Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 1 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 7...

 



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



“Ole wao wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo wa malisho yangu!” Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nasema hivi kuhusu wachungaji wanaowachunga watu wangu: Nyinyi mmewatawanya kondoo wangu na kuwafukuza, wala hamkuwatunza. Basi, nami pia nitawaadhibu kwa ajili ya matendo yenu maovu.

Yeremia 23:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kisha, nitawakusanya kondoo wangu waliobaki kutoka nchi zote nilikowatawanya, na kuwarudisha malishoni mwao. Nao watazaa na kuongezeka. Nitawapa wachungaji watakaowatunza vema, nao hawatakuwa na woga tena wala kufadhaika, na hakuna hata mmoja wao atakayepotea, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Yeremia 23:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



“Tazama, siku zaja nitakapomchipushia Daudi chipukizi adili. Huyo atatawala kama mfalme, na atatenda kwa busara, haki na uadilifu katika nchi. Katika siku za utawala wake, Yuda ataokolewa na Israeli ataishi kwa usalama. Naye ataitwa, ‘Mwenyezi-Mungu ni uadilifu wetu.’

Yeremia 23:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Mapokeo ya mababu

(Mat 15:1-9)
1Baadhi ya Mafarisayo na waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. 2Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. 3Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: Hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. 4Tena, hawali kitu chochote kutoka sokoni, mpaka wamekiosha kwanza.7:4 mpaka wamekiosha kwanza: Au Mpaka wametawadha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizozipokea toka zamani kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
5Basi, Mafarisayo na waalimu wa sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati mapokeo tuliyoyapokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?” 6Yesu akawajibu, “Wanafiki nyinyi! Nabii Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu alipoandika:
‘Mungu asema: Watu hawa, huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao, wako mbali nami.
7Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’
8Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.”
9Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu! 10Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’. 11Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu), 12basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’. 13Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.”
Mambo yanayomtia mtu unajisi
(Mat 15:10-20)
14Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe. 15Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.” 16Mwenye masikio na asikie!
17Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. 18Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi, 19kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.)
20Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi. 21Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, 22uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. 23Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”
Imani ya mama mmoja
(Mat 15:21-28)
24Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. 25Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. 26Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. 27Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” 28Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.” 29Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!” 30Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
Yesu anamponya bubu kiziwi
31Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. 32Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. 33Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. 34Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.” 35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. 36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. 37Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: Amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!”


Marko7;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Wednesday, 30 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 6...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo.

Wafilipi 3:18

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia.

Wafilipi 3:19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.

Wafilipi 3:20-21

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Yesu anakataliwa huko Nazareti

(Mat 13:53-58; Luka 4:16-30)
1Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akifuatwa na wanafunzi wake. 2Siku ya Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sunagogi. Wengi waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? 3Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao kina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?” Basi, wakawa na mashaka naye.
4Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake, kwa jamaa zake na nyumbani mwake.”
5Hakuweza kutenda miujiza hapo, ila aliwawekea mikono wagonjwa wachache, akawaponya. 6Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao.
Yesu anawatuma wanafunzi kumi na wawili
(Mat 10:5-15; Luka 9:1-6)
Kisha Yesu alivitembelea vijiji vya pale karibu akiwafundisha watu. 7Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu; 8akawaamuru: “Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni. 9Vaeni viatu lakini msichukue koti la ziada.” 10Tena aliwaambia, “Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 11Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakunguta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” 12Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu. 13Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya.
Kifo cha Yohane Mbatizaji
(Mat 14:1-12; Luka 9:7-9)
14Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, “Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu, ndiyo maana nguvu hizi zinafanya kazi ndani yake.” 15Wengine walisema, “Mtu huyu ni Elia.” Wengine walisema, “Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale.”
16Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.”
17Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake. 18Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.”
19Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze. 20Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana.
21Ndipo ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya. 22Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, “Niombe chochote utakacho, nami nitakupa.” 23Tena akamwapia, “Chochote utakachoniomba, nitakupa; hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.”
24Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, “Niombe nini?” Naye akamjibu, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.” 25Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, “Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.”
26Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia. 27Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani, 28akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake. 29Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Yesu anawapa chakula watu elfu tano
(Mat 14:13-21; Luka 9:10-17; Yoh 6:1-14)
30Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha. 31Yesu akawaambia, “Twendeni peke yetu mpaka mahali pa faragha mkapumzike kidogo.” Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno waliokuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. 32Basi, wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha.
33Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika. 34Aliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi. 35Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa. 36Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula.” 37Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Nao wakamwuliza, “Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari 200, na kuwapa chakula?” 38Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni kutazama.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”
39Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi. 40Nao wakaketi makundimakundi ya watu 100 na ya watu hamsini. 41Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume 5,000.
Yesu anatembea juu ya maji
(Mat 14:22-33; Yoh 6:15-21)
45Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ngambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu. 46Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali. 47Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji, akataka kuwapita. 49Lakini walipomwona akitembea juu ya maji, walidhani ni mzimu, wakapiga yowe. 50Maana wote walipomwona waliogopa sana. Mara Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” 51Kisha akapanda mashuani walimokuwa, na upepo ukatulia. Nao wakashangaa sana, 52kwa sababu hawakuwa bado wameelewa maana ya ile mikate. Akili zao zilikuwa bado zimepumbazika.
Yesu anawaponya wagonjwa kule Genesareti
(Mat 14:34-36)
53Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54Walipotoka mashuani watu walimtambua Yesu mara. 55Basi, kwa haraka wakazunguka katika nchi ile yote, wakaanza kuwachukua wagonjwa wamelala juu ya mikeka yao, wakawapeleka kila mahali waliposikia Yesu yupo. 56Kila mahali Yesu alipokwenda, vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi waguse walau pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.


Marko6;1-56

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe