Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 28 February 2017

Mwanamke Na Imani;Mjue Da'Nambua Jessica...!!


Wapendwa/Waungwana..[Mwanamke na Imani]Mwanamke wetu Leo ni "Dada Nambua Jessica..."
Dada huyu anamengi mengi ya kumuelezea..katika Imani yake,Kama mama,Mke na Rafiki..
Nisikunyime kumjua zaidi kwa mimi kukuelezea..ni vyema ukamsikilize wewe mwenyewe na hisi lazima utaondoka na lolote..
Unaweza kumsikiliza /Kumsoma na kumjua zaidi kupitia;Youtube; 






Asante sana Mpendwa da'Nambua Jessica kwa yote..Mungu azidi kukubariki na kukuongoza katika Safari yako..Akakutumie sawasawa na mapenzi yake..
Amina.

"Swahili Na Waswahili"Pamoja Sana.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo29....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu baba muumba wetu na muumba mbingu na nchi ..Tunashukuru kwa kutupa kibali cha kuiona tena siku hii..Ukaitawale siku hii na kutuongoza katika maisha yetu..Ukawe nasi Baba na kutubariki  Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Kazi,Biashara na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase na damu ya mwana kondoo wako.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tunaomba utusamehe dhambi zetu tulizokutenda kwa kuwaza,Kunena, kwa kutojua..Ukatupe Neema na roho mtakatifu akatuongoze katika yote..
Baba wa Mbinguni ukawaguse na kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu,Vifungo vyovyote vya mwovu...
Mfalme wa Amani ukatawale Nchi hii tunayoishi,Tanzani,Afrika na Dunia yote ..Ukawaongoze wanaotuongoza wakatuongoze kwenye Haki na kweli.
Sifa na utukufu ni kwako Baba wa Mbinguni...



Kinywa changu kimejaa sifa zako, na utukufu wako mchana kutwa.[Zaburi71:8].
Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu.[Wafilipi1:11].
wakisema, “Amina! Sifautukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!”[Ufunuo7:12].
                                   Muwe na Wakati Mwema.


Yakobo anawasili kwa Labani

1Yakobo aliendelea na safari yake, akafika katika nchi za watu wa mashariki. 2Siku moja akaona kisima mbugani, na kando yake makundi matatu ya kondoo wamepumzika. Kondoo walikuwa wananyweshwa kutoka kisima hicho kilichokuwa kimefunikwa kwa jiwe kubwa. 3Kwa kawaida, makundi yote ya kondoo yalipokusanyika, wachungaji walivingirisha hilo jiwe kwa pamoja toka kisimani na kuwanywesha kondoo. Halafu walikifunika tena kisima kwa jiwe hilo.
4Yakobo akawauliza wachungaji, “Ndugu zangu, mmetoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka Harani.” 5Naye akawauliza, “Je, mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakamjibu, “Tunamfahamu.” 6Akaendelea kuwauliza, “Je, hajambo?” Nao wakamjibu, “Hajambo; hata binti yake Raheli, yule kule anakuja na kondoo wake!” 7Hapo Yakobo akawaambia, “Naona bado ni mchana, na si wakati wa kuwakusanya kondoo pamoja. Basi, wanywesheni kondoo maji, mwende mkawachunge.” 8Lakini wao wakamwambia, “Hatuwezi kufanya hivyo mpaka makundi yote yawe yamekusanyika pamoja, na jiwe limevingirishwa kisimani, ndipo tuwanyweshe kondoo.”
9Yakobo alipokuwa bado anazungumza na hao wachungaji, Raheli akafika na kondoo wa baba yake, kwani ndiye aliyekuwa akiwachunga. 10Yakobo alipomwona Raheli, bintiye Labani, kaka ya mama yake, na alipowaona kondoo wa Labani, mjomba wake, akaenda na kulivingirisha lile jiwe kwenye mdomo wa kisima, akalinywesha maji kundi la Labani, mjomba wake. 11Kisha Yakobo akambusu Raheli na kulia kwa sauti. 12Halafu Yakobo akamjulisha Raheli kuwa yeye ni wa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Raheli akapiga mbio nyumbani akamwarifu baba yake.
13Labani aliposikia habari za Yakobo, mpwa wake, alikwenda mbio kumlaki, akamkumbatia, akambusu, akamkaribisha nyumbani kwake. Yakobo akamsimulia Labani mambo yote yaliyotokea. 14Naye Labani akasema, “Hakika, wewe ni jamaa yangu, damu moja nami!” Yakobo akakaa naye kwa muda wa mwezi mmoja.

Yakobo anaoa binti za Labani
15Siku moja Labani alimwambia Yakobo, “Wewe ni jamaa yangu lakini hiyo haimaanishi kwamba utanitumikia bure. Niambie unataka ujira kiasi gani!” 16Sasa, Labani alikuwa na binti wawili: Mkubwa aliitwa Lea, na mdogo aliitwa Raheli. 17Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na wa kupendeza. 18Yakobo alimpenda Raheli; kwa hiyo akamwambia Labani, “Nitakutumikia miaka saba ili unioze Raheli, binti yako mdogo.” 19Labani akamwambia, “Afadhali nimwoze Raheli kwako wewe kuliko kumwoza mtu mwingine yeyote. Endelea kuishi nami.” 20Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli.
21Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.” 22Basi, Labani akaandaa karamu na kuwaalika watu wote wa huko. 23Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye. 24(Labani akamtoa Zilpa, mjakazi wake, awe mtumishi wa Lea.) 25Asubuhi, Yakobo akagundua ya kuwa ni Lea! Basi, akamwuliza Labani, “Umenitendea jambo gani? Je, si nilikutumikia kwa ajili ya Raheli? Mbona basi, umenidanganya?” 26Labani akamjibu, “Nchini mwetu hatufanyi hivyo; si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya mkubwa. 27Mtimizie Lea siku zake saba, nasi tutakupa Raheli kwa utumishi wa miaka saba mingine.” 28Yakobo akakubali. Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake. 29(Labani akamtoa Bilha, mjakazi wake, awe mtumishi wa Raheli). 30Basi, Yakobo akalala na Raheli pia. Lakini Yakobo akampenda Raheli kuliko Lea; akamtumikia Labani miaka mingine saba.

Watoto wa Yakobo
31Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Lea anachukiwa, akamjalia watoto; lakini Raheli alikuwa tasa. 32Lea akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Reubeni, akisema, “Mwenyezi-Mungu ameyaona mateso yangu; bila shaka sasa mume wangu atanipenda.” 33Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Simeoni, akisema, “Mwenyezi-Mungu amenipa mtoto mwingine wa kiume kwa sababu amesikia jinsi ninavyochukiwa.” 34Akapata mimba mara nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Lawi, akisema, “Wakati huu mume wangu atajiunga nami, kwani nimemzalia watoto watatu wa kiume.” 35Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Yuda, akisema, “Safari hii nitamsifu Mwenyezi-Mungu.” Kisha Lea akaacha kuzaa.
Mwanzo29;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 27 February 2017

kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo28...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeanza vyema wiki/siku hii Mungu 
aliyotupa kibali cha kuiona tena...Tunamshukuru Mungu kwa kutuchagua na kutupa nafasi hii..Ikawe yenye Baraka,Amani,Upendo,Furaha,Imani na kumtukuza yeye aliye tuumba na kuumba Mbingu na Nchi..
Akabariki kuingia/kutoka kwetu,Vilaji/vinywaji,Kazi,Biashara,Masomo na Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia akavitakase..
Akawaguse na Kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo vya mwovu,waliokata Tamaa,Waliyokataliwa,Wagonjwa,waliomagerezani pasipo na hatia,Wafiwa ukawe mfariji wao..
Mfalme wa Amani ukatawale Nchi na mji huu tunaoishi,Ukatawale Tanzania,Afrika na Dudia yote..
Mungu baba ukawalinde na kuwaongoza watoto wetu kwenye Masomo wapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa..

Wale walikuwa likizo na Leo wamerudi Shule Baba wa mbinguni wakaanze nawe na kumaliza nawe,Ukawaokoe na kuwalinda katika ujana wao..wawe na Hofu yako Baba..
Baba wa mbinguni Tunakwenda kinyume na mwovu,Tunajikabidhi na kujiachilia mikononi mwako,Tukishukuru na Tukiamini kwamba wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina...!!!
Tuanze na Mungu..Mbarikiwe Sana.


1Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani. 2Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani. 3Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu. 4Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!” 5Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.

Esau anaoa mke wa tatu
6Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani. 7Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu. 8Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani. 9Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.

Ndoto ya Yakobo kule Betheli

10Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani. 11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala. 12Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo. 13Mwenyezi-Mungu alisimama juu ya ngazi hiyo,akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi unayoilalia nitakupa wewe na wazawa wako. 14Wazawa wako watakuwa wengi kama mavumbi ya dunia, na milki yao itaenea kila mahali: Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Kusini. Kwako jamii zote duniani zitabarikiwa. 15Mimi nipo pamoja nawe; nitakulinda popote uendapo na kukurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapotimiza ahadi niliyokupa.”
16Ndipo Yakobo akaamka usingizini, akasema, “Hakika, Mwenyezi-Mungu yupo mahali hapa, nami sikujua!” 17Yakobo akaogopa na kusema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu na lango la mbinguni.”
18Yakobo akaamka asubuhi na mapema, akachukua lile jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake, akalisimika kama nguzo na kuliweka wakfu kwa kulimiminia mafuta. 19Akapaita mahali hapo Betheli; lakini jina la awali la mji huo lilikuwa Luzu. 20Kisha Yakobo akaweka nadhiri akisema, “Iwapo, ee Mungu, utakuwa pamoja nami na kunilinda katika safari yangu, ukinipa chakula na mavazi 21ili nirudi nyumbani kwa baba yangu salama, basi, wewe Mwenyezi-Mungu utakuwa ndiwe Mungu wangu. 22Nalo jiwe hili nililosimika hapa kama nguzo, litakuwa nyumba yako Mungu, nami nitakupa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote utakavyonipa.”
Mwanzo28;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday 24 February 2017

Jikoni Leo; Na Da'Farhat- Chicken And Vegetable Spring Rolls In Kiswahili Na Best Homemade Whole Fried Fish In kiswahili


Haya Wapendwa/Waungwana ni siku nyingi kidogo tumekosa "Jikoni Leo"
Tuanze na Dada huyu na mapishi yake haya...

Karibuni...





Kama unayako mapishi unapenda nawengine wajifunze na kukufuatilia..usisite kututumi/kutujuulisha
Email;Rasca@hotmail.co.uk au unaweza kuni Inbox kwa mitandao ya kijamii, Natumia Rachelsiwa..


Zaidi;Farhat Yummy

"Swahili Na Waswahili"Pamoja Daima.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo27....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana,Yeye awezaye yote,Mfalme wa Amani,Mungu ni pendo apenda watu,Anayefanya njia pasipo na njia,
Akisema atakubariki na atafanya hivyo,Unastahili kuabudiwa,Kutukuzwa Baba wa mbinguni,Wewe Uliyetuumba,wewe ni habari njema,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Kuamka wazima na wenye Afya ni kwa Neema/Rehema ya Mungu tuu na si kwa uwezo,Nguvu/Utashi na uelewa wetu,Mungu wetu si mtu hata aseme uongo,Ahadi zake ni Amina na kweli..


Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako naye atakutegemeza,Kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.{Zaburi55;22]
Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako,Mtumainiye yeye naye atafanya kitu.{Zaburi37:5}
Sasa ndugu yangu mpendwa yanini kutangatanga,Kujibebesha mizigo isiyo yako na usiyoiweza?Mpe leo maisha yako Mungu ukiamini na yeye anatosha, na kufuata njia zake kamwe hatokuacha, Furaha ipo kwakwe,Tumaini ni yeye,Upendo wa kweli unapatikana kwakwe,Faraja ya kweli ipo kwa Mungu...
Mtumainiye Mqwenyezi-Mungu na kutenda mema,Upate kuishi katika nchi na kuwa salama{Zaburi37:3}
Mungu akatubariki kuingiakwetu/Kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri na Tutembeapo,Vilaji/Vinywaji,Kazi,Biashara,Elimu na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Mungu akavitakase na kuvifunika na damu ya Mwokozi..


Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, nadamu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.{1Yohane 1:7}

Tunajiachilia Mikononi mwako Baba wa Mbingu,Tukishukuru na Kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
                                      Amina..!!
                                       Mungu akaonekane kwenye Maisha yenu.
                                    


Isaka anambariki Yakobo

1Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” 2Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. 3Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. 4Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.”
5Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, 6Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, 7amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. 8Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. 9Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. 10Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.”
11Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina. 12Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.” 13Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.”
14Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. 15Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. 16Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. 17Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha.
18Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” 19Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” 20Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
21Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” 22Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” 23Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. 24Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” 25Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. 26Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” 27Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema,
“Tazama, harufu nzuri ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu!
28Mungu akumiminie umande wa mbinguni;
akupe ardhi yenye rutuba,
nafaka na divai kwa wingi.
29Jamii za watu zikutumikie,
na mataifa yakuinamie kwa heshima.
Uwe mtawala wa ndugu zako,
watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima.
Kila akulaaniye na alaaniwe,
kila akubarikiye na abarikiwe!”

Esau anaomba baraka

30Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni. 31Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!” 32Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.” 33Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!”
34Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!” 35Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.” 36Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?” 37Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?” 38Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa. 39Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia,
“Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba,
na mbali na umande wa mbinguni.
40Utaishi kwa upanga wako,
na utamtumikia ndugu yako;
lakini utakapoasi
utaivunja kongwa yake shingoni mwako.”
41Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.” 42Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua. 43Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani. 44Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa. 45Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?”

Yakobo anatumwa kwa Labani

46Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?”
Mwanzo27;1-46

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 23 February 2017

Chaguo La Mswahili Leo;Tina Campbell featuring Teddy Campbell SPEAK THE WORD

Tina na Mume wake Teddy..wimbo umenigusa/nimeupenda...
Swali..wewe Mke/Mume kipi mnafanya pamoja ukiacha kulala pamoja?


"Speak The Word".....Twende pamoja.



"Swahili Na Waswahili"Burudika.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo26..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeanza siku hii vyema na Mungu yu pamoja nanyi..
Asante Mungu wetu kwa kutupa kibali cha kuiona leo hii..Tunaomba Baba ukaibariki siku hii na Kutuongoza kwa kila jambo..Ikawe yenye Baraka,Amani na Imani..Ukatamalaki Mungu Baba katika Maisha yetu,Kazi,Biashara,Elimu,Familia na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba ukavitakase na ukavifunike na Damu yako ..Ukabariki kuingia/kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri na tutembeapo,vilaji/vinywaji...
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena na kutenda.. ukatufanye chombo chako Baba wa mbingu na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukawaguse na kuwaponya wanaopitia Magumu/Majaribu, Vifungo mbalimbali vya mwovu,Shida/Tabu,Wagonjwa walio mahospitalini/majumbani,walio magerezani pasipo na hatia..
Wafiwa ukawe mfariji wao,Waliokata tamaa wakapate Tumaini.
Hakuna linaloshindika mbele zako Mfalme wa Amani,Ukatawale na kuibariki Nchi hii tunayoishi,Ukabariki Tanzania,Afrika na Dunia yote Mfalime wa Amani ukatawale na kuwaongoza vyema wanaotuongoza wakatuongoze kwa haki na kweli.
Tunakwenda kinyume na mwovu..
Tunakuja mbele zako na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tukishukuru na kuamini kwamba wewe ni Bwana na Mwokozi wetu.
Amina...!!!

Amani ya Bwana ikae nanyi Daima.


Isaka anahamia Gerari

1Baadaye palitokea njaa nchini humo, njaa tofauti na ile ya hapo awali wakati wa uhai wa Abrahamu. Isaka akaenda Gerari kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti. 2Mwenyezi-Mungu akamtokea Isaka na kumwambia, “Usiende Misri, bali kaa katika nchi nitakayokuambia. 3Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa nawe na kukubariki. Nitatimiza ahadi niliyompa baba yako Abrahamu, kwani nitakupa wewe na wazawa wako nchi hizi zote. 4Nitawazidisha wazawa wako wawe kama nyota za mbinguni na kuwapa nchi hizi zote. Kutokana na wazawa wako, mataifa yote duniani yatabarikiwa, 5kwa sababu Abrahamu alinitii mimi, akazingatia maagizo yangu, amri zangu, masharti yangu na sheria zangu.”
6Basi, Isaka akakaa huko Gerari. 7Watu wa huko walipomwuliza habari za mkewe, yeye alijibu, “Huyu ni dada yangu.” Aliogopa kusema kwamba ni mke wake kwa kuogopa kwamba wakazi wa nchi wangemuua kwa sababu ya Rebeka, maana Rebeka alikuwa mzuri sana. 8Baada ya kukaa huko kwa muda mrefu, Abimeleki mfalme wa Wafilisti alichungulia dirishani akamwona Isaka akimkumbatia mkewe Rebeka. 9Abimeleki akamwita Isaka na kumwambia, “Kumbe huyo ni mke wako! Mbona ulisema ni dada yako?” Isaka akajibu, “Kwa kuwa niliogopa kwamba ningeuawa kwa sababu yake.”
10Abimeleki akamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilotutendea? Mmoja wa watu wangu angaliweza kulala na mkeo bila wasiwasi, nawe ungekuwa umetutia hatiani.” 11Ndipo Abimeleki akawaonya watu wote akisema, “Yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake, atauawa.”
12Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki, 13naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana. 14Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu. 15Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai. 16Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.”
17Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko. 18Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake. 19Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika, 20wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye. 21Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna. 22Kisha Isaka akaenda mahali pengine na kuchimba kisima kingine. Lakini hicho hawakukigombania; hivyo Isaka akakiita Rehobothi akisema, “Sasa Mwenyezi-Mungu ametuachia nafasi, nasi tutastawi katika nchi hii.”
23Kutoka huko, Isaka alikwenda Beer-sheba. 24Usiku huohuo Mwenyezi-Mungu alimtokea na kumwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako Abrahamu. Usiogope kwa kuwa niko pamoja nawe; nitakubariki na kuwazidisha wazawa wako kwa ajili ya Abrahamu, mtumishi wangu.” 25Kwa hiyo, Isaka akajenga huko madhabahu, akamwabudu Mwenyezi-Mungu. Akapiga kambi huko; na watumishi wake wakachimba kisima.

Isaka na Abimeleki wanapatana

26Abimeleki alitoka Gerari akiwa pamoja na Ahuzathi, mshauri wake, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, akamwendea Isaka. 27Isaka akawauliza, “Kwa nini mmekuja kwangu hali mnanichukia na mlinifukuza kwenu?” 28Wao wakamjibu, “Tumeona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe. Kwa hiyo, tunafikiri inafaa tule kiapo pamoja nawe na kufanya agano, 29kwamba hutatudhuru, nasi kadhalika hatutakudhuru. Tulikutendea mema, tukakuacha uende zako kwa amani, bila kukutendea baya lolote lile. Na sasa wewe ni mbarikiwa wa Mwenyezi-Mungu.” 30Basi, Isaka akawafanyia karamu, nao wakala na kunywa. 31Kesho yake wakaamka asubuhi na mapema na kula kiapo. Kisha Isaka akawasindikiza na kuagana nao kwa amani. 32Siku ileile watumishi wa Isaka walimjia na kumpasha habari za kile kisima walichokuwa wamechimba, wakasema, “Tumepata maji!” 33Basi, Isaka akakiita kisima hicho Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba hata leo.

Wake za Esau

34Esau alipokuwa na umri wa miaka arubaini, alioa wake wawili Wahiti: Yudithi bintiye Beeri, na Basemathi bintiye Eloni. 35Wanawake hao waliyafanya maisha ya Isaka na Rebeka kuwa machungu.
Mwanzo26;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.