Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 3 August 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Ufunuo....15


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..

Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri. Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.

1 Wakorintho 7:6-7

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Basi, wale ambao hawajaoa na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo. Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia, basi na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa.

1 Wakorintho 7:8-9


Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: Mke asiachane na mumewe; lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe.

1 Wakorintho 7:10-11

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda. Misiba mikuu ya mwisho

1Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.
2Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. 3Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo:
“Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
matendo yako ni makuu na ya ajabu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,
njia zako ni za haki na za kweli!
4 Taz Zab 86:9 Bwana, ni nani asiyekucha wewe?
Nani asiyelitukuza jina lako?
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu
maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
5Baada ya hayo nikaona hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ya kuwapo kwa Mungu. 6Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa na kanda za dhahabu vifuani mwao. 7Kisha, mmojawapo wa wale viumbe wanne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. 8Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia hekaluni mpaka mwisho wa mabaa saba ya wale malaika saba.
Ufunuo15;1-8
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: