Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 19 August 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 4 ....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!


Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.

Yakobo 1:5

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.

Yakobo 1:6

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.
Kujaribiwa kwa Yesu 
(Marko 1:12-13; Luka 4:1-13) 
1Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi. 2Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. 3Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.” 4Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu.’” 5Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, 6Taz Zab 91:11-12 akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: ‘Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe.’” 7Yesu akamwambia, “Imeandikwa pia: ‘Usimjaribu Bwana, Mungu wako.’” 8Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, 9akamwambia, “Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu.” 10Hapo, Yesu akamwambia, “Nenda zako Shetani! Imeandikwa: ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake.’” 11Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia. 

Yesu anaanza kazi Galilaya 
(Marko 1:14-15; Luka 4:14-15) 
12Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya. 13Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zebuluni na Naftali, akakaa huko. 14Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya: 15“Nchi ya Zebuluni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ngambo ya mto Yordani, Galilaya, nchi ya watu wa mataifa! 16Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!” 17Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, “Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekariia!” 

Yesu anawaita wavuvi wanne 
(Marko 1:16-20; Luka 5:1-11) 
18Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwaye Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. 19Basi, akawaambia, “Nifuateni, nami nitawafanya nyinyi wavuvi wa watu.” 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 21Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi, Yesu akawaita, 22nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata. 

Yesu anafundisha watu na kuponya wagonjwa 
(Luka 6:17-19)
 23Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. 24Habari zake zikaenea pande zote za Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: Waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. 25Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ngambo ya mto Yordani, yalimfuata.

Mathayo4;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: