Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 28 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 10...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote.

Zaburi 103:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake.

Zaburi 103:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao.

Zaburi 103:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.




Yesu anawatuma wafuasi sabini na wawili
1Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda. 2Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. 3Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma nyinyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwamwitu. 4Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani. 5Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: ‘Amani iwe katika nyumba hii!’ 6Kama akiwako mpenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni. 7Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile. 8Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni. 9Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.’ 10Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni: 11‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunayapangusa dhidi yenu. Lakini, jueni kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile ya watu wa Sodoma.
Ole kwa miji isiyotubu
(Mat 11:20-24)
13“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kukaa katika majivu kutubu. 14Hata hivyo, siku ya hukumu nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. 15Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu.”
16Halafu akasema, “Anayewasikiliza nyinyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea nyinyi, anakataa kunipokea mimi. Na yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma.”
Wale sabini na wawili wanarudi
17Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako.” 18Yeye akawaambia, “Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni. 19Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na nge, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru. 20Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Furaha ya Yesu
(Mat 11:25-27; 13:16-17)
21Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.”
22Kisha akasema, “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumfunulia.”
23Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, “Heri wanaoona yale mnayoyaona nyinyi! 24Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona nyinyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie.”
Mfano wa Msamaria mwema
25Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?” 26Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?” 27Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” 28Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.”
29Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” 30Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. 31Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. 32Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando. 33Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. 34Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza. 35Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’” 36Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?” 37Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”
Yesu nyumbani kwa Martha na Maria

38Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake. 39Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. 40Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.” 41Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi. 42Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyanganya.” 



Luka10;1-42

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Tuesday 27 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 9...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Watakaposikika wapandafarasi na wapiga mishale, kila mmoja atatimua mbio. Baadhi yao watakimbilia msituni, wengine watapanda majabali. Kila mji utaachwa tupu; hakuna mtu atakayekaa ndani.

Yeremia 4:29

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Nawe Yerusalemu uliyeachwa tupu, unavalia nini mavazi mekundu? Ya nini kujipamba kwa dhahabu, na kujipaka wanja machoni? Unajirembesha bure! Wapenzi wako wanakudharau sana; wanachotafuta ni kukuua.

Yeremia 4:30



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Nilisikia sauti kama ya mwanamke anayejifungua, yowe kama anayejifungua mtoto wa kwanza. Ilikuwa sauti ya Yerusalemu akitweta, na kuinyosha mikono yake akisema, ‘Ole wangu! Wanakuja kuniua!’”

Yeremia 4:31

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Yesu anawatuma wale kumi na wawili

(Mat 10:5-15; Marko 6:7-13)
1Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuponya pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa. 2Halafu akawatuma waende kuhubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3Akawaambia, “Mnaposafiri msichukue chochote: Msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada. 4Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho. 5Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” 6Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
Wasiwasi wa Herode
(Mat 14:1-12; Marko 6:14-29)
7Sasa, mtawala Herode alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: “Yohane amefufuka kutoka kwa wafu!” 8Wengine walisema kwamba Elia ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani. 9Lakini Herode akasema, “Huyo Yohane nilimkata kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?” Akawa na hamu ya kumwona.
Yesu anawapa chakula watu elfu tano
(Mat 14:13-21; Marko 6:30-44; Yoh 6:1-14)
10Wale mitume waliporudi, walimweleza Yesu yote waliyoyafanya. Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida. 11Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa.
12Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, “Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani.” 13Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Wakamjibu, “Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!” 14(Walikuwapo pale wanaume wapatao 5,000.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini.” 15Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote. 16Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. 17Watu wote wakala, wakashiba. Wakakusanya mabaki ya chakula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
Petro anamkiri Yesu kuwa Kristo
(Mat 16:13-19; Marko 8:27-29)
18Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?” 19Nao wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane Mbatizaji; wengine, Elia; wengine, mmojawapo wa manabii wa kale ambaye amefufuka.” 20Hapo akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.”
Yesu anazungumzia kifo chake
(Mat 16:20-28; Marko 8:30–9:1)
21Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo. 22Akaendelea kusema kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria na kuuawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa. 23Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa. 25Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe? 26Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. 27Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”
Yesu anageuka sura
(Mat 17:1-8; Marko 9:2-8)
28Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali. 29Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kungaa sana. 30Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao walikuwa Mose na Elia, 31ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kutoka kwake ambako angekamilisha huko Yerusalemu. 32Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Basi, tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Kwa kweli hakujua anasema nini.
34Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana. 35Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: “Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni.” 36Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona.
Yesu anamponya mtoto mwenye pepo
(Mat 17:14-18; Marko 9:14-27)
37Kesho yake walipokuwa wakishuka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu. 38Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaza sauti, akasema, “Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu-mwanangu wa pekee! 39Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi. 40Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.” 41Yesu akasema, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?” Kisha akamwambia huyo mtu, “Mlete mtoto wako hapa.” 42Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake. 43Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu.
Yesu anaongea tena juu ya kifo chake
(Mat 17:22-23; Marko 9:30-32)
Wale watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, 44“Tegeni masikio, muyasikie mambo haya: Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.” 45Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo huo.
Ni nani aliye mkuu?
(Mat 18:1-5; Marko 9:33-37)
46Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi. 47Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye, 48akawaambia, “Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkuu kuliko wote.”
Asiyepingana nanyi yuko upande wenu
(Marko 9:38-40)
49Yohane alidakia na kusema, “Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.” 50Lakini Yesu akamwambia, “Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu.”
Wasamaria wanakataa kumkaribisha Yesu
51Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu. 52Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali. 53Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu alikuwa anaelekea Yerusalemu. 54Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona hayo, wakasema, “Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni uwateketeze?” 55Lakini yeye akawageukia, akawakemea.9.55 Baadhi ya hati huongeza: Akasema, “Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo; kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa.” 56Wakatoka, wakaenda kijiji kingine.
Wanaostahili kuwa wafuasi
(Mat 8:19-22)
57Walipokuwa wakisafiri njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.” 58Yesu akasema, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.”
59Kisha akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.” Lakini huyo akasema, “Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba yangu.” 60Yesu akamwambia, “Waache wafu wazike wafu wao; bali wewe nenda ukatangaze ufalme wa Mungu.”
61Na mtu mwingine akamwambia, “Nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikawaage wale walio nyumbani kwangu.” 62Yesu akamwambia, “Yeyote anayeshika jembe tayari kulima na huku anaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”

Luka9;1-62

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe