Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 28 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 27 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana,Tumshukuru katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unatosha Baba wa Mbinguni..
Hakuna kama wewe Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.
Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote
vinavyoonekana na visivyoonekana..
Matendo yako ni ya Ajabu..!



Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?” Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.” Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako.
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mfalme wa Amani tunaomba utuepushe katika majaribu
Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’ “Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.



Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Baba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahwe tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
 ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na ukavifunike kwa Damu ya
 Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Mfalme wa Amani tunakabidhi maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka,Mungu wetu Amani yako ikawe nasi..
Upendo wetu ukadumu,furaha na baraka zisitupite..
Utu wema na fadhili,Ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu..
Ukatupe ulinzi wako sisi na vyote tunavyovimiliki..
Ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia
 magumu/majaribu mbalimbali,ukawaokoe na kuwaponya wote walio katika vifungo vya yule mwovu..
Ukawarudishe kundini wote waliopotea,Baba ukasikie kuomba kwetu,Baba ukawape neema ya kuweza kujiombea na kufuata njia zako ili wawe huru..
Utupe neema ya kusimamia Neno lako  Amri na Sheria zako 
siku zote za maisha yetu,Ee Baba utuhurumie..!



Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Asante Mungu wetu yote tunayaweka mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu hakuna mwingine kama wewe..
Sifa na Utukufu tunakurudisha Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami na kunisoma
Mfalme wa Amani na baraka aendelee kutawala katika maisha yenu
Mkono wa Mungu ukawaguse na kuwatendea katika maisha yenu..
Nawapenda.


Sheria za Mungu zilizoandikwa kwenye mawe

1Basi, Mose akiwa pamoja na wazee wa Israeli aliwaambia watu hivi: “Shikeni amri zote ninazowapa leo. 2Siku ile mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni, mtasimika mawe makubwa na kuyapiga lipu. 3Juu yake mtaandika maneno yote ya sheria zote hizi, mtakapoingia katika nchi inayotiririka maziwa na asali ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu, aliwaahidi. 4Mkiwa ngambo ya mto Yordani, mtasimika mawe hata juu ya mlima Ebali, kama ninavyowaamuru hivi leo, na kuyapiga lipu. 5Mtamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, madhabahu mahali hapo palipo na mawe ambayo hayakuchongwa. 6Naam, madhabahu yoyote mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lazima ijengwe kwa mawe yasiyochongwa. Juu ya madhabahu hiyo mtamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu sadaka za kuteketezwa. 7Mtamtolea sadaka za amani, na kula papo hapo na kufurahi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 8Mtaandika waziwazi juu ya mawe hayo maneno yote ya sheria hii.”
9Basi, Mose pamoja na makuhani Walawi wakawaambia watu wote wa Israeli, “Nyamazeni mnisikilize enyi watu wa Israeli. Leo hii nyinyi mmekuwa watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 10Kwa hiyo mtatii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mkizifuata amri zake na masharti yake ambayo ninawaamuru leo.”

Laana ya kutotii

11Siku hiyo Mose aliwaagiza watu na kusema, 12“Mkisha vuka Yordani, makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Gerizimu kuwabariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini. 13Na makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Ebali wakati laana zitakapotolewa: Reubeni, Gadi, Asheri, Zebuluni, Dani na Naftali. 14Nao Walawi watawatangazia watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15“ ‘Alaaniwe mtu yeyote afanyaye sanamu ya kuchonga au ya kusubu na kuisimamisha kwa siri, kitu ambacho kimetengenezwa na mikono ya fundi na ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
16“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayemdharau baba yake au mama yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
17“ ‘Alaaniwe mtu yeyote aondoaye alama ya mpaka wa jirani yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
18“ ‘Alaaniwe mtu yeyote ampotoshaye kipofu njiani.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
19“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayepotosha haki ya mgeni au yatima au mjane’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
20“ ‘Alaaniwe mwanamume alalaye na mke wa baba yake, maana amemwaibisha baba yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
21“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mnyama yoyote’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
22“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na dada yake awe ni binti ya baba yake au binti ya mama yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
23“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mama mkwe wake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
24“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayeua mtu kwa siri’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
25“ ‘Alaaniwe mtu yeyote apokeaye hongo ili aue mtu asiye na hatia’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
26“ ‘Alaaniwe mtu yeyote asiyekubali maneno haya ya sheria na kuyatii’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’


Kumbukumbu la Sheria 27:1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 27 September 2017

Kifo cha Mtanzania Hispania - Mwanasarakasi



KIFO CHA MWANASARAKASI MOHAMMED IDI MOHAMMED (“MOHDY”)
Na Freddy Macha




Sarakasi ni kati ya sanaa hatari na za kusisimua sana.
Kwa sasa Ulaya wapo vijana na watu wa makamo mbalimbali waliohamia toka Afrika Mashariki (hasa Kenya na Tanzania) wakitumbuiza kadamnasi kwa sarakasi, Uingereza, Ureno, Ujerumani na Hispania.
Nchini Hispania kuna visiwa vya Grand Canary ambapo Watanzania wachache huruka ruka kuvutia maelfu ya watalii.
Moja yake ni Lanzarote. Hapa Mtanzania Mohammed Idi Mohamed aliyehamia baada ya kuishi Ujerumani kwa kipindi. Mohdy, Muddy au Modi (wanavyomjua wengi) aliwahi pia kufanya kazi Tanzania, Ureno na Uingereza.
Alifariki Jumatatu 18 Septemba, 2017, asubuhi. Sababu za kifo chake zimeelezwa na waganga ni kuvuja damu kutoka mfereji wa koo kwenda mapafu na kutokea tumboni. Alipasukwa mshipa huu wa damu ghafla na kuanguka bafuni akipiga mswaki. Bahati nzuri Muddy alijikatia bima ya maisha ambayo imeondoa tatizo la kusafirisha mwili wake nyumbani kuzikwa. Michango iiliyoombwa kutolewa itasaidia familia yake na gharama nyingine za mazishi. Tuma kupitia Western Union. Huwa bei nafuu zikitumwa zifike kesho yake badala ya siku hiyo hiyo... Marehemu ameacha watoto wawili na wajukuu. Mungu aiweke roho yake pema peponi.

Kwa walio Ujerumani, ni Malimbo Saidi Malimbo, simu (+49 ) 1522-4082848.

Uingereza, Saidi Kanda (+44) 4040-66607. Tanzania, Eddy Sengo, (+255) 656 210 725.

Picha ihsani ya Fab Moses, Lanzarote, Hispania


-London, 26 Septemba 2017

-Bpepe: gmacha52@gmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 26 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii na kua tayari kuendelea na majukumu yetu..
Si kwamba sisi ni wema sana,Si kwa nguvu zetu wala ujuzi wetu
sisi kuwa hivi tulivyo hapana ni kwa neema/rehema zako Mungu..

Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh,Usifiwe Jehovah..
Unastahili kuabudiwa Mfalme wa Amani,Unatosha Mungu wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane
Hakuna kama wewe Mungu wetu,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho
Matendo yako ni ya Ajabu,wewe ndiye Ndimi Mwenyezi-Mungu..
Baba wa upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
wewe ukisema ndiyo nani aseme siyo?



Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.



Mfalme wa Amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishushana kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
 wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na
 yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu 
na utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo 
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.

Baba wa Mbinguni tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuwabariki wenyekuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu 
Baba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,Familia/ndugu 
na wote wanaotuzunguka Mfalme wa Amani tunaomba amani yako
ikatawale,ulinzi wako ukawe nasi,Upendo ukatawale,furaha, 
hekima na busara vikatawale katika maisha yetu..
Yahweh ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amari na Sheria zako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.



Tazama wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu
waliokatika vifungo vya yule mwovu,wagonjwa ..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..
Ukawaponye kimwili na kiroho pia..
Baba ukawape neema ya kuweza kujiombea na kukujua wewe
wakafuate yaliyo yako na kuamini kuwa wewe ndiye mponyaji..
ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe..
ukapokee sala/maombi yao ukasikie kulia kwao,ukawafute machozi yao,ukawainue na kuwaongoza,ukawatakase na kuwafunika kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo..
 wafiwa ukawe mfariji wao na ukawape nguvu,imani katika kipindi kigumu kwao..


Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu nani muweza wa yote..
Hakuna lililogumu kwako..
Sifa na utukufu ni wako Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo asanteni sana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na mkadumu katika pendo lake..
Amani ya Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda.


Matoleo ya mavuno

1“Baada ya kufika na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapa iwe yenu na kuishi huko, 2baadhi ya malimbuko ya mazao utakayovuna katika nchi anayokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, utayachukua katika kikapu mpaka pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amepachagua pawe makao yake. 3Utamwendea kuhani anayehudumu wakati huo, na kumwambia, ‘Leo ninakiri mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuwa nimeingia katika nchi aliyowaapia wazee wetu kuwa atatupa.’
4“Naye kuhani atakapochukua kikapu hicho mikononi mwako na kukiweka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, 5utatamka maneno haya mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako: ‘Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyetangatanga huko na huko, kisha akashuka kwenda Misri akaishi huko kama mgeni. Yeye na jamaa yake walikuwa watu wachache tu walipokuwa huko, lakini wakawa taifa kubwa lenye nguvu na watu wengi. 6Wamisri walitutendea kwa ukatili wakatutesa na kutulazimisha kufanya kazi ngumu ya watumwa. 7Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata. 8Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu. 9Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali. 10Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’
“Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake. 11Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe. 12Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu. 13Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau. 14Sikula zaka yoyote nilipokuwa ninaomboleza; sikuitoa nje ya nyumba yangu nilipokuwa najisi na sikutoa zaka hiyo kwa wafu. Nimekutii ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoamuru. 15Uangalie chini kutoka makao yako matakatifu mbinguni, uwabariki watu wako Israeli na nchi uliyotupatia kama ulivyowaapia wazee wetu; nchi inayotiririka maziwa na asali.’

Watu wa Mwenyezi-Mungu

16“Leo hii, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaamuru kuyashika masharti na maagizo haya. Muwe waangalifu kuyatekeleza kwa moyo wote na roho yote. 17Leo hii mmekiri Mwenyezi-Mungu, kuwa Mungu wenu, na kwamba mtafuata njia zake na kushika masharti, amri zake na maagizo yake na kutii sauti yake. 18Naye Mwenyezi-Mungu ametamka rasmi leo hii kwamba nyinyi ni watu wake yeye mwenyewe kama alivyowaahidi na kwamba mnatakiwa kushika amri zake zote. 19Atawafanyieni nyinyi kuwa taifa kubwa kuliko mataifa yote aliyoyaumba. Nanyi mtalitetea jina lake, sifa yake na heshima yake. Nyinyi mtakuwa watu wake, walio mali yake, kama alivyoahidi.”



Kumbukumbu la Sheria 26:1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 26 September 2017

Wanawake Wabunifu Kenya

Kwa simu Toka London yawaletea vipindi viwili vya wanawake wanaojituma



1. Mwanamke anayeongoza Timu ya Mpira







2. Mafuta Mapya ya Ngozi na Haiba- Yaliyobuniwa na Mwanamke





zaidi ingia;Kwa Simu Toka London- Na Freddy Macha


"Swahili Na Waswahili"Pamoja Diama.

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 25 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote..
Utukuzwe Jehovah,Uabudiwe Yahweh,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..


Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.



Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na tukijiachilia mikononi mwako..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
 kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Jehovah tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi
tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.
Mfalme wa Amani tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi,famili/ndugu na wote wanaotuzunguka
Ukatamalaki na kutuatamia,tunaomba ulinzi wako, Amani na Upendo
Hekima na Busara vikatawale katka familia zetu..
Tuhurumiane na kusaidiana,tuelekezane kwa upendo na tuchukuliane..
Tukanene yaliyoyako Mungu wetu,Ukatupe kutambua/kujitambua
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako siku zote.
Ukatufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yetu Kristo...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi

Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea, hata umati wa watu ukashangaa. Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia. Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.


Yahweh ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,
wagonjwa,waliokata tamaa,waliokataliwa wanao taabika..
wanaopitia magumu/majaribu,walio katika vifungo vya yule mwovu
Baba wa mbinguni ukawape uponyaji wa mwili na roho pia
wakapate tumaini lako na ukawasimamishe tena..
Ukawape neema ya kuweza kujiombea na kusimamia Neno lako
Ukawafungue na kuwaongoza katika yote,Ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukaonekane katika mapito yao

“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’ Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.” Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”

Baba wa Faraja ukawafariji Wafiwa,ukawape amani na uvumilivu..
Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tuliyoyanena na tusiyoyanena Baba yote unajua na kutujua sisi
zaidi ya tujijuavyo..
Tumaini la kweli lipo kwako,Amani ina wewe..
Upendo wa kweli una wewe Mungu wetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo,Mungu aendelee kuwabariki
Mungu akawe nanyi na kuwalinda,msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.



 

1“Ikiwa kuna ugomvi kati ya watu wawili, wakaenda kuamuliwa mahakamani, mmoja akaonekana hana hatia, na mwingine akahukumiwa, 2kama yule aliyehukumiwa amepewa adhabu ya kuchapwa viboko, hakimu atamwamuru huyo alale chini na kuchapwa viboko kulingana na kosa lake. 3Mwenye hatia anaweza kuchapwa viboko arubaini lakini si zaidi. Mkizidisha kiasi hicho mtakuwa mmemfedhehesha ndugu yenu.
4“Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka.

Jukumu la kaka kwa ndugu yake marehemu

5“Kama ndugu wawili wa kiume wanaishi mahali fulani na mmoja wao akafariki bila kuacha mtoto wa kiume, mkewe marehemu asiolewe na mtu mwingine nje ya jamaa hiyo. Ni wajibu wa ndugu wa marehemu kumwoa mjane huyo. 6Mtoto wa kwanza wa kiume atakayezaliwa nao atahesabiwa kuwa mtoto wa marehemu, ili jina lake lisifutwe nchini Israeli. 7Lakini kama huyo ndugu wa marehemu hamtaki huyo mwanamke mjane, basi, mwanamke huyo atakwenda mbele ya wazee wa mji na kusema, ‘Kaka wa mume wangu marehemu anakataa kuendeleza jina la kaka yake marehemu katika Israeli; hapendi kunitimizia jukumu lake la kaka wa mume wangu marehemu.’ 8Kisha wazee wa mji watamwita huyo mwanamume kuongea naye. Kama bado atasisitiza kwamba hataki kumwoa, 9huyo mwanamke mjane atamwendea mbele ya hao wazee wa mji, atamvua kiatu chake kimoja na kumtemea mate usoni na kumwambia, ‘Hivi ndivyo anavyopaswa kutendewa mtu anayekataa kuidumisha nyumba ya kaka yake.’ 10Na jina la nyumba yake katika Israeli litakuwa: ‘Nyumba ya mtu aliyevuliwa kiatu.’”

Sheria nyingine

11“Wanaume wawili wakipigana na mke wa mmoja wao akamsaidia mumewe kwa kumkamata sehemu za siri yule anayepigana na mumewe, 12mtaukata mkono wa kulia wa huyo mwanamke; msimhurumie.
13“Msiwe na vipimo vya kupimia vya namna mbili: Kimoja kizito na kingine chepesi. Msitumie mizani za udanganyifu. 14Wala msiwe na aina mbili za vipimo vya kupimia, kubwa na ndogo.
15“Tumieni mizani na vipimo vyenye uzito sahihi ili mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 16Wote wanaofanya mambo hayo, wote wanaotenda kwa udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Amri ya kuwaua Waamaleki

17“Kumbukeni kitendo cha Waamaleki mlipokuwa safarini kutoka Misri. 18Kumbukeni walivyowashambulieni huko njiani mkiwa wanyonge na kuwapiga wale wote waliokuja nyuma yenu wamechoka. Waamaleki hawakumwogopa Mungu. 19Kwa hiyo wakati Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapowapumzisha kutokana na mashambulio ya adui zenu wote wanaowazunguka katika nchi ambayo amewapa mwimiliki na kuishi humo, ni lazima muwaangamize Waamaleki wote.


Kumbukumbu la Sheria 25:1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 25 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 24 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Munguametuchagua na ametupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii...
Tumshkuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Tumshukuru Mungu kwa Ulinzi wake wakati wote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa neema/rehema hii..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe Mungu wetu..
Uhimidiwe Yahweh,Uabudiwe milele..

Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Hakuna kama wewe,Matendo yako ni ya ajabu..
Unatosha Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
wewe ndiye Ndimi Mwenyezi-Mungu..!




Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Imba kwa shangwe ewe uliye tasa, wewe ambaye hujapata kuzaa! Paza sauti na kuimba kwa nguvu, wewe usiyepata kujifungua mtoto. Maana watoto wako wewe uliyeachwa watakuwa wengi kuliko wa aliye na mume. Panua nafasi hemani mwako, tandaza mapazia hapo unapoishi, usijali gharama zake. Zirefushe kamba zake, na kuimarisha vigingi vyake; maana utapanuka kila upande; wazawa wako watamiliki mataifa, miji iliyokuwa mahame itajaa watu. Usiogope maana hutaaibishwa tena; usifadhaike maana hutadharauliwa tena. Utaisahau aibu ya ujana wako, wala hutaikumbuka tena fedheha ya ujane wako. Muumba wako atakuwa mume wako; Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; yeye aitwa ‘Mungu wa ulimwengu wote’. “Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu amekuita tena wewe kama vile mke aliyeachwa na kuhuzunika, mke aliyeolewa akiwa kijana akaachwa. Mungu wako anasema: Nilikuacha kwa muda mfupi tu; kwa huruma nyingi, nitakurudisha. Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuonea huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu Mkombozi wako, nimesema. “Nitafanya kama nilivyofanya wakati wa Noa: Wakati ule niliapa kwamba sitaifunika tena ardhi kwa gharika. Basi sasa naapa kwamba sitakukasirikia tena wala sitakukemea tena. Milima yaweza kutoweka, vilima vyaweza kuondolewa, lakini fadhili zangu hazitakuondoka, agano langu la amani halitaondolewa. Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.



Mfalme wa Amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza
Tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
 wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga kristo
zishindwe katika jina lipitalo majina yote jina la
Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi: “Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua; mimi naitegemeza nguvu yako ili uyashinde mataifa mbele yako, na kuzivunja nguvu za wafalme. Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako, na hakuna lango litakalofungwa. Mimi nitakutangulia, na kuisawazisha milima mbele yako. Nitaivunjavunja milango ya shaba, na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma. Nitakupa hazina zilizofichwa gizani, na mali iliyo mahali pa siri, upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako. Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo, naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine ila mimi. Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui, ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi, wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi; mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine. Mimi hufanya mwanga na kuumba giza; huleta fanaka na kusababisha balaa. Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote. Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu, mawingu na yadondoshe uadilifu; dunia na ifunuke, ichipushe wokovu, na kuchanusha uadilifu pia! Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.”

Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa
Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Jehovah tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji

Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale,Ukatamalaki na ukatuatamie..
Amani na upendo vikatawale katika Nyumba/Ndoa zetu..
watoto wetu,wazazi,ndugu/familia na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu ukawe mlinzi mkuu,mkono wako wenye nguvu ukatuguse
na ukalete uponyaji kwa wote wanaotaabika,wenye shida/tabu,
Wagonjwa ,Wafiwa ukawe mfariji wao..
Wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Na wanaliokatika vifungo vya yule mwovu..
Baba ukawafungue na ukawaponye kimwili na kiroho pia..
Ukawape neema ya kukujua wewe na kufuata njia zako..
wakaweze kujiombea na ukapokee maombi/sala zao..
Ukasikie kulia kwao Baba ukawafute machozi yao..
 Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..


Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake, mtu aliye chombo cha udongo kushindana na mfinyanzi wake! Je, udongo humwuliza anayeufinyanga: “Unatengeneza nini hapa?” Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!” Ole wake mtoto amwambiaye baba yake, “Kwa nini umenizaa?” Au amwambiaye mama yake, “Ya nini umenileta duniani?” Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli, Mungu, Muumba wa Israeli asema: “Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu, au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe? Ni mimi niliyeifanya dunia, na kuumba binadamu aishiye humo. Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu, na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu. Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua, atekeleze matakwa yangu. Nitazifanikisha njia zake zote; ataujenga upya mji wangu Yerusalemu, na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni, bila kutaka malipo wala zawadi.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi, pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu, zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli, zote zitakuwa mali yako. Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo; watakusujudia na kukiri wakisema: ‘Kwako kuna Mungu wa kweli, wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’” Kweli wewe ni Mungu uliyefichika, Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi. Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika, wote kwa pamoja watavurugika. Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu, litapata wokovu wa milele. Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele. Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee, ndiye aliyeiumba dunia, ndiye aliyeiumba na kuitegemeza. Hakuiumba iwe ghasia na tupu, ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Yeye asema sasa: “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi sikunena kwa siri, wala katika nchi yenye giza. Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobo wanitafute katika ghasia. Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli, maneno yangu ni ya kuaminika.” Enyi watu wa mataifa mliosalia, kusanyikeni pamoja mje! Nyinyi mmekosa akili: Nyinyi mwabeba sanamu za miti na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu. Semeni wazi na kutoa hoja zenu; shaurianeni pamoja! Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa? Ni nani aliyetamka mambo haya zamani? Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu? Hakuna Mungu mwingine ila mimi! Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi; hakuna mwingine ila mimi. Nigeukieni mimi mpate kuokolewa, popote mlipo duniani. Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi nimeapa kwa nafsi yangu, ninachotamka ni ukweli, neno langu halitarudi nyuma: Kila binadamu atanipigia magoti, kila mtu ataapa uaminifu. “Watasema juu yangu, ‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’” Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu watamjia yeye na kuaibishwa. Lakini wazawa wa Israeli watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi.


Roho Mtakatifu akatuongoze na tukawe na kiasi..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Baba wa upendo na Baraka aendelee kuwamiminia Baraka,
Amani ikawe nanyi na Pendo lenu likadumu..
Mungu akaonekane katika maisha yenu..
Nawapenda.

Talaka na kuoa tena

1“Ikiwa mwanamume ameoa mke na baadaye akawa hapendezwi naye kwa sababu ameona kwake kitu kisichofaa, basi, huyo mwanamume akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, kisha huyo mwanamke akaondoka, 2akaolewa na mwanamume mwingine, 3kama huyo mume wa pili akimchukua, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, au kama huyo mumewe akifa, 4basi, yule mume wa kwanza haruhusiwi tena kumchukua huyo mwanamke kuwa mke wake kwa sababu alikwisha kutiwa unajisi. Kufanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.
5“Mwanamume aliyeoa karibuni asiende vitani wala asipewe kazi yoyote nyingine; aachwe huru kwa muda wa mwaka mmoja, ili akae nyumbani na kufurahi na mkewe.
6“Mtu yeyote asichukue jiwe la chini au la juu la kusagia kuwa rehani; kufanya hivyo ni kama kuchukua uhai wa mtu huyo.
7“Mtu yeyote akimwiba Mwisraeli mwenzake na kumfanya mtumwa wake au kumwuza utumwani, mtu huyo lazima auawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
8“Kama mtu akishikwa na ukoma mnapaswa kuwa waangalifu kufuata maagizo ya Walawi. Kama nilivyowaamuru ndivyo mtakavyofuata kwa uangalifu. 9Kumbukeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu alivyomtendea Miriamu mlipokuwa safarini kutoka Misri.
10“Ukimkopesha jirani kitu chochote, usiingie kwake kuchukua rehani. 11Msubiri nje na umwache yeye mwenyewe akuletee hiyo rehani. 12Kama yeye ni maskini usikae na rehani hiyo usiku kucha. 13Mrudishie kila siku jioni ili usiku aweze kujifunika na kukutakia baraka. Kufanya hivyo ni jambo la uadilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
14“Usimdhulumu kibarua maskini na mhitaji, awe Mwisraeli au mmoja wa wageni wanaoishi katika miji yenu. 15Kila siku, kabla jua halijakuchwa, mlipe ujira wake wa siku hiyo, maana yeye ni maskini na huo ujira ni tegemeo la moyo wake; ili asije akamlilia Mwenyezi-Mungu, nawe ukawa na hatia.
16“Wazazi wasiuawe kwa makosa ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya makosa ya wazazi wao. Kila mtu atauawa kwa makosa yake mwenyewe.
17“Msipotoshe haki za wageni na yatima. Wala msichukue vazi la mjane kuwa rehani. 18Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Kwa hiyo ninawapeni amri hiyo.
19“Mnapovuna mavuno yenu shambani na kusahau masuke mengine humo, msirudi kuyachukua, ila waachieni wageni, yatima na wajane, ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu awabariki katika kazi zenu zote. 20Mkipukutisha mizeituni yenu kuvuna matunda, msirudi kupukutisha tena vitawi vyake, ila waachieni wageni, yatima na wajane. 21Mnapochuma zabibu, msirudi kuokota zabibu zilizobaki ila waachieni wageni, yatima na wajane. 22Mtakumbuka kuwa nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri; kwa hiyo ninawapeni amri hii.



Kumbukumbu la Sheria 24:1-22


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.