Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 20 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 9...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali
cha kuiona leo hii,Si kwamba tumetenda mema sana,wala si kwamba
sisi ni wazuri mno,wala si kwa nguvu/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo
ni kwa neema/rehema zake Mungu wetu..

Tumshukuru Mungu wetu kwa yote aliyotutendea/anayoendelea kututendea..





Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja. Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.” Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?” Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”
Asante Mungu Baba kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kwakuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbingu,Usifiwe ee Baba,
Uabudiwe Jehovah,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,hakuna kama wewe Mungu wetu,Unatosha Mfalme wa Amani..





Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: ‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike, nitawamiminia Roho wangu siku zile, nao watatoa unabii. Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’ “Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. Maana Daudi alisema juu yake hivi: ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia hata sitatikisika. Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini, maana hutaiacha roho yangu kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. Umenionesha njia za uhai, umenijaza furaha kwa kuwako kwako!’


Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku
nyingine Jehovah..!
Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza,tukijishusha
na tukijiachilia mikononi mwako Yahweh..
Baba tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti...





“Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’ Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia. Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’ “Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.” Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?” Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu. Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.” Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.” Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao 3,000 wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo. Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali.


Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wengine..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe
sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale Nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbingu uwepo wako uwe nasi,Baraka na furaha zitufuate,
utu wema na fadhili,unyenyekevu ,busara,hekima na upole kiasi
viwe nasi, huruma,kusaidia na kuonyana kwa upendo..
ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako
Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..





Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu. Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawiana. Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja. Waliendelea kukutana pamoja kila siku hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu. Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.
Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wote
wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu
mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu,walioanguka/potea
Mungu wetu tunaomba uwasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
ukawaponye kimwili na kiroho,ukapokee maombi/sala za watoto wako
ukasikie kulia kwao na ukawafute machozi yao,ukawape neema ya kujiombea na kukutafuta wewe,Nuru/mwanga ukaangaze tena kwenye maisha yao,Imani yao kwako ikawaponye na kuwaweka huru..
Amani ya moyo,furaha na baraka ziwe nao..
ee Baba ukapokee sala/maombi yetu..
Tunakushukuru na kukusifu Daima..
tukiamini wewe ni Mungu wetu,Mungu wetu si kipofu unaona,Mungu wetu si kiziwi unasikia,Mungu wetu si bubu Unajibu na kutenda kama
inavyokupendeza wewe..


Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!



Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Mungu muweza wa yote awe nanyi daima..
Amani ya Kristo iwe nanyi wakati wote..
Nawapenda.

Agano na watu wa Gibeoni

1Wafalme wote waliokuwa ngambo ya mto Yordani katika nchi ya milimani na kwenye tambarare na eneo lote la pwani ya bahari ya Mediteranea kuelekea Lebanoni, Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, waliposikia habari za Waisraeli, 2wakakusanyika pamoja kwa nia moja ili kupigana vita na Yoshua na Waisraeli.
3Lakini wakazi wa Gibeoni walipopata habari juu ya jinsi Yoshua alivyoitenda miji ya Yeriko na Ai, 4waliamua kutumia hila. Wakatayarisha vyakula, wakapakiza magunia yaliyochakaa juu ya punda wao, viriba vilivyochakaa na kushonwa; 5wakavaa viatu, nguo zilizochakaa na vyakula vyao vyote vilikuwa vikavu vilivyoota ukungu. 6Basi, wakamwendea Yoshua kambini Gilgali, wakamwambia yeye na Waisraeli, “Sisi tumetoka nchi ya mbali; tafadhali tunaomba mfanye agano nasi.”
7 Taz Kut 23:32; 34:12, Kumb 7:2 Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.” 8Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?” 9Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri. 10Taz Hes 21:21-35 Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi. 11Ndipo wazee wetu na wananchi wote wa nchi yetu, wakatuambia, tuchukue posho ya safari, tuje kukutana nanyi na kuwaambia kwamba sisi ni watumishi wenu; tafadhali fanyeni agano nasi. 12Tazama mikate yetu ambayo ilikuwa bado moto tulipoichukua wakati tulipoondoka kwetu, lakini sasa imekauka na kuota ukungu. 13Viriba hivi tulivijaza maji vikiwa vipya, lakini sasa vimepasukapasuka. Hata mavazi na viatu vyetu vimechakaa, kwani safari ilikuwa ndefu sana.”
14Hivyo, Waisraeli wakachukua vyakula vyao, bila ya kumwuliza shauri Mwenyezi-Mungu. 15Yoshua akafanya nao mkataba wa amani; akafanya agano kwamba atawaruhusu kuishi. Viongozi wa jumuiya ya Israeli wakawaapia kutekeleza mapatano hayo.
16Siku tatu baada ya kufanya agano nao, Waisraeli wakagundua kwamba watu hao walikuwa jirani zao na waliishi miongoni mwao. 17Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu. 18Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao. 19Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru. 20Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula. 21Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema.
22Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu? 23Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”
24Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili. 25Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.” 26Basi, alilowatendea ni kuwaokoa mikononi mwa Waisraeli ili wasiangamizwe; hivyo hawakuwaua. 27Lakini kutoka siku hiyo, Yoshua aliwafanya hao kuwa wakata-kuni na wachota-maji kwa ajili ya jumuiya nzima ya Waisraeli na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, popote pale Mwenyezi-Mungu alipochagua mpaka hivi leo.



Yoshua 9;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 19 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 8...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!!Mungu wetu yu mwema sana.

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..!
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Muumba wa Vyote vilivyomo,Muumba wa vyote vinavyoonekana
 na visivyo onekana..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye huruma..
Baba wa upendo,Baba wa faraja,Baba wa baraka,Baba wa Yatima..
Mume wa wajane,Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye uponyaji..
Muweza wa yote,Alfa na Omega,Hakuna kama wewe,Unatosha Mungu wetu
Utukuzwe Yahweh,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unastahili kuhimidiwa,Unastahili kuheshimiwa,Unastahili ee Baba....!


“Wastahili ee Bwana na Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu. Maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.”

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena  na kutupa kibali cha kuendelea kuiona
leo hii..
Asante kwa afya,uzima/pumzi na tukiwa tayari kuendelea na majukumu yetu..

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako  Jehovah..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..



Enyi Waisraeli, mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mmejikwaa kwa sababu ya uovu wenu. Ombeni toba kwake, mrudieni na kumwambia: “Utusamehe uovu wote, upokee zawadi zetu, nasi tutakusifu kwa moyo. Ashuru haitatuokoa, hatutategemea tena farasi wa vita. Hatutaviita tena: ‘Mungu wetu’ hivyo vinyago tulivyochonga wenyewe. Kwako ee Mungu yatima hupata huruma.” Mwenyezi-Mungu asema, “Nitaponya utovu wao wa uaminifu; nitawapenda tena kwa hiari yangu, maana sitawakasirikia tena. Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli nao watachanua kama yungiyungi, watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni. Chipukizi zao zitatanda na kuenea, uzuri wao utakuwa kama mizeituni, harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni. Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu, watastawi kama bustani nzuri. Watachanua kama mzabibu, harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni. Enyi watu wa Efraimu, mna haja gani tena na sanamu? Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu, mimi ndiye ninayewatunzeni. Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi, kutoka kwangu mtapata matunda yenu. Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya, mtu aliye na busara ayatambue. Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu; watu wanyofu huzifuata, lakini wakosefu hujikwaa humo.”

Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba utufunike kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..


“Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo. “Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata mwandani wako asijue ufanyalo. Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.

Jehovah tunayakabidhi maisha yetu mikononi mwako..
Yahweh ukabariki Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba
Amani yako ikatawale,upendo wetu ukadumu,furaha na umoja ukawe
nasi,ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako
siku zote za maisha yetu.Tukawe na kiu/shauku ya kukutafuta Mungu
na kujifunza zaidi wema na fadhili zako,ukatupe macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako,tukanene yaliyo yako..
tukapate kutambua/kujitambua,tukasamehe na kusaidiana
tukaelimishane na kuelekezana kwa upendo na amani..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza. Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu. “Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine. “Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”

Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu na ukawaponye
wote wanaotaabika,wagonjwa,waliokatika vifungo mbalimbali
waliokata tamaa Mungu wakapate tumaini,ukawape neema ya kujiombea
Mungu wetu ukawainue walioanguka,ukapokee sala/maombi yao..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami
Sina neno zuri la kusema zaidi ya kuwaombea Baraka,
Amani na yote yaliyomema yasiwapite..
Mungu aendelee kuwatunza na pendo lenu Imani yenu ikadumu
  tumshukuru Mungu kwa kila jambo..
Nawapenda.

Mji wa Ai unatekwa

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usiwe na wasiwasi wowote; wachukue wanajeshi wako wote uelekee mji wa Ai, kwani mfalme wa Ai nimemtia mikononi mwako, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. 2Mtautendea mji wa Ai pamoja na mfalme wake kama vile mlivyoutendea mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake. Mali zake pamoja na mifugo yake mtakayoteka itakuwa ni mali yenu. Nendeni mwuvamie mji kutoka upande wa nyuma.”
3Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku. 4Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote. 5Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia. 6Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze. 7Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu. 8Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.” 9Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli.
10Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakusanya Waisraeli na kuelekea mjini Ai, akiwa pamoja na wazee. 11Wanajeshi wote waliofuatana naye walikaribia mji na kupiga kambi kaskazini yake, ngambo ya bonde mkabala wa mji wa Ai. 12Ndipo akachukua watu wengine 5,000 na kuwaweka wavizie kati ya mji wa Betheli na Ai, magharibi ya mji wa Ai. 13Kikosi kikubwa kiliwekwa kaskazini mwa mji na wale waliobaki waliwekwa magharibi ya mji. Lakini usiku huo, Yoshua akalala bondeni.
14Mfalme wa mji wa Ai alipoona hivyo, aliharakisha na kwenda kwenye mteremko wa kuelekea Araba ili akabiliane na Waisraeli vitani. Lakini hakujua kwamba mji wake ulikuwa umeviziwa kutoka nyuma. 15Kisha Yoshua pamoja na watu wake wakajifanya kana kwamba wanashindwa, wakaanza kukimbia kuelekea jangwani. 16Watu wote waliokuwa mjini waliitwa wawafuatie Waisraeli; na walipokuwa wanamfuatia Yoshua, walitoka na kwenda mbali na mji wao. 17Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai,8:17 Ai: Kigiriki. Kiebrania: Ai na Betheli. waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli.
18Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai. 19Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto. 20Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia. 21Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua. 22Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao. 23Lakini mfalme wa mji wa Ai walimteka akiwa hai na kumpeleka kwa Yoshua.
24Waisraeli walipomaliza kabisa kuwaua watu wote wa Ai huko nyikani ambako waliwafuatia wakarudi mjini Ai na kuwaua wote waliosalia humo. 25Jumla ya watu wa Ai waliouawa siku hiyo, wanaume kwa wanawake, walikuwa 12,000. 26Yoshua hakuushusha mkono wake aliokuwa ameushikilia mkuki wake kuelekea Ai mpaka alipowaua wakazi wote wa mji huo. 27Waisraeli waliteka tu wanyama na mali kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. 28Basi, Yoshua aliuteketeza mji wa Ai kwa moto na kuufanya magofu hadi hivi leo. 29Kisha akamtundika mfalme wa Ai mtini mpaka jioni. Lakini jua lilipoanza kutua, Yoshua aliamuru maiti yake iondolewe mtini na kutupwa kwenye lango la mji kisha warundike rundo kubwa la mawe juu ya maiti hiyo; rundo hilo liko huko mpaka leo.

Sheria inasomwa mlimani Ebali

30 Taz Kumb 27:2-8 Kisha, Yoshua akamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, madhabahu mlimani Ebali, 31Taz Kut 20:25 kama Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Waisraeli, kadiri ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose kwamba itakuwa madhabahu iliyojengwa kwa mawe ambayo hayakuchongwa, wala kuguswa na chombo chochote cha chuma. Juu ya madhabahu hiyo walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketezwa na sadaka za amani. 32Na huko, mbele ya umati wote wa Waisraeli, Yoshua aliandika nakala ya sheria ya Mose juu ya mawe. 33Taz Kumb 11:29; 27:11-14 Waisraeli wote pamoja na viongozi wao, wazee na waamuzi na wageni wote waliokuwa kati yao, wakasimama kila upande mkabala na sanduku la agano mbele ya makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Nusu yao wakasimama mbele ya mlima Gerizimu na nusu nyingine wakasimama mbele ya mlima Ebali, kama vile Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyoagiza hapo awali kuhusu kubarikiwa kwa Waisraeli. 34Kisha, Yoshua akawasomea sheria zote, pamoja na baraka na laana kama ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria. 35Hakuna neno lililoamriwa na Mose ambalo Yoshua hakulisoma mbele ya umati wa Waisraeli, wakiwemo miongoni mwao wanawake, watoto na wageni.


Yoshua 8;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 18 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 7...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa mema mengi 

aliyotutendea/anayoendelea kututendea..
Mungu wetu ,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye huruma..
wewe ndiye Ndimi Mwenyezi-Mungu  Mungu wa wote wenye mwili
hakuna jambo lolote lililogumu linaloweza kukushinda Mungu wetu..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbingu,Uhimidiwe Jehovah
Uabudiwe Yahweh,Hakuna kama wewe Mungu wetu,Matendo yako
ni ya ajabu mno,Matendo yako ni makuu sana,Unatosha Baba wa Mbinguni


Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake. Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu, makao matakatifu ya Mungu Mkuu. Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa; Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema. Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika; Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka. Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu; oneni maajabu aliyoyafanya duniani. Hukomesha vita popote duniani, huvunjavunja pinde na mikuki, nazo ngao huziteketeza. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Mungu wetu..


Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure. Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kupumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.
Tazama Jana imepita Jehovah Leo ni siku mpya Yahweh
na Kesho ni siku nyingine Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tukakuja mbele zako tukijinyenyekeza tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na 
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,masomo

na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende
sawasawa na mapenzi yako...
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe 
sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanotuzunguka..

Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya hekima,busara,kutambua/kujitambu katika yote,tukanene yaliyo yako tukachukuliane,tukapendane na pendo letu likawe la kweli nasi  kwa unafiki,tukaonyane na kuelemishana kwa upendo,tukasameheane,tukawe wanyeyekevu kwa watu wote,na Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo/tuendapo,tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Heri wote wamchao Mwenyezi-Mungu, wanaoishi kufuatana na amri zake. Utapata matunda ya jasho lako, utafurahi na kupata fanaka. Mkeo atakuwa kama mzabibu wa matunda mengi nyumbani mwako; watoto wako kama chipukizi za mzeituni kuzunguka meza yako. Naam, ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akubariki kutoka Siyoni! Uione fanaka ya Yerusalemu, siku zote za maisha yako. Uishi na hata uwaone wajukuu zako! Amani iwe na Israeli!

Mungu wetu ukawakuguse na mkono wako wenye nguvu wote 

wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,waliokatika vifungo
vya yule mwovu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Yahweh ukawaponye kimwili na kiroho pia,Baba ukawasimamishe
wale wote walioanguka,Mungu wetu ukawasamehe wale wote
waliokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea
Baba ukapokee sala/maombi ya watoto wako wote wakuombao
kwa imani na wafiwa ukawape nguvu,uvumilivu ,Baba ukawafariji..


Ee Mwenyezi-Mungu, sina moyo wa kiburi; mimi si mtu wa majivuno. Sijishughulishi na mambo makuu, au yaliyo ya ajabu mno kwangu. Ila nafsi yangu imetulia na kuwa na amani, kama mtoto mchanga alivyotulia na mama yake; ndivyo nafsi yangu ilivyo tulivu. Ee Israeli, umtumainie Mwenyezi-Mungu, tangu sasa na hata milele.
Asante Mungu wetu sifa na utukufu tunakurudishia wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!
Asanteni sana wapendwa kwa kuwa nami
UPendo Wenu Ukadumu Daima..
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea katika yote
Baraka,Amani na furaha viwe nanyi daima..
Nawapenda.



Kosa na adhabu ya Akani

1Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotolewa viangamizwe kwani Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alichukua baadhi ya vitu vilivyoamriwa viteketezwe. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli.
2Yoshua akawatuma watu kutoka Yeriko kwenda mji wa Ai, ulio karibu ya Beth-aveni, mashariki ya Betheli, akawaambia, “Nendeni mkaipeleleze nchi.” Nao wakaenda na kuupeleleza mji wa Ai. 3Waliporudi, wakamwambia Yoshua, “Hakuna haja kupeleka watu wote kuushambulia mji wa Ai, maana wakazi wake ni wachache tu. Watu elfu mbili au tatu watatosha.” 4Basi, watu kama elfu tatu hivi wakaenda kuushambulia mji wa Ai, lakini wakakimbizwa na wakazi wa mji huo. 5Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji.
6Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao. 7Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani! 8Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao? 9Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”
10Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo? 11Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao. 12Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe. 13Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu! 14Kwa hiyo kesho asubuhi wote mtakuja mbele yangu, kabila baada ya kabila. Kabila nitakalolichagua litakwenda mbele, ukoo baada ya ukoo. Ukoo nitakaouchagua utakwenda mbele, jamaa baada ya jamaa. Na jamaa nitakayoichagua itakwenda mbele, mtu mmojammoja. 15Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’”
16Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa. 17Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa. 18Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa. 19Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.” 20Akani akamjibu; “Ni kweli nimetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Na hivi ndivyo nilivyofanya: 21Nilipoona vazi moja zuri kutoka Shinari kati ya nyara, shekeli 200 za fedha na mchi wa dhahabu wenye uzito wa shekeli 50, nikavitamani na kuvichukua; nimevificha ardhini ndani ya hema langu; na fedha iko chini ya vitu hivyo.”
22Basi, Yoshua akawatuma wajumbe, nao wakakimbia hemani kwa Akani. Na kumbe, vilikuwa vimefichwa hemani na fedha ikiwa chini yake. 23Wakavichukua hemani na kuvipeleka kwa Yoshua na watu wote wa Israeli; nao wakaviweka chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu. 24Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakamchukua Akani, mwana wa Zera, pamoja na fedha, vazi, dhahabu, watoto wake wa kiume na binti zake, ng'ombe, punda na kondoo wake, hema lake na kila kitu alichokuwa nacho na kuwapeleka kwenye bonde la Akori. 25Yoshua akamwuliza Akani, “Kwa nini umetuletea taabu? Mwenyezi-Mungu atakuletea taabu wewe mwenyewe leo.” Waisraeli wote wakampiga Akani kwa mawe mpaka akafa. Kisha wakawapiga jamaa yake yote kwa mawe mpaka wakafa, wakawateketeza wote kwa moto. 26Halafu wakarundika mawe mengi juu yake, ambayo yako hadi leo. Hapo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikapoa; na mahali hapo pakaitwa Bonde la Akori7:26 Akori: Maana yake “taabu”. mpaka hivi leo.


Yoshua 7;1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Tuesday 17 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 6..




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi,Mfalme wa Amani,Muweza wa yote,Baba wa Rehema/neema,Jehovah..!Yahweh..!Adonai..!Elohim..!
El Elyon..!El Qanna,El Shaddai.!Emanuli-Mungu pamoja nasi...!!
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,
Uhimidiwe Yahweh,Unastahili kuabudiwa Jehovah..!
Unatosha Mungu wetu,Matendo yako ni makuu sana,
Matendo yako ni ya ajabu,Hakuna kama wewe Mungu wetu..!

Tazama Jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu..
Tunakuja mbele zako tukijinyeyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,
kwajua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea...
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga Kristo na vyote vinavyokwenda
kinyume nawe Mungu wetu vishindwe katika Jina lililokuu kupita majina yote Jina la Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu. Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende
sawasawa na mapenzi yako...
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako itawale katika
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,famila/ndugu na wote wanaotuzunguka,Baba upendo wetu ukadumu,huruma na kusaidiana,tuchukuliane na kuonyana kwa amani,hekima na busara vikatawale,
Utuwema na fadhili viwe nasi,ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu mwanga wako ukatawale katika nyumba zetu...
Tukawe barua njema Mungu wetu na tukasomeke
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Endeleeni kupendana kindugu. Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao. Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?” Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.
Baba ukawaguse kwa mkono wako wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu,wagonjwa,wenye njaa,wenye shida/tabu na wote wasumbukao na kuleemewa na mnizigo
Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia..
Baba wa Mbinguni ukawape neema  ya kuweza kujiombea na kufuata njia zako,Mungu wetu tunaomba ukapokee sala/maombi yetu...
wafiwa ukawe mfariji wao Baba wa Mbinguni..

Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.

Tunakushukuru Mungu wetu na kukuabudu daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana Wapendwa kwa kuwa nami,
Mungu wetu aendelee kuwabariki na msipungukiwe katika mahitaji yenu..
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapenzi yake
Amani  ya Kristo ikatawale katka maisha yenu..
Nawapenda.

Waisraeli wanauteka mji wa Yeriko

1Milango ya kuingilia mjini Yeriko ilikuwa imefungwa imara kwa ndani kuwazuia Waisraeli wasiingie. Hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka katika mji huo. 2Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Angalia! Mimi nitautia mikononi mwako mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na askari wake shujaa. 3Wewe na wale watu wenye silaha wote mtauzunguka huo mji mara moja kila siku kwa siku sita. 4Makuhani saba, kila mmoja akiwa amechukua baragumu yake ya pembe za kondoo dume, watatangulia mbele ya sanduku la agano. Katika siku ya saba mtauzunguka mji huo mara saba, huku makuhani wakipiga mabaragumu. 5Watakapopiga hayo mabaragumu kwa mlio mkubwa na mara tu mtakaposikia huo mlio, watu wote watapiga kelele kubwa, nazo kuta za mji zitaanguka chini. Ndipo watu watauvamia mji kila mmoja kutoka mahali aliposimama.”
6Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, “Libebeni sanduku la agano na makuhani saba wachukue mabaragumu saba za kondoo dume, watangulie mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu.” 7Yoshua akawaambia watu, “Nendeni mbele; uzungukeni mji, nao watu wenye silaha waende mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.”
8Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano. 9Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo. 10Lakini Yoshua akawaamuru watu, “Msipige kelele au kutoa sauti, wala neno lolote lisitoke vinywani mwenu, mpaka siku ile ambapo nitawaambieni mpige kelele; wakati huo ndipo mtakapopiga kelele.” 11Basi, Yoshua aliwafanya wale watu wauzunguke mji mara moja kila siku wakiwa wamebeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu na kurudi kambini kulala usiku.
12Asubuhi yake Yoshua akaamka alfajiri na mapema, na makuhani wakalibeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. 13Wale makuhani saba wenye mabaragumu saba za kondoo dume walitembea mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu wakipiga mabaragumu mfululizo. Watu wenye silaha walilitangulia sanduku la Mwenyezi-Mungu na walinzi wengine nyuma yake. Mabaragumu yakaendelea kupigwa. 14Siku ya pili yake waliuzunguka huo mji mara moja; na kurudi tena kambini kwao. Walifanya hivyo kwa muda wa siku sita. 15Siku ya saba, waliamka alfajiri na mapema, wakauzunguka mji huo mara saba kwa namna ileile. Ilikuwa ni siku hiyo tu ambayo waliuzunguka mji huo mara saba. 16Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji! 17Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu. 18Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa. 19Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.”
20Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka. 21Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda.
22Yoshua akawaambia wale wapelelezi wawili walioipeleleza nchi hiyo, “Nendeni katika nyumba ya yule kahaba; mkamlete yule mwanamke na wale wote ambao ni ndugu zake kama mlivyomwapia.” 23Basi, wale vijana wapelelezi wakaenda; wakamleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote wa jamaa yake, wakawaweka nje ya kambi ya Israeli. 24Kisha, wakauchoma moto mji wa Yeriko na kila kitu kilichokuwako isipokuwa fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma; hivyo viliwekwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 25Lakini yule kahaba Rahabu pamoja na watu wote wa nyumba ya baba yake, Yoshua aliyaokoa maisha yao. Rahabu akaishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe ambao Yoshua aliwatuma kwenda kuupeleleza mji wa Yeriko.
26Wakati huo Yoshua alitamka apizo rasmi mbele ya watu akisema,
“Atakayeujenga tena mji wa Yeriko,
na alaaniwe na Mungu,
Yeyote atakayeweka msingi wa mji huo,
mzaliwa wake wa kwanza na afe.
Yeyote atakayejenga lango la mji huo,
mwanawe kitinda mimba na afe.”
27Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yoshua na sifa zake zikaenea nchini kote.

Yoshua 6;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Monday 16 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 5..



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Mtakatifu..!Mtakatifu..!,Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu, Muumba wa Mbingu na Nchi..
Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa Abarahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote..
Mume wa wajane,Baba wa Yatima,Baba wa upendo..
Baba wa Baraka,Baba wa Huruma,Kimbilio letu..
Msaada wetu,Mwanga wetu,Nuru ya maisha yetu..
Hakuna kama wewe,Hakuna wa kufanana nawe..
Unatosha ee Mungu wetu,Matendo yako ni ajabu..
Matendo yako ni makuu Mno..!
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa Mungu wetu,Unasahili kuabudiwa Jehovah..
Sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu..!

Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.”
Asante kwa wema na fadhili zako Yahweh
Asante kwa ulinzi wako  wakati wote Mungu wetu
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Mungu wetu..
Asante kwa pumzi/uzima na tukiwa tayari kwa majukumu yetu..
Ni kwa neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako Jehovah sisi kuwa hivi tulivyo,si kwa nguvu/utashi wetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana zaidi ya wengine waliotangulia/kufa na wengine wakiwa taabani vitandani..
Tunakushukuru ee Mungu wetu..

Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako’. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nzareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”

Mwenyezi-Mungu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Baba
tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Yahweh ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Upendo wako ukawe nasi daima,Baraka zako zitufuate,
wema na fadhili zako ziwe nasi,furaha na shangwe ziwe nasi,Hekima,Busara ziwe nasi,huruma na kusaidia wengine,tukaonyane na kuelimisha kwa upendo, tukachukuliane na kusameheana..
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako,ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako..
Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wagonjwa, wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye shida/tabu,waliokatika vifungo vya yule mwovu na wote wataabikao na kuelemewa na mizigo
Mungu wetu tunaomba ukawabariki na kuwaponya kimwili na kiroho...
Baba ukaonekane na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,
kufuata njia zako,nuru yako ikaangaze katika maisha yao..

Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Baba wa mbinguni ukasikie kulia kwao na ukawafute machozi yao wote wanokuomba na kuamini
kwamba wewe ni Mungu wao na wewe ndiye mponyaji mkuu,Mungu wetu ukapokee sala/maombi yao,Baba ukawaweke huru na ukawafunike kwa
Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
Wafiwa ukawe mfariji wao..
Jehovah tunayaweka haya yote mikononi mwako
 tukishukuru na tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi jana,leo na hata Milele..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwaongoza katika yote
Msipungukiwe katika mahitaji yenu,Baba wa Mbinguni
akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda. 

1Wafalme wote wa Waamori walioishi ngambo ya magharibi ya Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa pwani ya bahari ya Mediteranea, waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili ya Waisraeli mpaka walipokwisha vuka, wakafa moyo; wakaishiwa nguvu kabisa kwa kuwaogopa Waisraeli.

Kutahiriwa kwa Waisraeli huko Gilgali

2Wakati huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya jiwe gumu ili uwatahiri Waisraeli.” 3Basi, Yoshua akatengeneza visu hivyo vya jiwe gumu na kuwatahiri Waisraeli huko Gibea-haaralothi.5:3 Gibea-haaralothi: Maana yake mlima wa magovi. 4Sababu ya kuwatahiri Waisraeli ni hii: Waisraeli wote, wanaume, waliotoka Misri ambao walikuwa na umri wa kwenda vitani, wote walifariki safarini jangwani baada ya kutoka nchini Misri. 5Hao wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini wale wote waliozaliwa safarini huko jangwani baada ya kutoka Misri, walikuwa bado hawajatahiriwa. 6Taz Hes 14:28-35 Waisraeli walisafiri kwa muda wa miaka arubaini nyikani hata wanaume wote waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakaangamia kwa kuwa hawakusikiliza aliyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alikuwa amewaapia watu hao kwamba hawataiona nchi ile inayotiririka maziwa na asali ambayo yeye aliwaapia baba zao kuwa atawapa. 7Kwa hiyo ilikuwa ni watoto wa watu hao ambao Mwenyezi-Mungu aliwakuza badala yao, hao ndio Yoshua aliwatahiri, kwani hawakuwa wametahiriwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani.
8Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona. 9Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali5:9 Gilgali: Linasikika kama neno lenye maana “kuondolewa”. mpaka hivi leo.
10Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko. 11Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile. 12Taz Kut 16:35 Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani.

Yoshua na kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu

13Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?” 14Naye akamjibu; “Wala wenu wala wa adui zenu! Ila mimi ni kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu, na sasa nimewasili.” Yoshua akainama chini akasujudu, kisha akamwuliza, “Bwana wangu, mimi mtumishi wako, unataka nifanye nini?” 15Huyo kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Yoshua akafanya hivyo.



Yoshua 5;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.