Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 3 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 25....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, upendo, subira na unyenyekevu. Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato,
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Adui kutoka kaskazini
1Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika Yuda, Mwenyezi-Mungu alinimpa mimi Yeremia ujumbe kuhusu watu wa Yuda. Mwaka huo ulikuwa wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. 2Mimi Yeremia niliwaambia ujumbe huo watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: 3“Kwa muda wa miaka ishirini na mitatu sasa, yaani tangu mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, mpaka hivi leo, nimekuwa nikipata neno la Mungu na kuwaambieni kila wakati, lakini nyinyi hamkusikiliza. 4Hamkutaka kusikiliza wala hamkutega sikio msikie, ingawa Mwenyezi-Mungu aliwaleteeni watumishi wake manabii kila wakati, 5wakawaambieni kwamba kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu na matendo yake mabaya, ili mpate kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa nyinyi na wazee wenu tangu zamani, muimiliki milele. 6Mwenyezi-Mungu aliwaonya Mmsifuate miungu mingine wala kuitumikia na kumkasirisha Mungu kwa kuabudu sanamu ambazo mmejitengenezea wenyewe. Kama Mmkimtii Mwenyezi-Mungu basi, yeye hatawaadhibu. 7Lakini Mwenyezi-Mungu asema kuwa nyinyi mlikataa kumsikiliza. Badala yake, mlimkasirisha kwa sanamu mlizojitengenezea wenyewe, na hivyo mkajiletea madhara nyinyi wenyewe.
8“Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: “Kwa kuwa hamkuyatii maneno yangu, 9basi, nitayaita makabila yote ya kaskazini, pamoja na mtumishi wangu Nebukadneza, mfalme wa Babuloni. Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake pamoja na mataifa yote ya jirani. Nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kuwa kitu cha kuchukiza, kuzomewa na kudharauliwa milele. 10Tena, nitakomesha miongoni mwao sauti za furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi. Sauti za kusaga hazitakuwapo, wala mwanga wa taa. 11Nchi hii yote itakuwa magofu matupu na ukiwa, na mataifa ya jirani yatamtumikia mfalme wa Babuloni kwa muda wa miaka sabini. 12Kisha baada ya miaka hiyo sabini kukamilika nitamwadhibu mfalme wa Babuloni pamoja na taifa hilo. Nitaiangamiza nchi hiyo ya Wakaldayo kwa sababu ya uovu wao na kuifanya nchi iwe magofu milele. 13Nitailetea nchi hiyo mambo yote niliyotamka dhidi yake na yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki ambayo Yeremia alitabiri dhidi ya mataifa yote. 14Wababuloni nao itawalazimu kuwa watumwa wa mataifa mengine na wafalme wengine. Nitawaadhibu kadiri ya maovu yao waliyotenda.”
Kikombe cha hukumu
15Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Chukua mkononi mwangu hiki kikombe cha divai ya ghadhabu yangu uyanyweshe mataifa yote ninayokutuma kwao. 16Mataifa hayo yatakunywa na kupepesuka na kurukwa na akili kwa sababu ya mauaji nitakayosababisha kati yao.”
17Basi, nikachukua hicho kikombe mkononi mwa Mwenyezi-Mungu, nikayanywesha mataifa yote ambayo Mwenyezi-Mungu alinituma kwao. 18Kwanza Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na viongozi wake, ili kuifanya iwe jangwa, ukiwa, kitu cha kuzomewa na kulaaniwa, kama ilivyo mpaka leo. Halafu: 19Farao, mfalme wa Misri, maofisa na viongozi wake, pamoja na watu wake wote; 20wageni wote walioishi nchini Misri; wafalme wote wa nchi ya Uzi; wafalme wote wa miji ya Wafilisti, Ashkeloni, Gaza, Ekroni na mabaki ya Ashdodi. 21Watu wote wa Edomu, Moabu na Amoni; 22wafalme wote wa Tiro na Sidoni; wafalme wa nchi za pwani ya bahari ya Mediteranea; 23wakazi wa Dedani, Tema, Buzi na watu wote wanyoao denge; 24wafalme wote wa Arabia; wafalme wote wa makabila yaliyochanganyika jangwani; 25wafalme wote wa Zimri, Elamu na Media; 26wafalme wote wa kaskazini, mbali na karibu, mmoja baada ya mwingine. Falme zote ulimwenguni zitakunywa. Na, baada ya hao wote naye mfalme wa Babuloni atakunywa.
27Mwenyezi-Mungu akaniamuru: “Utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Kunyweni, mlewe na kutapika; angukeni wala msiinuke tena, kwa sababu ya mauaji ninayosababisha miongoni mwenu. 28Kama wakikataa kukipokea kikombe hicho mkononi mwako na kunywa, wewe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nasema kwamba ni lazima wanywe! 29Tazama! Sasa ninaanza kuleta maafa katika mji unaoitwa kwa jina langu; je, mnadhani mnaweza kuepukana na adhabu? Hamtaachwa bila kuadhibiwa, maana ninaleta mauaji dhidi ya wakazi wote wa dunia. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.
30“Basi, wewe Yeremia utatabiri maneno haya yote dhidi yao, na kusema hivi:
Mwenyezi-Mungu atanguruma kutoka juu,
atatoa sauti yake kutoka makao yake matakatifu;
atanguruma kwa nguvu dhidi ya watu wake,
na kupaza sauti kama wenye kusindika zabibu,
dhidi ya wakazi wote wa dunia.
31Vishindo hivyo vitasikika hadi mwisho wa dunia,
maana Mwenyezi-Mungu ana mashtaka dhidi ya mataifa;
anawahukumu wanadamu wote,
na waovu atawaua kwa upanga!
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
32Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema:
“Tazama, maafa yatalikumba taifa moja baada ya lingine,
na tufani itazuka kutoka miisho ya dunia.”
33Siku hiyo, watakaouawa na Mwenyezi-Mungu watatapakaa kutoka upande mmoja wa dunia hadi mwingine. Hawataombolezewa, hawatakusanywa wala kuzikwa; watabaki kuwa mavi juu ya ardhi.
34Ombolezeni enyi wachungaji;
lieni na kugaagaa majivuni enyi wakuu wa kundi;
siku za kuchinjwa kwenu na kutawanywa zimefika;
mtauawa kama kondoo madume waliochaguliwa.25:34 kondoo dume waliochaguliwa: Tafsiri moja ya zamani. Kiebrania vyombo.
35Wachungaji hawatakuwa na pa kukimbilia,
wala wakuu wa kundi hawataweza kutoroka.
36Sikilizeni kilio cha wachungaji
na mayowe ya wakuu wa kundi!
Mwenyezi-Mungu anayaharibu malisho yao,
37na makundi yaliyokuwa matulivu yameharibiwa
kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.
38Mwenyezi-Mungu amewaacha watu wake,
kama vile simba aachavyo pango lake;
nchi yao imekuwa jangwa tupu,
kwa sababu ya vita vya wadhalimu,
na hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.


Yeremia25;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: