Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Sunday 23 August 2015

Muendelee vyema na Jumapili hii;Burudani-Kinondoni Revival Choir Twalilia Tanzania,Solomon Mukubwa Mfalme Wa Amani na nyingine.....

Nimatumaini yangu wote mpo salama wasalimini na Mungu yu pamoja nanyi
Muwe na wakati mwema......
1Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. 2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. 3Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.4Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.”

Neno La Leo;Yohana 14:1-31

Yesu njia ya kwenda kwa Baba

5Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?” 6Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. 7Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.”
8Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.” 9Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’ 10Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. 11Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. 12Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba. 13Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. 14Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.

Roho Mtakatifu
15“Mkinipenda mtazishika amri zangu. 16Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. 17Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
18“Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu.19Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. 20Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu. 21Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
22Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” 23Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. 24Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
25“Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, 26lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
27“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. 28Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. 29Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. 30Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; 31lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!
Bible Society of Tanzania










"Swahili Na Swahili" Mungu ibariki Tanzania/Watanzania,Africa. 

MISS TANZANIA USA: MAJAJI WAMPOKONYA USHINDI DOREEN PANGA NA KUMVIKA TAJI AEESHA KAMARA NJE YA UKUMBI


Aeesha Kamara sasa ndiye mshindi wa Miss Tanzania USA pageant
  Miss Africa 2014-15 akipata picha ya pamoja na Doreen Panga baada
ya kuvikwa taji la Miss Tanzania USA 
Miss Africa 2014-15 akipata picha ya
pamoja na Aeesha Kamara baada kuvikwa taji na maamuzi ya majaji ambao
hawakukubaliana na mshindi aliyetangazwa kwanza.

Doreen Panga kutoka New York usiku wa Aug 22, 2015, alivuliwa taji la Miss
Tanzania USA na majaji wa shindano hilo nje ya ukumbi taji alilolivaa kwa
dakika 45 na kumvika Aeesha Kamara wa Maryland kwa madai kwamba Doreen
Panga hakua chaguo lao.

Majaji hao Peter Walden, Elaine Roecklein, Tee Thompson, Bertini Huemegni,
Tina Semiti Magembe, Mayor Mlima, Uche Ibezzue wakiongozwa na Michael Lewis
McBride kwa pamoja walikataa kukubaliana na mshindi aliyetangazwa na
kufanya kikao nje ya ukumbi wakati watu wakiondoka ondoka nao
wakisikitishwa na maamuzi ya kutangazwa mshindi huku na kama majaji
wangekaa kimya basi masahabiki wa shindano hilo wangepelekea lawama kwa
majaji.Jaji Dr. Secelela Malecela japo kwamba alipingana na Doreen Panga
kutangazwa mshindi lakini hakukubaliana na majaji wenzake Doreen avuliwe
taji na apewe Aeesha Kamara aliyekua chagua la majaji wengine, yeye
alipendekeza kwa kua kosa lishafanyika waachane nalo wahakikishe mwakani
halitokei tena. Wazo lake lilipingwa na majaji wenzake pale pale.

Shindano hilo lilianza vizuri kwa nyimbo za Taifa za Marekani na Tanzania
zilizoongozwa na watoto Brian akiwa kwenye kinanda na dada yake Briana
akiwa kwenye kipza sauti,

Baadae walitambulishwa ma miss wa
kesho watoto wa DMV wenye umri wa miaka 9 na 12 na baada ya hapo waliingia
malikia wenyewe huku wakisindikizwa na wimbo wa Diamond wa mdogo mdogo na
baadae kujitambulisha kwa majaji.

Washiriki wa miss Tanzania USA
walikua Rechel Mujaya kutoka Atlanta, Joyce Mkapa toka New York, Doreen
Panga toka New York, Aeesha Kamara toka Maryland, Aziza Gama toka Maryland
na Brenda Panga toka New York. Washiriki walianza shindano kwa kujielezea
wakifuatia na shindano la vipaji na baadae kujibu maswali ya majaji.

Pia katika shindano hilo kulikua na burudani mbalimbali akiwemo Mr Tz
ambaye aliitambulisha singo ya wimbo wake mpya uliotoka mwei uliopita,
Wasanii wengine walikua kutoka Ivory Coast na Jamaica.

Baada ya hapo ndipo kulitangazwa mshindi kuwa ni Doreen Panga ushindi ambao
waliowengi hawakukubaliana nao wakiwemo majaji na mkurugenzi na mwanzilishi
wa Miss Africa USA ambao walisikika wakinong'ona huku wakiulizana imekuaje
bila kupata majibu.

Wakati majaji wakiwa nje ya ukumbi wakitafakali imekuaje tumeacha shughuli
zetu tumekuja hapa tunatoa maamuzi sasahihi halafu mtu anatuzarau maamuzi
yetu. Mashabiki walianza kuondoka baada ya shindano hilo kufikia ukingoni
na wengine wakimtupia lawama wandaaji kwa kuvurunda shindano.

Majaji walipokua wakijadiliana wafanye nini walikuja na kuazimia kwa kauli
moja  lazima wampe ukweli mwandaaji kwamba hawakufurahika na
kilichotokea ndani ya ukumbi. Mwandaaji wa Miss Tanzania USA aliitwa ndipo
majaji wakatoa dukuduku lao na mwandaaji akajitetea kwamba mshindi amesema
hataweza kushiriki mashindano hayo na ameamua kumpa taji mshindi wa pili
ambaye alikua Aziza Gama, baada ya kusikia hayo majaji walimwita Doreen
Panga na kumuuliza sababu yake ya kutaka kumvisha taji mshindi wa pili ni
nini yeye akawajibu ni kutokana na kazi zangu ninazofanya hospitali
sitaweza kupata muda wa ushiriki kwa hiyo badala yake nitampa taji mshindi
wa pili.

Majaji walishindwa kuafikiana na Doreen na kuamua kupiga kura upya ndipo
wote kwa pamoja kasolo Dr Secelea Malexela walimchagua Aeesha Kamara kwamba
ndiye aliyestahiki kuvigwa taji na ndio aliyekua chaguo lao.

Doreen Panga akavuliwa taji na kuvikwa Aeesha Kamara huku Doreen akionesha
kutokubaliana na majaji lakini wao ndio waamuzi wa mwisho na kitendo
walichokifanya ni kulinda heshima yao.

Sasa Miss Tanzania USA ni Aeesha Kamara.






Saturday 22 August 2015

Mshumaa wa wiki.....Barry White


 Mshumaa wa wiki ni kipengele kinachozungumzia kuhusu msanii ama kundi la muziki wa zamani katika kipindi cha Mishumaa ya Kale

Kipindi hiki hukujia kila Ijumaa kuanzia saa 11 jioni mpaka 1 usiku kwa saa za Marekani ya Mashariki

Kinatayarishwa na kurushwa na Vijimambo Radio na Kwanza Production, kwa ushirikiano na NesiWangu Media

Tuesday 18 August 2015

Kipindi cha Jukwaa Langu Agosti 17 2015


Kipindi hiki ambacho kinakujia kila JUMATATU, kinajadili mambo mbalimbali na zaidi kuhusu UCHAGUZI MKUU WA TANZANIA 2015

Katika kipindi hiki utasikia mjadala wetu na wageni Jeff Msangi toka Toronto Canada na Darmatus Nambai aliyehudhuria studio kuhusu DEMOKRASIA na MABADILIKO kuelekea uchaguzi nchini Tanzania

KARIBU

Tuesday 11 August 2015

Kipindi cha JUKWAA LANGU Jumatatu wiki hii (Aug 10, 2015)


Katika kipindi cha JUKWAA LANGU wiki hii, tulijadili kuhusu kung'atuka uongozi kwa Prof Ibrahimu Lipumba na pia kukua kwa ufuasi kwa mgombea uRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Edward Lowassa.

Pia, hotuba ya Zitto Kabwe huko Iringa, na mengine mengi

Ungana na Dj Luke Joe (wa hapa), Rose Chitallah, Shamis Abdul (wa hapa) na Mubelwa Bandio (wa hapa) toka Kilimanjaro Studio, Beltsville Maryland na Jeff Msangi (msome hapa) kutoka Toronto Canada kujadili haya.

Pia, kulikuwa na simu za wasikilizaji kadhaa

KARIBU

Monday 10 August 2015

MAISHA ya sasa. Ni kukimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY


Na Mubelwa T Bandio

MAISHA. Nimejifunza kuwa hayako sawa. Na naamini huo ndio usawa wake, kwani humu tuishimo hakuko sawa.

Hivyo, haitakuwa sawa kwa maisha kuwa sawa katika "uwanja" usio sawa kwa waishimo.

Na...

Najua nililoanza nalo na nitakaloendeleza halitaeleweka sawa, na huo ni udhihirisho wa usawa wetu, ambao nao hauko sawa.

Leo, Agosti 10,  ninapoadhimisha mwaka mwingine katika maisha yangu, naitumia siku hii KUAKISI maisha yangu kuliko kusherehekea.

UKWELI ni huu...

Unasoma hapa kwa kuwa "umekua" na kufikia umri wa kusoma na kuelewa. Huu ni umri wa kusherehekea ama kuadhimisha siku kadhaa za kuzaliwa kwako.

Na, kama unasoma hapa, jambo moja ninaloweza kukuhakikishia ni kuwa UTAKUFA.

Kwa hiyo, kama wanadamu, haya mawili yanakuwa ya lazima. Ukizaliwa, utakufa. Tofauti ya maisha yetu ipo katikati ya haya mawili.

Kama nilivyowahi kuandika, kuwa UTAKUMBUKWA KWA DESHI YA MAISHA YAKO (rejea hapa)

Maishani, nimehudhuria BIRTHDAY(s) na MISIBA mingi tu, na kote nimejifunza mengi kuhusu maisha yetu ya sasa, tuyatakayo na namna tunavyojitahidi kuifikia TAMATI yetu.

Labda funzo kuu nililowahi kushiriki nanyi ni lile nililoliandika HAPA Agosti 22, 2011 baada ya kuhudhuria msiba wa Dada yetu hapa Washington DC.

Maisha yetu ya sasa yanaonekana kuwa ya mchakamchaka, twayakimbiza matumaini na (katika hali ya kushangaza) hata siku zaonekana kuwa fupi kuliko awali.

Kabla hujajipanga, ni kesho, ni juma lijalo, ni mwezi ujao na mwaka bila kukamilisha mengi uliyoamini ungependa kuyakamilisha katika muda uliojipangia.

Ninapoangalia miaka hii niliyoishi, naiona kuwa mingi sana. Si kwa kuwa nimeishi mingi kuzidi wote, bali kwa kuzingatia ni mara ngapi nimekuwa nikiamini nimefika mwisho wa uhai.

Nakumbuka kusoma makala ya Kaka Eric Shigongo, iliyosema kuuona mwaka mpya ni nafasi ya ziada. Na naamini katika hilo.

Mara kadhaa (na ni zaidi ya moja) nimekuwa kwenye nafasi ya kuona kama kesho ilikuwa mbali na isiyofikika kwangu nikiwa hai. Siku ambayo hunijia akilini zaidi juu ya hilo, ni HII

Lakini leo wasoma niandikalo.

NI NAFASI YA ZIADA katika kuikimbiza "siku ya mwisho"

Nikirejea kwenye kichwa cha bandiko hili,fikra kwamba maisha yetu ya sasa ni kama kuikimbiza kesho kuliko kuifikiria leo na hata jana, kunatufanya tuonekane kuyawaza yajayo kuliko tulikotoka.

Ni hili linalonifanya niamini kuwa, maisha yetu ya sasa yamewekeza katika yajayo. Na kama nilivyoeleza kabla, jambo pekee ambalo sote tuna hakika nalo, ni kifo.

Na ndio maana nikasema, MAISHA ya sasa. Ni kukimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY

Anyway!

Nisijesahau kujitakia EARTHday njema.

Najua fika kuwa hongera na shukrani za maisha yangu nazipokea kwa sababu ni Mungu aliyeniweka hai mpaka sasa.

Na ndiye aliyenipa WAZAZI wangu ambao sina ninanloweza kueleza kuhusu nafasi yao maishani ikalingana na walilotenda.

Labda jambo moja tu, kwamba walinibariki na NDUGU ambao uwepo wao umekuwa kama egemeo la kukua kwangu. Hawa ndugu wameniwezesha kuambatana na JAMAA ambao kwa muongozo wa ndugu, wameniwezesha kuwa nilivyo. Si unakumbuka kuwa Twachagua maongezi, maongezi yachagua mawazo na mawazo yatuchagulia jamii? (Isome hapa)

Nina maRAFIKI ambao wananisaidia katika kukua kwangu. Hawa nawajumusha na wale wanajiona kama maadui kwangu, ambao mara nyingi wamenifanya kujitahidi kukamilisha mambo ili wasipate la kusema.

Hahahahahaaaaaaaaaaaaaaaa

Kipekee, namshukuru mke wangu mpenzi Esther na wanangu Paulina na Annalisa kwa kuwa wavumilivu kwenye harakati zangu (nyingine hazielewekagi yaani)

Hahahaaaaaaaaaaaaaa

Ni siku nyingine ya kukumbuka kuzaliwa kwangu. Nalikaribia hitimisho la maisha, na nikilijongelea, najitahidi kukamilisha dhumuni yangu ya kuwa humu duniani.



Mungu akubariki na kuonyeshe namna muafaka ya kutenda kila lililo jema, kadhi uikaribiavyo.