hili kubwa.” 8Kisha, Hiramu alimpelekea Solomoni ujumbe, akisema, “Nimepokea ujumbe wako, nami niko tayari kutimiza mahitaji yako kuhusu mbao za mierezi na za miberoshi. 9Watu wangu watasomba magogo na kuyateremsha kutoka Lebanoni mpaka baharini na kuyafunga mafungumafungu yaelee juu ya maji mpaka mahali utakaponielekeza. Huko, yatafunguliwa, nawe utayapokea. Kwa upande wako, wewe utanipa chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.”
10Basi, Hiramu alimpa Solomoni mbao zote za aina ya mierezi na miberoshi alizohitaji, 11naye Solomoni akampa Hiramu ngano madebe 240,000, na mafuta safi madebe 200 kila mwaka, kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake.
12Basi, Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni hekima kama alivyomwahidi. Kukawa na amani kati ya Solomoni na Hiramu; wakafanya mkataba kati yao.
13Mfalme Solomoni alikusanya watu 30,000 kutoka kila mahali nchini Israeli, wafanye kazi za kulazimishwa, 14akamweka Adoniramu awe msimamizi wao. Aliwagawa watu hao katika makundi matatu ya watu 10,000 kila moja, akayapeleka makundi hayo kwa zamu, mwezi mmoja Lebanoni na miezi miwili nyumbani. 15Solomoni alikuwa pia na wachukuzi wa mizigo 70,000, na wachongaji mawe milimani 80,000, 16mbali na maofisa wakuu 3,300 waliosimamia kazi hiyo na wafanyakazi wote. 17Kwa amri ya mfalme, walichimbua mawe makubwa na ya thamani, ili yachongwe kwa ajili ya kujengea msingi wa nyumba. 18Basi, hivyo ndivyo wajenzi wa Solomoni na Hiramu na watu wa mji wa Gebali walivyotayarisha mawe na mbao za kujengea nyumba hiyo.




1Wafalme5;1-18


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 8 March 2018

Heri ya siku ya wanawake Duniani..[Happy Women's Day]





Heri ya siku ya wanawake Duniani
:Mwanamke simama kwenye nafasi yako.
Usiyumbe uwe imara kwenye majukumu yako kama Mama,Mke,Dada,Shangazi ...
Pangilia muda wako vyema .
Simama kwenye maombi/sala(Imani)
Kwenye kujifunza,kujituma,kujiheshimu na kuheshimu wengine.
Tuwe jasili,nidhamu na si nidhamu ya woga.
Tuwe na misimamo makini katika maamuzi na utendaji.
Hatua moja inaanzia hapo ulipo.
Tupunguze kulalamika.
Mungu atusaidie na kutuongoza

               “Rachelsiwa “        
                           ~
       “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.” Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.” Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata. Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.” Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo. Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka. Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.””
‭‭2 Wafalme‬ ‭4:1-44

"Swahili Na Waswahili"Happy Women's Day.