Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 27 August 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 10....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.”

1 Wafalme 3:5

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi.

1 Wafalme 3:6

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu.

1 Wafalme 3:7

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Mitume kumi na wawili

(Marko 3:13-19; Luka 6:12-16)
1Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. 2Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: Wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; 3Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.
Yesu anawatuma mitume kumi na wawili
(Marko 6:7-13; Luka 9:1-6)
5Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. 6Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. 7Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ 8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. 9Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. 10Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake.
11“Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 12Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. 13Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi. 14Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. 15Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.
Udhalimu
(Marko 13:9-13; Luka 21:12-17)
16“Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. 17Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. 18Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa. 19Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. 20Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.
21“Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 22Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa.
23“Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.
24“Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake. 25Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?
Anayestahili Kuogopwa
(Luka 12:2-7)
26“Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. 27Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinongonezwa, litangazeni hadharani. 28Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. 29Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. 30Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi.
Kumkiri na kumkana Kristo
(Luka 12:51-53; 14:26-27)
32“Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 33Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
Mafarakano
(Luka 12:8-9)
34“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. 36Taz Mika 7:6 Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.
37“Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. 39Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.
Tuzo
(Marko 9:41)
40“Anayewapokea nyinyi, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. 41Anayempokea nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayempokea mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. 42Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hakika hatakosa kamwe kupata tuzo lake.”

Mathayo10;1-42

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: