Collabo ya kihistoria kati ya Mfalme Mzee Yusuf na Malkia Khadija Kopa katika wimbo na video ya pamoja yenye malengo ya kuhamasisha jamii kupinga ukatili dhidi ya wanawake.
Video hii iliyorekodiwa mkoani Morogoro inamuonyesha Mzee Yusuf na Khadija Kopa kama mume na mke ambao wamebahatika kupata watoto wawili 'Kulwa' na 'Doto' ambao ni mapacha. Mzee Yusuf ni dereva wa daladala wakati Khadija ni mama wa nyumbani lakini pia mjasiriamali.
Pamoja na kwamba watoto wao ni mapacha ambao wanafanana na kulingana kwa karibu kila kitu ikiwemo umri lakini tofauti ya jinsi yao inaonekana kumpa haki zaidi mtoto wa kiume ambaye anaonekana kuelekea shuleni wakati pacha mwenzie anaonekana kuhangaika na shughuli za nyumbani ikiwemo kutafuta maji, kufanya usafi n.k.
Kwa upande mwingine, Mzee anaonekana kutokuijali familia yake haachi pesa ya matumizi nyumbani na hata anapoulizwa anakuwa mkali sana wakati huo huo anaonekana kuchezea mabinti wengine akiwa kazini.
Stori inabadilika kabisa pale mzee anapokutana na Mwanamabadiliko ambaye anafanikiwa kumshawishi kubadili tabia hizo kwa ajili ya manufaa ya familia yake. Kuanzia hapo Mzee anaonekana akinunua nguo za shule za mwanae wa kike na kubandika ujumbe wa mabadiliko katika gari na nyumba yake.
Baada ya hapo maisha yanaonekana kuwa ya raha mustarehe.
"Tukae na tu-starehe tule raha na maisha." Kinasema kibwagizo katika wimbo huo.