Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 8 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo35....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mtakatifu Mtakatifu Baba wa Mbinguni, Muumba Mbingu na Nchi, Muumba wetu, Muweza wa yote,Mungu wetu na Baba Yetu,Mwokozi na Mponyaji wetu..Tunasema asante Baba kwa kibali chako ulichotupa cha kuendelea kuiona siku hii..Shukrani na utufu ni kwako Baba, Mfalme wa Amani ukatawale siku hii na maisha yetu yawe juu yako,Ukatuongoze tuingiapo/Tutokapo,Hatua zetu ziwe nawe,Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Baba ukavitakase na damu ya Mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu..
Ukatusamehe pale tulipoenda kinyume nawe Baba..
Nasi ukatupe kuweza kuwasamehe waliotukosea...
Ukatupe sawasawa na mapenzi yako...
Tukatumike kama chombo chako na kutuongoza katika Kunena/kutenda..

Wema wako ,Fadhili zako, Upendo na Neema/Rehema zisipungue..
Kwakuwa Ufalme ni Wako,Nguvu na Utukufu ni wako Baba..

Wema wa Mungu
5Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni;
uaminifu wako wafika mawinguni.
6Uadilifu wako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama
7Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako!
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
8Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;
wawanywesha kutoka mto wa wema wako.
9Wewe ndiwe asili ya uhai;
kwa mwanga wako twaona mwanga.
10Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua;
uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.
11Usikubali wenye majivuno wanivamie,
wala watu waovu wanikimbize.
12Kumbe watendao maovu wameanguka;
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.
                   [Zaburi 36:5-12]
Tunashukuru na kukusifu..Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa mbinguni, Tukishukuru na kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina....!!!!

Yakobo anahamia Betheli

1Siku moja, Mungu alimwambia Yakobo, “Anza safari, uende kuishi Betheli na kunijengea humo mahali pa kunitambikia mimi Mungu niliyekutokea wakati ulipomkimbia kaka yako Esau.” 2Basi, Yakobo akawaambia jamaa yake na wote aliokuwa nao, “Tupilieni mbali sanamu za miungu ya kigeni mlizo nazo, mjitakase na kubadili mavazi yenu. 3Kisha, tutakwenda Betheli ili nimjengee mahali pa kumtambikia Mungu aliyenisaidia siku ya taabu, Mungu ambaye amekuwa nami popote nilipokwenda.” 4Basi, wakampa Yakobo sanamu zote za miungu ya kigeni walizokuwa nazo pamoja na vipuli walivyokuwa wamevaa masikioni; naye akavifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
5Yakobo na wanawe walipokuwa wanasafiri, Mungu aliwatia hofu wenyeji wa miji yote ya jirani hata hawakuthubutu kuwafuatia. 6Basi, Yakobo akawasili Luzu yaani Betheli katika nchi ya Kanaani, pamoja na watu wote aliokuwa nao. 7Akajenga hapo madhabahu na kupaita El-betheli kwani hapo ndipo mahali Mungu alipojionesha kwake wakati alipokuwa akimkimbia kaka yake. 8Debora, mlezi wa Rebeka, alifariki, akazikwa chini ya mwaloni upande wa kusini wa Betheli. Kwa hiyo Yakobo akauita mji huo Alon-bakuthi.
9Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. 10Mungu alimwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa hivyo tena, bali sasa jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo Yakobo akaitwa Israeli. 11Tena Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu mwenye nguvu. Ujaliwe wazawa wengi; kwako wewe kutatokea taifa, mataifa na wafalme. 12Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaka, nitakupa wewe na wazawa wako.” 13Basi, baada ya kuongea na Yakobo, Mungu akamwacha na kupanda juu. 14Yakobo akasimika nguzo ya jiwe la ukumbusho mahali hapo Mungu alipozungumza naye, akaiweka wakfu kwa kuimiminia tambiko ya kinywaji na mafuta. 15Basi, Yakobo akapaita mahali hapo alipozungumza na Mungu Betheli.

Kuzaliwa kwa Benyamini na kifo cha Raheli

16Yakobo na jamaa yake yote waliendelea na safari yao kutoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efratha, Raheli akashikwa na uchungu mkali wa kuzaa. 17Naye alipokuwa katika uchungu huo, mkunga akamwambia, “Usiogope, umepata mtoto mwingine wa kiume.” 18Raheli huku akikata roho, akampa huyo mtoto jina Ben-oni. Lakini baba yake akamwita mtoto huyo Benyamini. 19Basi, Raheli akafariki na kuzikwa kando ya njia iendayo Efratha (yaani Bethlehemu). 20Yakobo akasimika nguzo ya kumbukumbu juu ya kaburi la Raheli ambayo ipo mpaka leo. 21Israeli akaendelea na safari yake na kupiga kambi yake baada ya kuupita mnara wa Ederi.
22Wakati Israeli alipokuwa anakaa nchini humo, mwanawe Reubeni, alilala na Bilha, suria wa baba yake; naye Israeli akasikia habari hizo.

Wana wa Yakobo

(1Nya 2:1-2)

Yakobo alikuwa na watoto wa kiume kumi na wawili. 23Wana wa Lea walikuwa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zebuluni. 24Watoto wa kiume wa Raheli walikuwa Yosefu na Benyamini. 25Watoto wa kiume waliozaliwa na Bilha, mjakazi wa Raheli, walikuwa Dani na Naftali. 26Na watoto wa kiume waliozaliwa na Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hao ndio watoto wa kiume wa Yakobo, aliowazaa alipokuwa kule Padan-aramu.

Kifo cha Isaka

27Yakobo aliondoka akaenda Mamre kwa baba yake Isaka, huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, mahali ambapo Abrahamu na Isaka walikaa kama wageni. 28Isaka alikuwa na miaka 180 29akafariki akiwa mzee wa miaka mingi. Watoto wake, Esau na Yakobo wakamzika.
Mwanzo35;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 7 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo34

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Asante Mungu wetu kwa siku hii njema ,Umetupa kibali chako na kutuchagua kuiona leo hii..Tunashukuru Baba wa Mbinguni kwa Neema/Rehema hii..Tunaomba ukaibariki siku hii na ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri,Hatua zetu,Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Vyote tutavyogusa/tumia baba ukavitakase..
Kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu Ikatutakase Miili yetu,Akili zetu na kutuokoa..

Ndiyo maana Yesu pia,Kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe,Aliteswa na kufa nje ya mji.[Waebrania 13;12]


Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda..
Baba ukatusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakujua/kutojua,kuwaza na kunena..
Baba wa mbinguni ukawaponye/kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo vya mwovu,Shida/Tabu ukawaweke huru na ukaonekane kwenye maisha yao..

Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa nao,Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao[Waebrania 13;3]

Endeleeni kutembea katika njia iliyo nyoka,Ili kile kilicho lemaa kisiumizwe bali kiponywe[Waebrania 12;13]

Tunajiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni tukishukuru na kuamini wewe ni Bwana na mwokozi wetu..
Amina...!!!
Yesu Kristo ni  yuleyule jana,Leo na hata milele[Waebrania 13:8]
Tunawatakieni nyote neema ya Mungu[Waebrania13;25]


Simeoni na Lawi wanalipiza kisasi kwa ajili ya dada yao

1Siku moja, Dina, binti yake Yakobo na Lea, alikwenda kuwatembelea wanawake wa nchi hiyo. 2Basi, Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, aliyekuwa mkuu wa nchi hiyo, alipomwona Dina, akamshika, akalala naye kwa nguvu. 3Lakini Shekemu akavutiwa sana na huyo msichana, akampenda hata akaanza kumbembeleza. 4Kwa hiyo, Shekemu akazungumza na Hamori baba yake, akamwambia, “Tafadhali, niombee huyo msichana nimwoe.”
5Yakobo akapata habari kwamba Dina, bintiye, alikuwa amenajisiwa na Shekemu; lakini kwa kuwa wanawe walikuwa malishoni, alinyamaza mpaka waliporudi. 6Hamori, baba yake Shekemu, akaenda kwa Yakobo ili azungumze naye, 7na wakati huohuo watoto wa kiume wa Yakobo wakawa wanarudi nyumbani kutoka malishoni. Waliposikia hayo, vijana hao wakaona uchungu mwingi na kukasirika sana, kwa vile Shekemu alikuwa amewafanyia watu wa Israeli ovu hilo la kulala na binti ya Yakobo, maana jambo hilo lilikuwa mwiko.
8Lakini Hamori akawaambia, “Mwanangu Shekemu anampenda sana binti yenu. Basi, tafadhali mumruhusu amwoe. 9Acheni tuoane: Nyinyi mtatuoza binti zenu, nasi tutawaoza binti zetu. 10Kwa hiyo mtaishi pamoja nasi; mtakuwa huru katika nchi hii. Mtaishi humu, mfanye biashara na kujipatia mali.” 11Hali kadhalika, Shekemu akawaambia baba na ndugu zake Dina, “Tafadhali, mniwie radhi, nami nitawapeni chochote mtakachosema. 12Niambieni kiasi chochote cha mahari na zawadi, hata kikiwa kikubwa namna gani, nami nitatoa, mradi tu mnioze msichana huyu.”
13Basi, watoto wa kiume wa Yakobo wakamjibu Shekemu na baba yake Hamori kwa hila, kwa kuwa Shekemu alikuwa amekwisha mnajisi dada yao Dina. 14Waliwaambia, “Hatuwezi kumwoza dada yetu kwa mtu asiyetahiriwa. Kufanya hivyo ni aibu kwetu. 15Tutakubaliana nanyi tu kwa sharti hili: Kwamba mtakuwa kama sisi kwa kumtahiri kila mwanamume miongoni mwenu. 16Hapo ndipo tutakapowaoza binti zetu na kuwaoa binti zenu; tutaishi pamoja nanyi na kuwa jamaa moja. 17Lakini msipokubaliana nasi na kutahiriwa, basi, sisi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.”
18Pendekezo lao likawapendeza Hamori na mwanawe Shekemu. 19Kijana huyo hakusita hata kidogo kutekeleza sharti hilo, kwa vile alivyompenda binti wa Yakobo. Isitoshe, Shekemu ndiye aliyeheshimika kuliko wote nyumbani kwao.
20Basi, Hamori na mwanawe, Shekemu, wakaenda kwenye lango la mji, mahali pa mikutano, wakaongea na watu wao wakisema, 21“Watu hawa ni marafiki zetu. Tuwakaribishe waishi nchini mwetu na kufanya biashara, kwa sababu tunayo nchi ya kututosha sisi na wao pia; kisha tutaoa binti zao na kuwaoza binti zetu. 22Lakini wao watakubali kuishi nasi na tutakuwa jamaa moja kwa sharti hili: Kwamba tutamtahiri kila mwanamume miongoni mwetu kama wao walivyotahiriwa. 23Je, hamwoni kwamba mifugo yao na mali yao yote itakuwa mali yetu? Haya, tukubaliane nao ili wakae pamoja nasi.” 24Wanaume wote waliokusanyika penye lango la mji huo wakakubaliana na Hamori na mwanawe Shekemu. Kisha, wanaume wote wakatahiriwa.
25Siku tatu baadaye, waliotahiriwa wakiwa bado wana maumivu makali, watoto wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, kaka zake Dina, walizitwaa panga zao, wakauvamia mji ghafla na kuwaua wanaume wote. 26Waliwaua kwa upanga Hamori na mwanawe Shekemu, wakamtoa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakaenda zao. 27Baada ya mauaji hayo, watoto wengine wa kiume wa Yakobo waliingia mjini na kuuteka nyara mji huo, kwa sababu dada yao alikuwa amenajisiwa. 28Walichukua kondoo na mbuzi, ng'ombe, punda na chochote kilichokuwa mjini au shambani. 29Waliteka nyara mali yote, watoto na wanawake wote na chochote kilichokuwa majumbani.
30Basi, Yakobo akamwambia Simeoni na Lawi, “Nyinyi mmeniletea taabu kwa kunifanya nichukiwe na wakazi wa nchi hii ya Wakanaani na Waperizi. Mimi sina watu wengi, na kama wakikusanyika kunishambulia wataniangamiza mimi pamoja na jamaa yangu.” 31Hao ndugu wawili wakajibu, “Ana haki gani ya kumtendea dada yetu kama malaya?”
Mwanzo34;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 6 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo33...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Natumaini mmeanza Wiki/Siku hii  na Mungu..
Tunamshukuru ee Mungu wetu,Muumba wetu na Muumba Mbingu na Nchi,

Baba wa Yatima,Mume wa Wajane,Mfalme wa Amani, Mungu asiye lala wala kusinzia,Aponyaye/Aokoae,Yeye ni mlinzi mkuu,Yeye atupaye Ridhiki zetu,Yeye ni muweza wa yote, Hakuna wa kufanana naye
Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Munguhakuna yeyote aliye kama yeye; hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu.[1Samueli 2:2]
                      Asante Mungu Baba kwa  kutuchagua tena na kutupa Kibali cha kuiona siku hii tena,Si kwa uwezo,Nguvu/Utashi,kwamba sisi ni wema sana ni Neema/Rehema zako Baba wa Mbingu.....
Baba tunaikabidhi siku hii na tunajiachilia mikononi mwako,Roho wa Mungu akatuongoze katika Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri,tutembeapo/hatua zetu ziwe nawe,Tuingiapo/Tutokapo,Vinywaji/Vilaji..Kunena/kutenda..
Ukatutakase Miili yetu,Akili zetu na Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Ukawaguse/Kuwaokoa wote wanaopitia Magumu/Majaribu,vifungo vya mwovu,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,wenye Shida/Tabu...


Anawahurumia watu dhaifu na fukara, anayaokoa maisha yao wenye shida.[Zaburi 72:13]
Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima.[Zaburi 10:14]
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.[Waroma 12:12]
Ukatupe sawasaswa na mapenzi yako.
Tunayaweka haya mikononi mwako Tukiamini na Kushuru...Amina..!!!
                    
Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina. Maneno ya mwisho[Waebrania 13:21]      


Yakobo anakutana na Esau

1Basi, Yakobo alitazama, akamwona Esau akija pamoja na watu 400. Hapo, akawagawa watoto wake kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wawili. 2Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Raheli na mwanawe Yosefu. 3Kisha yeye mwenyewe akawatangulia, akaenda akiinama mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake.
4Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia. 5Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.”
6Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima. 7Hali kadhalika Lea akaja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Hatimaye, Raheli na Yosefu wakaja, wakainama kwa heshima.
8Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.” 9Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.” 10Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa. 11Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.
12Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.” 13Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa. 14Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.”
15Hapo Esau akasema, “Heri nikuachie baadhi ya watu wangu.” Lakini Yakobo akasema, “Kuna haja gani ya kufanya hivyo? Yanitosha kwamba mimi nimepata fadhili yako, ewe bwana wangu.” 16Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri. 17Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukothi, na huko akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo, mahali hapo pakaitwa Sukothi.
18Kutoka Padan-aramu, Yakobo alifika salama mjini Shekemu, katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi yake karibu na mji huo. 19Sehemu hiyo ya ardhi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazawa wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. 20Huko, akajenga madhabahu na kupaita Mungu ni Mungu wa Israeli.
Mwanzo33:1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday 5 March 2017

Jumapili Indelee Vyema;Burudani-Mireille Basirwa - Tunashuka na nyingine..




Wapendwa/Waungwana nimatumaini yangu mmekuwa na siku njema,Basi Mungu andelee kuwabariki awalinde na kuwaokoa katika yote..Bwana akaonekane katika maisha yenu,Muendelee kupokea Neema ya Mungu
Roho mtakatifu akawaongoze katika yote..
.
Awape sawaswa na Mapenzi yake..


Mpendwa wetu Da'Mireille Basirwa alifiwa na mtoto wake hivi karibuni..Pole sana Mpendwa ,Tunamuomba Mungu aendelee kukufariji na kukupa Nguvu, Uvumilivu wakati wote..

Neno La Leo;Zaburi 34:1-22


Sifa kwa wema wa Mungu
(Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki)
1Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
2Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,
wanyonge wasikie na kufurahi.
3Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,
sote pamoja tulisifu jina lake.
4Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,
na kuniondoa katika hofu zangu zote.
5Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;
nanyi hamtaaibishwa kamwe.
6Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,
na kumwokoa katika taabu zake zote.
7Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,
na kuwaokoa katika hatari.
8  Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.
Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
9Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;
maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.
10Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;
lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
11Njoni enyi vijana mkanisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.
12  Je, watamani kufurahia maisha,
kuishi maisha marefu na kufurahia mema?
13Basi, acha kusema mabaya,
na kuepa kusema uongo.
14Jiepushe na uovu, utende mema;
utafute amani na kuizingatia.
15Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,
na kusikiliza malalamiko yao;
16lakini huwapinga watu watendao maovu,
awafutilie mbali kutoka duniani.
17Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,
na kuwaokoa katika taabu zao zote.
18Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
19Mateso ya mwadilifu ni mengi,
lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.
20  Huvilinda viungo vya mwili wake wote,
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
21Ubaya huwaletea waovu kifo;
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
22Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.














"Swahili Na Waswahili"Pamoja.

Friday 3 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo32..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?

Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu, tumshangilie mwamba wa wokovu wetu! Twende mbele zake na shukrani; tumshangilie kwa nyimbo za sifa. Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu; yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake, vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya; kwa mikono yake aliiumba nchi kavu. Njoni tusujudu na kumwabudu; tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu! Maana yeye ni Mungu wetu, nasi ni watu wa kundi lake, ni kondoo wake anaowachunga. Laiti leo mngesikiliza sauti yake: “Msiwe wakaidi kama kule Meriba, kama walivyokuwa kule Masa jangwani, wazee wenu waliponijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea. Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao, nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka! Hawajali kabisa njia zangu!’ Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’”
[Zaburi 95:1-11]
Asante Baba wa Mbinguni kwa Neema/Rehema na Kibali ulichotupa, Umetuchagua kuiona tena siku hii Baba..
Shukrani na utukufu ni kwako wewe uliyeumba Mbingu na Nchi,Uliyetufanya kama tulivyo..
Ulitulinda jana, Leo ni siku mpya na Kesho ni yako Muumba wetu..
Si kwauwezo wetu Nguvu/Utashi, au sisi ni wema sana Baba ni kwa mapenzi na uweza wako Jehovah..
Tunakwenda kinyume na mwovu..Tunajiachilia mikononi mwako Mfalme wa  Amani..Utusamehe dhambi zetu zote tunazozijua,tusizozijua,tulizonena na tulizowaza...Ukatutakase Baba miili yetu,Akili zetu na Roho Mtakatifu akatuongoze katika Kunena na Kutenda...
Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa.[Waroma 3:24]

Ukatubariki Baba Tuingiapo/Tutokapo,Vyombo vya usafiri,Tutembeapo, Hatua zetu,Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vilaji/Vinywaji...
Ukawaponye na Kuwagusa Wagonjwa Baba,Wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu,walio kweye vifungo vyovyote,Wafiwa ukawe mfariji wao...

Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.[Waefeso 2:8]

Tunarudisha Shukrani na Utukufu kwako na Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..


Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;[Waebrania 12:28]

                            Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema yaMungu.[Tito 3:15]
                       

                          Amina....!!
Yakobo ajitayarisha kukutana na Esau

1Yakobo aliendelea na safari yake. Basi, malaika wa Mungu wakakutana naye. 2Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu.
3Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu. 4Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa. 5Nina ng'ombe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’”
6Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.” 7Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia, 8akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.”
9Kisha Yakobo akamwomba Mungu akisema, “Ee Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka! Ewe Mwenyezi-Mungu uliyeniambia nirudi katika nchi yangu kwa jamaa yangu, ukaniahidi kunitendea mema, 10sistahili hata kidogo fadhili ulizonipa kwa uaminifu mimi mtumishi wako. Nilipovuka mto Yordani, sikuwa na kitu ila fimbo; lakini sasa ninayo makundi haya mawili. 11Nakuomba uniokoe sasa kutoka kwa ndugu yangu Esau, maana nina hofu kuwa atatushambulia na kutuua sote, akina mama pamoja na watoto. 12Wewe uliniahidi kunitendea mema na kuwafanya wazawa wangu wawe wengi kama mchanga wa bahari ambao hauhesabiki kwa wingi wake.”
13Basi, Yakobo akalala hapo usiku huo. Kisha akatenga sehemu ya mali yake, iwe zawadi kwa ndugu yake Esau: 14Mbuzi majike 200 na mabeberu 20, kondoo majike 200 na madume 20, 15ngamia 30 wanyonyeshao pamoja na ndama wao, ng'ombe majike 40 na mafahali kumi, na punda majike 20 na madume kumi. 16Akawakabidhi watumishi wake, kila mmoja kundi lake, akawaambia, “Nitangulieni mkiacha nafasi kati ya kundi na kundi katika msafara wenu.” 17Akamwagiza yule aliyetangulia, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani? Unakwenda wapi? Na wanyama hawa ni wa nani?’ 18Wewe utamjibu, ‘Hii ni mali ya mtumishi wako Yakobo, nayo ni zawadi yako wewe bwana wangu Esau. Tena Yakobo mwenyewe yuko nyuma anafuata.’” 19Akatoa agizo hilohilo kwa mtumishi wa kundi la pili na la tatu na wengine wote, akisema, “Mtamwambia Esau maneno hayohayo mtakapokutana naye. 20Zaidi ya yote, mtamwambia, ‘Mtumishi wako Yakobo yuko nyuma, anafuata.’” Yakobo alifanya hivyo akifikiri, “Pengine nitamtuliza kwa zawadi hizi ninazomtangulizia, na baadaye naweza kuonana naye ana kwa ana; huenda atanipokea.” 21Basi, akatanguliza zawadi zake, lakini yeye mwenyewe akalala kambini usiku huo.

Pambano usiku

22Usiku huohuo Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili na watoto wake kumi na mmoja, akapita kivuko cha Yaboki. 23Baada ya kuwavusha ngambo ya kijito wale waliokuwa nao na mali yake yote, 24Yakobo alibaki peke yake. Mtu mmoja akaja, akapigana naye mwereka mpaka alfajiri. 25Mtu huyo alipoona kwamba hawezi kumshinda Yakobo, alimgusa Yakobo nyonga ya kiuno, naye akateguka alipokuwa anapigana naye mwereka. 26Kisha yule mtu akamwambia Yakobo, “Niache niende zangu, kwani kunapambazuka.” Lakini Yakobo akamwambia, “Sikuachi kamwe, mpaka umenibariki!” 27Naye akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akamjibu, “Yakobo.” 28Yule mtu akamwambia, “Hutaitwa Yakobo tena, bali Israeli, kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu, ukashinda.” 29Ndipo Yakobo akamwambia, “Tafadhali, nakuomba uniambie jina lako.” Lakini yeye akamwambia, “Ya nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki Yakobo. 30Yakobo akapaita mahali hapo Penueli, akisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, nami sikufa.” 31Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Yakobo alipoondoka Penueli; akawa anachechemea kwa sababu ya kiuno chake. 32Ndiyo maana mpaka leo Waisraeli hawali msuli wa nyonga, kwa maana yule mtu alimgusa Yakobo panapo nyonga katika msuli wa kiuno chake.
Mwanzo32:1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 2 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo31...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu wetu Muumba wetu, muumba wa Mbingu na Nchi,

Yeye aliyetupa kibali cha kuiona siku hii..
‘Baba yetu uliye mbinguni:

Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
11Utupe leo chakula chetu cha kila siku.
12Utusamehe makosa yetu,
kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea.
13Usitutie katika majaribu,
lakini utuokoe na yule Mwovu.’ [

Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]
                      [Mathayo6;9-13]
                                      Mungu awe nanyi Daima.



Yakobo amtoroka Labani


1Basi, ikasikika kwamba watoto wa kiume wa Labani walinungunika na kusema, “Yakobo amenyakua kila kitu cha baba yetu; ndivyo alivyopata kuwa tajiri.” 2Yakobo alijua pia kuwa Labani hakumjali yeye kama hapo awali. 3Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya wazee wako na kwa jamaa yako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
4Basi Yakobo akataka Raheli na Lea waitwe; nao wakamwendea mbugani alikokuwa anachunga wanyama. 5Yakobo akawaambia, “Naona kuwa baba yenu hanijali tena kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. 6Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote. 7Hata hivyo yeye amenidanganya na kuubadilisha ujira wangu mara kumi. Lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru. 8Kila mara baba yenu aliposema, ‘Wanyama wenye madoadoa ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi kundi lote lilizaa wanyama wenye madoadoa. Na kila aliposema, ‘Wanyama wenye milia ndio watakaokuwa ujira wako,’ basi, kundi lote lilizaa wanyama wenye milia. 9Ndivyo Mungu alivyochukua wanyama wa baba yenu, akanipa mimi.
10“Wakati wa majira ya wanyama kupata mimba niliota ndoto, na katika ndoto hiyo niliona mabeberu wote waliopanda majike walikuwa wenye milia, madoadoa na mabakamabaka. 11Malaika wa Mungu akaongea nami katika ndoto hiyo, akaniita, ‘Yakobo,’ nami nikaitika, ‘Naam!’ 12Naye akaniambia, ‘Tazama mabeberu wote wanaowapanda majike wana milia, madoadoa na mabaka mabaka. Jambo hili limekuwa hivyo kwa sababu nimeona alivyokutendea Labani. 13Mimi ndimi yule Mungu aliyekutokea kule Betheli, mahali pale ulipoweka lile jiwe wakfu kwa kulimiminia mafuta na ambapo uliniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii urudi katika nchi yako.’”
14Raheli na Lea wakamjibu Yakobo, “Sisi hatuna tena sehemu au urithi wowote katika nyumba ya baba yetu! 15Aidha yeye anatuona sisi kama wageni, kwa maana ametuuza; na mali ileile tuliyonunuliwa nayo ndiyo anayotumia. 16Mali yote ambayo Mungu ameichukua kutoka kwa baba yetu ni yetu sisi na watoto wetu. Kwa hiyo, fanya hayo aliyokuagiza Mungu!”
17Basi, Yakobo akajitayarisha kusafiri, akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. 18Alichukua wanyama wake wote pamoja na mali yote aliyochuma huko Padan-aramu, akaanza safari ya kurudi nchini Kanaani kwa baba yake Isaka. 19Wakati huo Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya wanyama wake. Hivyo Raheli alipata nafasi ya kuiba vinyago vya miungu ya baba yake. 20Yakobo alimdanganya Labani, Mwaramu, kwa kuondoka bila kumjulisha. 21Basi, Yakobo akachukua mali yake yote, akatoroka. Baada ya kuvuka mto Eufrate, alielekea Gileadi, nchi ya milima.


Labani anamfuata Yakobo

22Siku tatu baadaye, Labani alijulishwa kwamba Yakobo amemtoroka. 23Basi, Labani akawachukua ndugu zake, akamfuata Yakobo kwa muda wa siku saba, akamkuta milimani, nchini Gileadi. 24Lakini usiku, Mungu akamtokea Labani, Mwaramu, katika ndoto, akamwambia, “Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya.”
25Basi, Labani akamfikia Yakobo. Wakati huo Yakobo alikuwa amepiga kambi yake milimani. Labani naye, pamoja na ndugu zake, akapiga kambi yake kwenye milima ya Gileadi. 26Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Mbona umenidanganya, ukawachukua binti zangu kama mateka vitani? 27Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa, wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi? 28Mbona hukunipa fursa ya kuwabusu kwaheri binti zangu na wajukuu zangu? Kweli umetenda kipumbavu! 29Nina uwezo wa kukudhuru; lakini Mungu wa baba yako alinitokea usiku wa kuamkia leo, akanitahadharisha akisema, ‘Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya’. 30Najua ulitoroka kwa sababu ya hamu kubwa ya kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?” 31Yakobo akamjibu, “Niliogopa kwa sababu nilidhani ungelininyanganya binti zako. 32Lakini utakayempata na vinyago vya miungu yako asiishi! Mbele ya hawa ndugu zetu, onesha chochote kilicho chako, ukichukue.” Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba vinyago vya miungu ya Labani.
33Basi, Labani akatafuta vinyago hivyo vya miungu yake katika hema la Yakobo, la Lea na la wale wajakazi wawili; lakini hakuvipata. Akatoka katika hema la Lea na kuingia hema la Raheli. 34Raheli alikuwa amevichukua hivyo vinyago, akavificha chini ya matandiko ya ngamia na kuketi juu yake. Labani akavitafuta katika hema lote; lakini hakuvipata. 35Ndipo Raheli akamwambia baba yake, “Samahani baba, usiudhike, kwani siwezi kusimama mbele yako kwa sababu nimo katika siku zangu.” Basi, Labani akavitafuta vinyago vya miungu yake, lakini hakuvipata.
36Ndipo Yakobo akakasirika, akamshutumu Labani akisema, “Kosa langu ni nini? 37Je, umepata nini kilicho chako hata baada ya kuipekua mizigo yangu yote? Kiweke mbele ya ndugu zangu na ndugu zako, ili wao waamue kati yetu sisi wawili! 38Nimekaa nawe kwa muda wa miaka ishirini; na muda huo wote kondoo wako, wala mbuzi wako hawajapata kuharibu mimba, wala sijawahi kula kondoo dume wa kundi lako. 39Mimi sikukuletea hata mara moja mnyama wako aliyeuawa na mnyama wa porini, bali nilifidia hasara hiyo mimi mwenyewe. Wewe ulinitaka nilipe bila kujali kama aliibiwa mchana au usiku! 40Hivyo, mchana nilistahimili jua kali na usiku baridi ilinipiga hata nisiweze kupata usingizi hata kidogo. 41Kwa miaka ishirini hii yote nimeishi nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita nikawachunga wanyama wako. Lakini wewe, ukabadilisha ujira wangu mara kumi. 42Kama Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu ambaye alimfanya baba yangu Isaka kutetemeka, asingelikuwa upande wangu, hakika ungeliniacha niondoke mikono mitupu. Lakini Mungu aliyaona mateso yangu na kazi niliyofanya kwa mikono yangu, akakukemea usiku wa kuamkia leo.”
43Hapo Labani akamjibu Yakobo, “Binti hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, wanyama hawa ni wanyama wangu, na yote unayoyaona hapa ni yangu. Lakini mimi ninaweza kufanya nini leo juu ya hawa binti zangu na watoto wao waliowazaa? 44Basi, tufanye agano mimi nawe, liwe ushahidi kati yako nami.”
45Basi, Yakobo akachukua jiwe, akalisimika kama nguzo ya ukumbusho. 46Tena Yakobo akawaambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Nao wakakusanya mawe na kufanya rundo. Kisha wakala chakula karibu na rundo hilo la mawe. 47Labani akaliita rundo hilo Yegar-sahadutha, lakini Yakobo akaliita Galeedi. 48Labani akasema, “Rundo hili ni ushahidi kati yako na mimi leo.” Kwa hiyo Labani akaliita Galeedi, 49na ile nguzo akaiita Mizpa akisema, “Mwenyezi-Mungu na atulinde tuwapo mbali bila kuonana. 50Kama ukiwatesa binti zangu, au ukioa wanawake wengine zaidi ya hawa, basi ujue kwamba hakuna aliye shahidi kati yetu ila Mungu mwenyewe.” 51Halafu Labani akamwambia Yakobo, “Tazama rundo hili la mawe na nguzo ambayo nimeisimika kati yako nami. 52Rundo hili ni ushahidi na nguzo hii ni ushahidi kwamba mimi sitavuka rundo hili kuja kwako kukudhuru, na wala wewe hutavuka rundo hili na nguzo hii kuja kwangu kunidhuru. 53Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, ataamua kati yetu.” Basi, Yakobo akaapa kwa Mungu ambaye alimfanya baba yake Isaka, kutetemeka. 54Kisha akatoa tambiko huko mlimani na kuwaalika ndugu zake wale chakula. Baada ya kula, wakabaki huko usiku kucha.
55Asubuhi na mapema Labani akaamka, akawabusu wajukuu na binti zake, akawabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.
Mwanzo31:1-55
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 1 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo30...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Asante Baba wa Mbinguni Muumba wetu Na Uliyeumba Mbingu na Nchi...
Muweza wa yote,Mungu usiyelala wala kusinzia,Baba wa Yatima,Mume wa wajane,Mwokozi wetu,Mungu wa Ibrahim,Yakobo na Isaka,Mungu wetu si kiziwi,Unaweza Baba, Unatosha Jehovah,

Mungu si mtu,aseme uongo,wala si binadamu,abadili nia yake!Je,ataahidi kitu na asikifanye,au kusema kitu asikitimize?[Hesabu23:19]

Na Mungu ambaye ni utukufu wa Israeli hadanganyi,wala habadili wazo lake.Yeye si binadamu hata abadili mawazo[1Samueli15:29]

Je miungu ya uongo ya mataifa yaweza kuleta mvua?Au,je,Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je, si wewe ee Mwenyezi-Mungu uliye Mungu wetu?Tunakuweka wewe tumaini letu,maana wewe unafanya haya yote.[Yeremia14:22]

Tunashukuru Baba kwa kutupa Neema/Rehema hii ya kuiona Leo..
Sisi ni nani Baba mpaka ukatupa nafasi hii tena,Sisi si kwamba ni wema sana, wenye nguvu/utashi na uwezo wetu kuiona siku hii Baba..
Ni kwa mapenzi yako tuu Baba wa Mbingu...
Ukaibariki na kutuongoza Baba wa Mbinguni,Ukatufanye chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako...


Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe,ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu.[2Wakorintho3:5]
Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza Neno la Mungu si kamili[1Wakorintho13:9]

Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe tulipo kwenda kinyume nawe na kutenda dhambi..
Utupe Neema ya kushinda dhambi Baba..
Ukatutakase na kutufunika na Damu yako iliyomwagika pale msalabani..
Tunajikabidhi na kujiachilia mikononi mwako ee Baba wa Mbingu..
Ukaanze nasi na kutuongoza katika Kazi,Biashara,Masomo..

Ukabariki Kuingia/kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri na tutembeapo/hatua zetu,Vilaji/Vinywaji na
Ukavitakase vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..

Wagonjwa,wafiwa,wanaopitia Magumu/majaribu,Vifungo vya shetani...

Mungu wetu akawaponye...
Msifikiri mkono wa Mungu ni mfupi,hata asiweze kuwaokoeni;au masikio yake yamezibika,hata asiweze kuwasikieni[Isaya59:1]

Mkono wa nguvu wa Mwenyeze-Mungu umeleta ushindi!Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu![Zaburi 118:16]
Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu,ili awainue wakati ufaao.
Basi,usiogope,mimi nipo pamoja nawe.Usifadhaike,mimi ni Mungu wako.Nitakuimarisha na kukusaidia;nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.[Isaya 41:10]
Amina..!!!!!
Muwe na wakati mwema.


1Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu Lea, dada yake, akamwambia Yakobo, “Nipatie watoto, la sivyo, nitakufa.” 2Yakobo akamkasirikia Raheli sana na kumwambia, “Je, mimi nimekuwa badala ya Mungu aliyekuzuia kupata watoto?” 3Raheli akamjibu, “Mjakazi wangu Bilha yupo. Lala naye ili azae watoto badala yangu, nami pia nipate watoto kutokana naye.” 4Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye. 5Bilha akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa kiume. 6Raheli akasema, “Mungu amenitendea sawa, amekisikia kilio changu na kunipa mtoto wa kiume.” Akamwita mtoto huyo Dani. 7Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. 8Hapo Raheli akasema, “Nimepigana miereka mikali na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Naftali.
9Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo ili awe mkewe. 10Zilpa akamzalia Yakobo mtoto wa kiume. 11Lea akasema, “Bahati njema.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Gadi.12Zilpa, mtumishi wa Lea, alimzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. 13Lea akasema, “Bahati njema! Sasa wanawake wataniita heri.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Asheri.
14Ikawa wakati wa mavuno ya ngano, Reubeni alikwenda shambani na huko akapata tunguja, akamletea mama yake Lea. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali, nipe baadhi ya tunguja za mwanao.” 15Lakini Lea akamsemea kwa ukali, “Je, unadhani ni jambo dogo kuninyanganya mume wangu, na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu?” Raheli akamjibu, “Ikiwa utanipa tunguja za mwanao, Yakobo atalala kwako leo.”
16Basi, jioni Yakobo alipokuwa anarudi toka shambani, Lea alitoka kwenda kumlaki, akamwambia, “Leo huna budi kulala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala kwa Lea usiku huo. 17Mungu akasikiliza ombi la Lea, naye akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa tano wa kiume. 18Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu kwa sababu nilimpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Isakari. 19Lea akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa sita wa kiume. 20Akasema, “Mungu amenipa zawadi bora. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa maana nimemzalia watoto sita wa kiume.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Zebuluni.21Baadaye akazaa mtoto wa kike, akamwita Dina.
22Kisha Mungu akamkumbuka Raheli, akalikubali ombi lake na kumjalia kupata watoto. 23Raheli akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.” 24Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Yosefu akisema, “Mwenyezi-Mungu na aniongezee mtoto mwingine wa kiume.”

Yakobo anatajirika

25Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Niruhusu nirudi nyumbani, katika nchi yangu. 26Nipe wake zangu na watoto wangu ambao nimejipatia kutokana na utumishi wangu kwako, niondoke nao. Unajua kwamba nimekutumikia vema.” 27Lakini Labani akamwambia, “Hebu niruhusu nami niseme. Nimetambua kwa kuagua kwamba Mwenyezi-Mungu amenibariki kwa sababu yako. 28Taja ujira wako, nami nitakulipa.” 29Yakobo akamwambia, “Wewe mwenyewe unajua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi nilivyowatunza wanyama wako. 30Kwa kuwa kabla sijaja ulikuwa na mali chache tu lakini tangu nifike, mali yako imeongezeka kwa wingi sana, na Mwenyezi-Mungu amekubariki kila nilikokwenda. Lakini sasa, nitaitunza lini jamaa yangu mwenyewe?”
31Labani akamwuliza, “Nikupatie nini?” Yakobo akamjibu, “Hutanipatia chochote. Nitaendelea kuwatunza wanyama wako ikiwa utanifanyia jambo hili: 32Niruhusu nipite kati ya wanyama wako wote leo, nitenge katika kundi kila kondoo mwenye madoadoa na mabakamabaka, kila kondoo mweusi, na mbuzi walio na madoadoa na mabakamabaka. Huo ndio utakaokuwa ujira wangu. 33Hivyo, siku zijazo, uaminifu wangu utaonekana waziwazi utakapokuja kuuangalia ujira wangu. Mbuzi yeyote asiye na madoadoa au mabakamabaka, au kondoo yeyote asiye mweusi akionekana katika kundi langu, huyo atakuwa ameibiwa.” 34Labani akasema, “Vema! Na iwe kama ulivyosema.” 35Lakini siku hiyohiyo Labani akaenda akawatenga mabeberu wote wenye milia na madoadoa, mbuzi wote majike waliokuwa na madoadoa na mabakamabaka, kila mnyama aliyekuwa na weupe mwilini mwake, na kila kondoo mweusi, akawaweka chini ya ulinzi wa wanawe. 36Labani akajitenga na Yakobo umbali wa mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akabaki akichunga wanyama wa Labani waliosalia.
37Basi, Yakobo akatwaa fito mbichi za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. 38Akazisimamisha fito hizo alizozibambua mbele ya wanyama katika mabirika ya kunyweshea maji, mahali ambapo wanyama walikuja kunywa maji. Na kwa kuwa wanyama walichukua mimba walipokuja kunywa maji, 39wakapata mimba mbele ya hizo fito; wakazaa wanyama wenye milia, mabakamabaka na madoadoa. 40Yakobo akawatenga hao wanakondoo, kisha akawaelekeza kwenye wanyama wenye milia na weusi katika kundi la Labani. Kwa njia hii, Yakobo akajipatia kundi lake mwenyewe, wala hakulichanganya na lile la Labani. 41Ikawa kila yalipofika majira ya wanyama wenye afya kuchukua mimba, Yakobo aliziweka zile fito mbele yao katika mabirika ya kunyweshea maji, ili wachukue mimba penye fito hizo. 42Lakini hakuziweka fito hizo mbele ya wanyama dhaifu walipochukua mimba. Punde si punde, wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye afya wakawa wa Yakobo. 43Basi, Yakobo akatajirika sana, akawa na makundi makubwa ya wanyama, watumishi wa kike na wa kiume, ngamia na punda.
Mwanzo30;1-43

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.