Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 15 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Mathayo,Leo Tunaanza Kitabu cha Luka ....1



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Mathayo
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Luka"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Waligawanywa kwa kura kwani kulikuwa na wakuu wa mahali patakatifu na viongozi wa kidini miongoni mwa koo zote mbili, yaani ukoo wa Eleazari na ukoo wa Ithamari.

1 Mambo ya Nyakati 24:5

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Naye Shemaya mwana wa Nathaneli, mwandishi, aliyekuwa Mlawi, aliwaandika mbele ya mfalme Daudi, maofisa wake, kuhani Sadoki, Ahimeleki mwana wa Abiathari na viongozi wa jamaa za makuhani na za Walawi. Ukoo wa Eleazari ulipata kura mbili, na ukoo wa Ithamari kura moja.

1 Mambo ya Nyakati 24:6


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Kura ya 1 ilimwangukia Yoaribu; ya 2 Yedaya; ya 3 Harimu; ya 4 Seorimu; ya 5 Malkia; ya 6 Miyamini; ya 7 Hakosi; ya 8 Abiya; ya 9 Yeshua; ya 10 Shekania; ya 11 Eliashibu; ya 12 Yakimu; ya 13 Hupa; ya 14 Yeshebeabu; ya 15 Bilga; ya 16 Imeri; ya 17 Heziri; ya 18 Hapisesi; ya 19 Pethahia; ya 20 Yehezkeli; ya 21 Yakini; ya 22 Gamuli; ya 23 Delaya; na ya 24 Maazia.

1 Mambo ya Nyakati 24:7-18

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 1Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. 2Waliyaandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona mambo hayo kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. 3Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, 4ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.

Ahadi ya kuzaliwa kwa Yohane
5Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
8Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.”
18Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.” 19Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema. 20Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.”
21Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni. 22Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
23Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25“Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.”
Ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu
26Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!”
29Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? 30Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. 32Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” 38Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.
Maria anamtembelea Elisabeti
39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea. 40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti. 41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu, 42akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. 43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.”
Utenzi wa Maria
46Naye Maria akasema,
“Moyo wangu wamtukuza Bwana,
47roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu.
Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
49Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu,
jina lake ni takatifu.
50Huruma yake kwa watu wanaomcha
hudumu kizazi hata kizazi.
51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:
Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi,
akawakweza wanyenyekevu.
53Wenye njaa amewashibisha mema,
matajiri amewaondoa mikono mitupu.
54Amemsaidia Israeli mtumishi wake,
akikumbuka huruma yake,
55kama alivyowaahidia wazee wetu,
Abrahamu na wazawa wake hata milele.”
56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji
57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. 58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. 60Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” 61Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” 62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. 63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. 64Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. 66Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Utenzi wa Zakaria
67Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu:
68“Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli,
kwani amewajia na kuwakomboa watu wake.
69Ametupatia Mwokozi shujaa,
mzawa wa Daudi mtumishi wake.
70Aliahidi hapo kale
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
71kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu
na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
72Alisema atawahurumia wazee wetu,
na kukumbuka agano lake takatifu.
73Alimwapia Abrahamu babu yetu,
kwamba atatujalia sisi
74tukombolewe mikononi mwa maadui zetu,
tupate kumtumikia bila hofu,
75tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake,
siku zote za maisha yetu.
76Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu,
utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
77kuwatangazia watu kwamba wataokolewa
kwa kuondolewa dhambi zao.
78Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma.
Atatuchomozea mwanga kutoka juu,
79na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo,
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.”
80Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.

Luka1;1-80

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: