Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 13 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Ruthu 2...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa uwezo wetu,wala si kwa nguvu/utashi wetu,si kwa akili zetu
wala si kwamba sisi ni wema sana zaidi ya wengine...
Ni kwa neema/rehema zako Baba ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Asifiwe Mwenyezi-Mungu Milele.!Amina..! Amina..!
Asifiwe Mwenyezi-Mungu,Mungu wa Israel,tangu milele na hata milele.!
Mwenyezi-Mungu yu hai..!Asifiwe  mwamba wa usalama wangu,Utukuzwe
Mungu wa wokovu wangu..!
Asifiwe Mwenyezi-Mungu maana hakuikataa sala yangu,
wala kuondoa fadhili zake kwangu..!
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku..! yeye hutubebea mizigo yetu,
yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu..!


Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu; anga ladhihirisha kazi ya mikono yake. Mchana waupasha habari mchana ufuatao, usiku waufahamisha usiku ufuatao. Hamna msemo au maneno yanayotumika; wala hakuna sauti inayosikika; hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote, na maneno yao yafika kingo za ulimwengu. Mungu ameliwekea jua makao yake angani; nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake, lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana. Lachomoza toka upande mmoja, na kuzunguka hadi upande mwingine; hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako ee Mungu wetu..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Jehovah tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona


Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa. Yatamanika kuliko dhahabu; kuliko dhahabu safi kabisa. Ni matamu kuliko asali; kuliko asali safi kabisa. Yanifunza mimi mtumishi wako; kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa. Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe? Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua. Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale. Hapo nitakuwa mkamilifu, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu!

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Jehovah tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah
ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mafalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu..
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu,popote tupitapo na ijulikane
kwamba upo Baba wa Mbinguni,Yahweh ukatawale,ukatamalaki na kutuatamia..Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako,Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Enyi watu wote duniani mshangilieni Mungu! Imbeni juu ya utukufu wa jina lake, mtoleeni sifa tukufu! Mwambieni Mungu: “Matendo yako ni ya ajabu mno! Nguvu zako ni kubwa mno hata maadui zako wanajikunyata kwa hofu. Dunia yote inakuabudu; watu wote wanakuimbia sifa!” Njoni mkaone mambo aliyotenda Mungu; ametenda mambo ya kutisha kati ya watu: Aligeuza bahari kuwa nchi kavu, watu wakapita humo kwa miguu; hapo nasi tukashangilia kwa sababu yake. Anatawala milele kwa nguvu yake kuu; macho yake huchungulia mataifa yote. Mwasi yeyote asithubutu kumpinga. Msifuni Mungu wetu, enyi mataifa yote; tangazeni sifa zake zipate kusikika. Yeye ametujalia maisha, wala hakutuacha tuanguke. Umetupima, ee Mungu, umetujaribu kama madini motoni. Umetuacha tunaswe wavuni; umetubebesha taabu nzito. Umewaacha watu watukanyage; tumepitia motoni na majini . Lakini sasa umetuleta kwenye usalama. Nitakuja nyumbani kwako na sadaka za kuteketezwa, nitakutimizia nadhiri zangu, nilizotamka na kukuahidi mimi mwenyewe nilipokuwa taabuni. Nitakutolea sadaka za kuteketezwa nononono, tambiko za kuteketezwa za kondoo madume; nitatoa sadaka za ng'ombe na mbuzi. Enyi mnaomcha Mungu, njoni nyote mkasikilize, nami nitawasimulieni aliyonitendea. Mimi nilimlilia msaada kwa sauti, sifa zake nikazitamka. Kama ningalinuia maovu moyoni, Mwenyezi-Mungu hangalinisikiliza. Lakini kweli Mungu amenisikiliza; naam, amesikiliza maneno ya sala yangu. Asifiwe Mungu, maana hakuikataa sala yangu, wala kuondoa fadhili zake kwangu.

Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa,Mungu wetu ukawape nguvu,uvumilivu wanaowauguza,,Baba wa Mbinguni ukawatendee 
Wajane na Yatima, Mungu wetu ukawavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Yahweh ukawafungue na kuwaweka huru wale waliokatika vifungo vya yule mwovu Jehovah haki ikatendeke
kwa walio magerezani pasipo na hatia..Mungu wetu ukawasamehe na kuwasimamisha tena wale wote walikwenda kinyume nawe/walioanguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wote walioelemewa na mizigo Mungu wetu ukawape chakula wenye njaa
Baba wa Mbinguni ukawafariji wafiwa,Mungu wetu ukaonekane katika
shida/tabu za watoto wako,Jehovah ukasikie kulia kwao,Baba ukawafute
machozi ya watoto wako,Mungu wetu ukasikie,ukapokee na kujibu Sala/maombi yetu,Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
wote wanao kuomba kwa bidii/imani Ee Baba tunaomba utusikie..


Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde. Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni. Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa. Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote! Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa. Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara. Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba.

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana,Mungu wa upendo
aendelee kuwabariki,Amani iwe nanyi pendo lenu likadumu
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Baba wa Mbinguni
akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Ruthu anafanya kazi katika shamba la Boazi

1Naomi alikuwa na ndugu aliyeitwa Boazi, wa ukoo wa Elimeleki mumewe. Huyo alikuwa mtu mashuhuri na tajiri. 2Siku moja, Ruthu Mmoabu alimwambia Naomi, “Niruhusu niende shambani kukusanya masalio ya mavuno. Nina hakika kumpata mtu ambaye ataniruhusu niokote nyuma yake.” Naomi akamwambia, “Haya, nenda binti yangu.”
3Basi Ruthu akaenda shambani, akawafuata wavunaji huku anayaokota masuke waliyoyaacha. Na kumbe akajikuta katika shamba la Boazi, yule wa ukoo wake Elimeleki.
4Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.” 5Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?” 6Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu. 7Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.”
8Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; 9angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.”
10Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?”
11Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. 12Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.”
13Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.”
14Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza. 15Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee. 16Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.”
17Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi. 18Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa. 19Basi mkwewe akamwuliza, “Uliokota wapi haya yote? Je, ulikuwa katika shamba la nani? Heri huyo aliyekufadhili.” Hapo Ruthu akamwambia Naomi kwamba alikuwa amefanya kazi katika shamba la mtu aliyeitwa Boazi. 20Basi, Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi-Mungu ambariki Boazi! Mungu hutimiza daima ahadi zake kwa walio hai na waliokufa.” Kisha akaendelea kusema, “Huyo mtu ni ndugu yetu wa karibu na ni mmoja wa wale wenye wajibu wa kututunza.”
21Kisha Ruthu Mmoabu akasema, “Isitoshe, aliniambia nijiunge pamoja na wafanyakazi wake mpaka wamalize mavuno yote.”
22Basi, Naomi akamwambia Ruthu, “Naam binti yangu. Ni vyema kufanya kazi pamoja na wanawake wengine katika shamba la Boazi, kwa maana labda ungesumbuliwa kama ungekwenda katika shamba la mtu mwingine.” 23Kwa hiyo, Ruthu akafanya kazi nao, akaokota masuke mpaka mavuno ya ngano na shayiri yalipomalizika. Wakati huo wote alikuwa anakaa na mama mkwe wake.

Ruthu2;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Tuesday 12 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Tumemaliza kitabu cha Waamuzi-Tunaanza Kitabu cha Ruthu Mungu yu mwema...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana,Tunamshukuru Mungu kwakumaliza
kitabu cha "Waamuzi"na Leo tunaanza Kitabu cha "Ruthu"
Mungu akatupe kibali cha kusoma na kuelewa,akatupe macho
ya rohoni,tusomapo tukapate kuelewa na kujifunza zaidi,ikawe
faida kwetu na kwa wengine,Tukawe na kiu,shahuku ya kujifunza
zaidi..Ee Mungu wetu utusaidie...!!

Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.”
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa uzima/pumzi,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii
Utukuzwe Ee-Mwenyezi Mungu..!Unifundishe masharti yako..
Utukuzwe Ee Mwenyezi-Mungu..!kwa sababu ya nguvu yako tutaimba
na kuusifu uwezo wako..
Utukuzwe Ee Mwenyezi-Mungu..!juu ya Mbingu  Utukufu wako uenee duniani kote..
Utukuzwe Ee Mwenyezi-Mungu...!Milele na Milele..!
Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe..!


Watu wa Israeli walipotoka Misri, wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini, Yuda ikawa maskani ya Mungu, Israeli ikawa milki yake. Bahari iliona hayo ikakimbia; mto Yordani ukaacha kutiririka! Milima ilirukaruka kama kondoo dume; vilima vikaruka kama wanakondoo! Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia? Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka? Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume? Nanyi vilima, mmerukaje kama wanakondoo? Tetemeka, ee dunia mbele yake Mwenyezi-Mungu; tetemeka mbele ya Mungu wa Yakobo, anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji, nayo majabali yakawa chemchemi za maji!
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako ...
Mungu wetu tunaomba utusamehe Dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

“Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu Semeni nyote mlio katika Israeli: “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu, wakati ule tuliposhambuliwa na maadui, hakika tungalimezwa tukiwa hai, wakati hasira zao zilipotuwakia. Tungalikumbwa na gharika, tungalifunikwa na mto wa maji, mkondo wa maji ungalituchukua!” Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, ambaye hakutuacha makuchani mwao. Tumeponyoka kama ndege mtegoni; mtego umeteguliwa, nasi tukaokoka. Msaada wetu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Jehovah tunaomba
ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji Baba tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe
kama inavyokupendeza wewe..

Mafalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Jehovah
tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatuguse kwa mkono
wako wenye nguvu Baba wa Mbinguni tukapate kutambua/kujitambua
Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako,Kusimamia Neno lako
amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona, masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii,Yahweh ukatubariki tuingiapo/tutokapo..
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu,popote tupitapo
na ijulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Ukatufanye chombo chema Baba wa mbinguni nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Nilifurahi waliponiambia: “Twende nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.” Sasa tuko tumesimama, kwenye malango yako, ee Yerusalemu! Yerusalemu, mji uliojengwa, ili jumuiya ikutane humo. Humo ndimo makabila yanamofika, naam, makabila ya Israeli, kumshukuru Mwenyezi-Mungu kama alivyoagiza. Humo mmewekwa mahakama ya hukumu ya haki, mahakama ya ukoo wa kifalme wa Daudi. Uombeeni Yerusalemu amani: “Wote wakupendao na wafanikiwe! Ndani ya kuta zako kuwe na amani, majumbani mwako kuweko usalama!” Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu, ee Yerusalemu, nakutakia amani! Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ninakuombea upate fanaka!

Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wasumbakao na kuelemewa na mizigo,Mungu wetu tunaomba uponyaji kwa wagonjwa Yahweh ukawape nguvuna uvumilivu wanaowauguza...
Yahweh tunaomba ukabariki mashamba/kazi Mungu wetu ukawape chakula cha kutosha na kuweka akiba  wenye njaa..
Baba wa mbinguni utaomba ukawaweke huru wale walio katika vifungo
vya yule mwovu,Mungu wetu haki ikatendeke kwa wote waliovifungoni
pasipo na hatia,Baba wa Mbinguni ukawasimamishe na kuwarudisha
wale wote walioanguka/potea Baba ukawasamehe wale wote waliokwenda
kinyume nawe,Mungu wetu ukawafariji wafiwa,Mfalme wa amani
ukatawale,ukabariki,ukasikie,ukapokee,ukajibu sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu Baba..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukiufu hata Milele....
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami..
Pendo lenu likadumu,Amani ikatawale maishani mwenu,Nuru ikaangaaze
katika nyumba zetu,Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ikawafunike..
Nawapenda.

Elimeleki na jamaa yake wanakwenda Moabu

1Hapo zamani, wakati waamuzi walipokuwa wanatawala Israeli, palitokea njaa nchini humo. Mtu mmoja kutoka Bethlehemu katika Yuda pamoja na mkewe na watoto wao wa kiume wawili walikwenda kuishi kwa muda nchini Moabu ili kuishi kama wageni. 2Mtu huyo aliitwa Elimeleki na mkewe aliitwa Naomi. Watoto wao wawili wa kiume, mmoja aliitwa Mahloni na mwingine Kilioni. Mtu huyo na jamaa yake walikuwa Waefrathi wa huko Bethlehemu katika Yuda. Walikwenda nchini Moabu, wakakaa huko. 3Lakini Elimeleki, mumewe Naomi, alifariki na Naomi akaachwa na wanawe wawili. 4Vijana hao walioa wasichana wa Kimoabu, Orpa na Ruthu. Baada ya miaka kumi hivi, 5Mahloni na Kilioni nao pia walifariki.

Naomi na Ruthu wanarudi Bethlehemu

6Baadaye, Naomi alipata habari kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amewabariki watu wake kwa kuwapa chakula. Basi, akaondoka kutoka Moabu kurudi kwao pamoja na wakwe zake. 7Akaondoka mahali pale alipoishi pamoja na wakwe zake, wakashika njia ya kurudi Yuda. 8Naye Naomi akawaambia hao wakwe zake wawili, “Rudini kila mmoja nyumbani kwa mama yake. Naomba Mwenyezi-Mungu awe mwema kwenu kama mlivyokuwa wema kwangu na kwa wale watu wangu waliofariki. 9Mwenyezi-Mungu awajalie, kila mmoja wenu apate mume na nyumba yake.” Kisha Naomi akawaaga kwa kuwabusu. Lakini wao walianza kulia kwa sauti 10na kumwambia, “La hasha! Tutakwenda pamoja nawe kwa watu wako.”
11Naye Naomi akawasihi, “Rudini, binti zangu. Kwa nini kunifuata? Je, mnafikiri naweza kupata tena watoto watakaokuwa waume zenu? 12Rudini nyumbani kwenu binti zangu, kwa maana mimi ni mzee mno, siwezi kuolewa tena. Hata kama ningesema ninalo tumaini, na hata kama ningepata mume usiku huu na kupata watoto, 13je, mngeweza kungoja mpaka wakue? Je, mngeweza kujizuia msiolewe na waume wengine? Sivyo, binti zangu! Mambo yangu ni magumu mno kwa ajili yenu, maana Mwenyezi-Mungu amenipiga kipigo.”
14Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. 15Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.”
16Lakini Ruthu akamjibu,
“Usinisihi nikuache wewe,
wala usinizuie kufuatana nawe.
Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda,
na ukaapo nitakaa,
watu wako watakuwa watu wangu,
na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.
17Pale utakapofia hapo nitakufa nami,
na papo hapo nitazikwa;
Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe
isipokuwa tu kwa kifo.”
18Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi. 19Ndipo wote wawili wakaendelea na safari hadi Bethlehemu. Walipofika huko, watu wote walishangaa, hata wanawake wakaulizana, “Je, huyu ni Naomi?”
20Naomi akasema, “Msiniite tena Naomi1:20 Naomi: Maana yake: Mwema. niiteni Mara,1:20 Mara: Maana yake: Mwenye uchungu. kwa maana Mungu mwenye nguvu ameyafanya maisha yangu yawe machungu mno. 21Nilipoondoka hapa, nilikuwa na vitu vingi, lakini sasa Mwenyezi-Mungu amenirudisha mikono mitupu. Mbona mwaniita Naomi na hali Mwenyezi-Mungu ameniadhibu, naye Mungu Mwenye Nguvu amenitesa.”
22Hivyo ndivyo Naomi pamoja na Ruthu Mmoabu, mkwewe, walivyorejea kutoka Moabu, na kuwasili Bethlehemu wakati uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.


Ruthu1;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 11 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 21...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametupa kibali cha kuendelea
kuiona Leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante Mungu Baba kwa Ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh,
Uabudiwe Daima,Unatosha Mungu wetu,Matendo yako ni makuu sana,
Matendo yako ni ya ajabu,Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..

Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani. Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Ya nini hasara hii? Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.” Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.”
Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku
nyingine Jehovah..
Mfalme wa amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Mungu Baba..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu, hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana. Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe,
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Yahweh tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Jehovah nasi tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tuaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh utusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe..

Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu, hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana. Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe,

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukatupe uponyaji wa moyoni,amani ikatawale katika maisha
yetu,ukatupe neema ya hekima,busara,upendo na vyote vinavyokupendeza wewe..
Ukatupe macho ya rohoni,masikio ya kusikia sauti yako na kutii
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno
lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatende
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katka yoye Baba na tukawe na kiasi..


Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu. Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.

Baba wa Mbinguni tazama wenye shida/tabu yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa Yahweh tazama wenye njaa Baba tunaomba ukawapatie chakula cha kutosha na kuweka akiba,Mungu wetu tazama Yatima na Wajane Baba tunaomba ukawaguse na kuwatendea,Mungu wetu tunaomba ukawavushe salama wote wanaopoitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawafungue na kuwaweka huru wale waliokatika vifungo vya yule mwovu Mungu wetu walio magerezani pasipo na hatia Mungu wetu tunaomba haki ikatendeke..
Yahweh  tunaomba ukawape tumaini wale wote waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,Mungu wetu ukaonekane kwa wote wanaokutafuta Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe..Mungu wetu tunaomba ukasikie,ukapokee,ukajibu sala/maobi yetu
Yahweh ukawatendee sawasawa na mapenzi yako watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Baba wa Mbinguni akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake,Amani ya kristo Yesu iwe nanyi Daima...
Nawapenda.

Kuchipuka tena kwa kabila la Benyamini

1Waisraeli walikuwa wameapa huko Mizpa kwamba hakuna hata mmoja wao ambaye angemwachia binti yake aolewe kwa watu wa kabila la Benyamini. 2Basi, wakaenda mpaka Betheli wakakaa huko mbele ya Mungu hadi jioni. Wakapaza sauti na kulia kwa uchungu mwingi. 3Wakasema “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limetukia hata tupungukiwe na kabila katika Israeli?” 4Kesho yake watu waliamka mapema, wakajenga madhabahu, wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. 5Kisha wakaulizana, “Je, miongoni mwa makabila yote ya Israeli kuna kikundi chochote ambacho hakikuhudhuria mkutano uliofanyika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Walikuwa wamefanya kiapo kwamba mtu yeyote ambaye hatahudhuria mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa ni lazima auawe. 6Lakini Waisraeli wakawaonea huruma ndugu zao wa kabila la Benyamini, wakasema, “Leo kabila moja la Israeli limeangamia. 7Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wake hao wanaume wa kabila la Benyamini waliosalia? Maana tulikwisha apa kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hatutawapa binti zetu wawe wake zao!” 8Wakataka kujua kama kulikuwa na kikundi chochote cha makabila ya Israeli ambacho hakikuhudhuria mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Wakagundua kwamba hakuna mtu yeyote kutoka Yabesh-gileadi aliyekuja kwenye mkutano huo. 9Waisraeli walipohesabiwa huko Mizpa hakuna mkazi yeyote wa Yabesh-gileadi aliyehudhuria. 10Hivyo jumuiya ya Israeli ikapeleka watu wake 12,000 walio hodari kabisa na kuwaamuru: “Nendeni mkawaue wakazi wa Yabesh-gileadi; wanawake pamoja na watoto. 11Mtawaua wanaume wote na wanawake wote wasio mabikira.” 12Basi wakakuta miongoni mwa wakazi wa Yabesh-gileadi wasichana 400 ambao hawakuwa wamelala na mwanamume yeyote, wakawapeleka kambini huko Shilo katika nchi ya Kanaani.
13Kisha jumuiya nzima ikawapelekea ujumbe wa amani watu wa kabila la Benyamini ambao walikuwa kwenye mwamba wa Rimoni. 14Wanaume hao wa kabila la Benyamini wakawarudia hao wenzao wakati huohuo. Basi wakapewa wale wanawake ambao walikuwa wamesalimishwa huko Yabesh-gileadi. Lakini wanawake hao hawakuwatosha. 15Waisraeli wakawaonea huruma watu wa kabila la Benyamini, maana Mwenyezi-Mungu alisababisha kuweko na mwanya katika Israeli.
16Kisha wazee wa jumuiya nzima wakasema, “Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wanawake hao wanaume waliosalia kwa vile wanawake wote wa kabila la Benyamini waliangamia? 17Lazima wanaume waliosalia wa kabila la Benyamini wapewe wanawake ili waendeleze kabila, na hivyo kusipotee kabila lolote katika Israeli. 18Lakini hatuwezi kuwatoa binti zetu wawe wake zao, maana tulikwisha apa kwamba mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa mwanamume wa kabila la Benyamini alaaniwe.” 19Basi wakakumbuka kwamba sikukuu ya Mwenyezi-Mungu iliyofanyika kila mwaka huko Shilo, mji ulio kaskazini ya Betheli, kwenye njia kuu itokayo Betheli kwenda Shekemu, ilikuwa inakaribia. 20Kwa hiyo wakawaamuru wale wanaume wa kabila la Benyamini, “Nendeni mkavizie na kuotea katika mashamba ya mizabibu.” 21Muwe macho. Wasichana wa Shilo watakapotoka nje kucheza wakati wa sikukuu, tokeni kwenye mizabibu na kila mtu ajinyakulie msichana mmoja awe mkewe. Kisha mrudi katika nchi ya Benyamini. 22Baba zao au kaka zao wakija kutulalamikia tutawaambia, “Sisi tunawaombeni mwahurumie watu wa Benyamini na kuwaachia wawachukue hao wanawake; maana hatukuwapata katika vita vya Yabesh-gileadi. Na kwa vile nyinyi wenyewe hamkutupatia hao binti zenu, hamtahukumiwa.” 23Wale wanaume wa kabila la Benyamini wakafanya hivyo, kila mmoja akajichagulia msichana miongoni mwa wasichana waliotoka nje kucheza huko Shilo na kumchukua kuwa mkewe. Kisha wakarudi katika eneo lao, wakaijenga miji yao upya na kuishi humo. 24Wakati huohuo Waisraeli wakaondoka, kila mtu akarudi katika eneo la kabila lake na jamaa yake. Kila mtu alirudi katika sehemu aliyogawiwa. 25Siku hizo hapakuwepo na mfalme katika Israeli. Kila mtu alifanya kama alivyoona kuwa sawa.



Waamuzi 21;1-25


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday 8 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 20...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru kwa kila jambo..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
si kwa nguvu zetu,wala si kwa akili zetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana,wala si kwa utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Ni kwa neema/rehema,ni kwa mapenzi yako Mungu wetu..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah
Uabudiwe daima,Tunakushuru Mungu wetu,Matendo yako ni makuu mno..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu....!!

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu,..
Yahweh tnaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya...
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea,Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.” Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu , naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani. Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali kabisa. Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu. Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia na siri ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni makanisa saba.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyo kupendeza wewe..


Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu tunaomba
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,Baba ukatupe amani ya moyo,
utuwema,fadhili,upendo kati yetu ukadumu,furaha,tupate kufarijiana
kusaidiana,kusameheana,kuhurumiana,kuonyana/kuelimishana kwa 
upendo na upole...
Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba
wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu..
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ijulikane
kwamba upo Baba wa Mbinguni,tukanene yaliyo yako..

Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




“Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika: “Mimi nishikaye zile nyota saba katika mkono wangu wa kulia na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu, nasema hivi: Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo. Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: Wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa mahali pake. Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: Wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi. “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Mshindi nitamjalia kula matunda ya mti wa uhai ulioko ndani ya bustani ya Mungu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwamkono wako wenye nguvu
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba
ukawavushe salama,Yahweh wagonjwa tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia Jehovah ukawape nguvu na moyo wale wanaouguza,Yahweh
tunaomba ukawape chakuka na ukabariki mashamba/kazi zao wenye njaa..Mungu wetu ukawape tunaini wale wote wenye hofu,mashaka,waliokataliwa,waliokata tamaa,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasimamishe na kuwarudisha wale wote walioanguka,walioptea/waliorudinyuma,Mungu wetu tunaomba ukawafungue na kuwaweka huru wale wote walio katika vifungo vya
yule mwovu na wale wote walio magerezani pasipo na hatia na haki ikatendeke...
Yahweh tunaomba ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia
zako,BABA tunaomba ukasikie kulia kwao Mfalme wa amani ukawafute machozi yao,Jehovah tunaomba ukapokee sala/maombi ya watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani..
Ee Mungu wetu tunaomba ukasike,ukapokee,ukajibu na ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo
Baraka,amani viwe nanyi daima..
Nawapenda.



Vita vya kuwaadhibu watu wa Benyamini

1Watu wote wa Israeli, kutoka Dani hadi Beer-sheba, pamoja na watu wa nchi ya Gileadi, jumuiya nzima, walikusanyika huko Mizpa, mbele ya Mwenyezi-Mungu. 2Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakajitokeza mbele ya mkusanyiko wa watu wa Mungu. Wote, jumla walikuwa askari wa miguu wenye silaha 400,000. 3Nao watu wa kabila la Benyamini, wakapata habari kwamba watu wale wengine wa Israeli walikuwa wamekusanyika huko Mizpa.
Basi Waisraeli wakamwuliza yule mwanamume Mlawi “Tueleze, uovu huo ulifanyikaje?” 4Yule Mlawi, mume wa yule suria, akawajibu, “Mimi na suria wangu tulifika mjini Gibea, mji wa kabila la Benyamini ili tulale huko usiku. 5Lakini watu wa mji wa Gibea wakaja usiku wakaizingira nyumba nilimokuwa nimelala. Walitaka kuniua, wakambaka suria wangu mpaka akafa. 6Mimi nikachukua maiti yake, nikamkatakata vipandevipande na kuvipeleka kwa makabila yote ya Israeli, maana wamefanya jambo la kuchukiza na potovu katika Israeli. 7Sasa enyi Waisraeli, shaurianeni na toeni uamuzi wenu.”
8Watu wote kwa pamoja, wakasimama na kusema, “Hakuna yeyote kati yetu atakayerudi hemani kwake au nyumbani kwake. 9Hivi ndivyo tutakavyofanya kuhusu Gibea: Tutapiga kura namna ya kuwashambulia. 10Tutachagua watu kumi katika kila watu mia moja wa Israeli, watu mia moja katika kila watu elfu moja, watu elfu moja katika kila watu elfu kumi. Hao watakuwa na jukumu la kuwaletea chakula wenzao watakaokuwa na kazi ya kuuadhibu mji wa Gibea katika nchi ya Benyamini kwa uhalifu wao na upotovu walioufanya katika Israeli.” 11Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa moyo mmoja dhidi ya mji wa Gibea.
12Watu wa makabila ya Israeli wakatuma wajumbe mpaka kila sehemu ya kabila la Benyamini, wakisema, “Je, ni uovu gani huu uliotukia miongoni mwenu? 13Sasa tupeni hao watu mabaradhuli wa Gibea ili tuwaue na kutokomeza uovu huu kutoka Israeli.” Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwasikiliza ndugu zao, Waisraeli. 14Basi walikusanyika huko Gibea kutoka katika kila mji wao, ili kupigana na Waisraeli. 15Watu wa kabila la Benyamini walikusanya kutoka miji yao jeshi la watu 26,000 wenye kutumia silaha, nao wakazi wa mji wa Gibea wakakusanya watu 700 waliochaguliwa. 16Kati ya watu hao waliochaguliwa kulikuwa na watu 700 waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja aliweza kurusha jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosea. 17Waisraeli, licha ya wa kabila la Benyamini, walikusanya watu 400,000 wawezao kutumia silaha. Wote walikuwa hodari wa vita.
18Waisraeli wakaenda Betheli kutaka shauri kwa Mungu, wapate kujua kabila ambalo litakwenda kwanza kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Mwenyezi-Mungu alitaja kabila la Yuda liende kwanza. 19Basi, Waisraeli wakaenda asubuhi, wakapiga kambi yao karibu na mji wa Gibea. 20Waisraeli wakatoka kupigana na watu wa kabila la Benyamini karibu na Gibea. 21Watu wa kabila la Benyamini wakatoka nje ya mji wa Gibea wakapigana na Waisraeli, wakawaangusha chini siku hiyo, watu wa Israeli 22,000. 22Lakini Waisraeli wakajipa moyo, wakajipanga tena kwa vita mahali pale walipojipanga kwa mara ya kwanza. 23Basi Waisraeli wakaenda juu, wakamlilia Mwenyezi-Mungu mpaka jioni. Kisha wakaomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu: “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Nendeni mkapigane nao.”
24Hivyo siku ya pili Waisraeli wakakaribia kupigana na watu wa kabila la Benyamini. 25Siku hiyo ya pili watu wa kabila la Benyamini walitoka Gibea na kuwashambulia Waisraeli, wakawaangusha chini Waisraeli 18,000. 26Watu wote wa jeshi la Waisraeli wakaenda Betheli. Walikaa huko mbele ya Mwenyezi-Mungu wakiomboleza na kufunga mpaka jioni. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. 27Waisraeli wakamwomba Mwenyezi-Mungu awape shauri. Wakati huo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa huko Betheli. 28Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni alikuwa na wajibu wa kuhudumu mbele yake. Waisraeli wakamwuliza Mwenyezi-Mungu, “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, watu wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Nendeni. Kesho nitawatia mikononi mwenu.”
29Hivyo, Waisraeli wakaweka watu mafichoni kuuzunguka mji wa Gibea. 30Waisraeli wakaenda kupigana na watu wa kabila la Benyamini katika siku ya tatu. Wakajipanga dhidi ya mji wa Gibea kama walivyofanya nyakati za hapo awali. 31Kisha watu wa kabila la Benyamini walipotoka mjini kuanza kupigana na Waisraeli, walivutwa kutoka nje ya mji. Ilitokea tena kama walivyofanya nyakati za hapo awali wakawaua baadhi ya watu wa Israeli kwenye njia kuu zielekeazo miji ya Betheli na Gibea, mpaka mbugani. Waliua Waisraeli wapatao thelathini. 32Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.” 33Hivyo watu wote wa Israeli wakatoka kwenye sehemu yao na kujipanga tena huko Baal-tamari. Wenzao waliokuwa wanaotea wakatoka haraka mahali pao upande wa magharibi20:33 magharibi: Makala ya Kiebrania: Mbugani. wa mji wa Gibea. 34Askari hodari waliochaguliwa kutoka makabila yote ya Israeli wakawasili hapo mbele ya mji wa Gibea. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Lakini watu wa Benyamini hawakufahamu kwamba kuangamia kwao kulikuwa karibu. 35Mwenyezi-Mungu aliwashinda watu wa Benyamini mbele ya Waisraeli. Waisraeli wakawaua watu wa Benyamini 25,100. Hao wote waliouawa walikuwa askari walioweza kutumia silaha. 36Hivyo watu wa kabila la Benyamini wakaona kwamba wameshindwa.
Waisraeli walirudi nyuma kana kwamba wanawakimbia watu wa kabila la Benyamini, kwani walitegemea wenzao waliokuwa wamewekwa kuotea mji wa Gibea. 37Wale waliowekwa kuuotea mji walitoka haraka na kuushambulia mji wa Gibea na kuwaua wote waliokuwamo kwa upanga. 38Walikuwa wamekubaliana na wale watu wengine wa Israeli juu ya ishara moja. Walikubaliana kwamba wale waliokuwa wanaotea watakapoona moshi mkubwa unapanda juu kutoka mjini, 39basi, waushambulie mji. Wakati huo, watu wa kabila la Benyamini walikuwa tayari wameua watu wapatao thelathini wa Israeli na kuambiana, “Tumewapiga kama hapo awali.” 40Lakini ile ishara ya mnara wa moshi ilipoanza kutokea katika mji, watu wa kabila la Benyamini walipotazama nyuma yao, wakashangaa kuona kwamba mji wao ulikuwa unateketezwa moto. 41Ndipo Waisraeli wakageuka, na watu wa kabila la Benyamini wakakumbwa na fadhaa kwani sasa waliona kuwa kuangamia kwao kulikuwa kumekaribia. 42Kwa hiyo wakageuka, wakawakimbia Waisraeli kuelekea jangwani, lakini vita vikawakumba; wakajikuta wako katikati ya majeshi mawili ya Israeli, na askari waliotoka wakawaangamiza. 43Waisraeli waliwazingira watu wa kabila la Benyamini, wakawafuatia kutoka Noha20:43 Noha: Makala ya Kiebrania: Mahali pao pa kupumzikia. hadi mashariki ya mji wa Gibea wakiwaua wengi wao. 44Siku hiyo watu 18,000 wa kabila la Benyamini, wote askari hodari, waliuawa. 45Watu wengine wa kabila la Benyamini waligeuka, wakakimbia kuelekea jangwani hadi mwamba wa Rimoni. Wengine 5,000 waliuawa kwenye njia kuu walipokuwa wanakimbia. Waisraeli waliendelea kuwafuatia vikali watu wa kabila la Benyamini hadi mji wa Gidomu wakawaua watu 2,000. 46Jumla ya watu wote wa kabila la Benyamini waliouawa siku hiyo ilikuwa 25,000, askari hodari wa kutumia silaha. 47Lakini wanaume 600 wa kabila la Benyamini walifaulu kukimbilia jangwani hadi kwenye mwamba wa Rimoni, wakakaa huko kwa muda wa miezi minne. 48Waisraeli wakawageukia watu wengine wa kabila la Benyamini, wakawaua wote: Wanaume, wanawake, watoto na wanyama. Na miji yote waliyoikuta huko wakaiteketeza moto.


Waamuzi 20;1-48

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.