Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 23 July 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Ufunuo....8


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...

Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.

Waebrania 12:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu.

Waebrania 12:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.”

Waebrania 12:5-6

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 1Kisha, malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. 2Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la kuzimu, kukatoka moshi wa tanuri kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa kuzimu. 3Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani, wakapewa nguvu kama ya nge. 4Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. 5Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na nge. 6Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

7Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. 8Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. 9Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. 10Walikuwa na mikia na miiba kama nge, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. 11Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani Mwangamizi.
12Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.
13Kisha, malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. 14Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Eufrate!” 15Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanadamu. 16Nilisikia idadi ya majeshi wapandafarasi ilikuwa 200,000,000. 17Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapandafarasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na manjano kama madini ya kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na madini ya kiberiti vilikuwa vinatoka vinywani mwao. 18Theluthi moja ya wanadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu, yaani moto, moshi na madini ya kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; 19maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilifanana na nyoka na ilikuwa na vichwa, nao waliitumia hiyo kuwadhuru watu.
20 Taz Zab 115:4-7; 135:15-17 Wanadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakutubu na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; wala kuacha kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. 21Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.
Ufunuo8;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: