Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 20 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 15....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa nanyi.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni mwuaji, mwizi, mhalifu au mwovu. Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi, asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi, mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi, kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?” Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Hukumu kwa watu wa Yuda
1Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Hata kama Mose na Samueli wangesimama mbele yangu na kunisihi, nisingewahurumia watu hawa. Waondoe kabisa mbele yangu. Waache waende zao! 2Na wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ wewe utawajibu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Waliopangiwa kufa kwa maradhi, watakufa kwa maradhi;
waliopangiwa kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga;
waliopangiwa kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa;
na waliopangiwa kuwa mateka, watatekwa mateka.
3Mimi Mwenyezi-Mungu nimeamua kuwaletea aina nne za maangamizi: Vita itakayowaua, mbwa watakaowararua; ndege wa angani watakaowadonoa na wanyama wa porini watakaowatafuna na kuwamaliza. 4Nitawafanya kuwa kitu cha kutisha kwa falme zote za dunia, kwa sababu ya mambo ambayo Manase mwana wa Hezekia, aliyafanya huko Yerusalemu, alipokuwa mfalme wa Yuda.
5“Ni nani atakayewahurumia, enyi watu wa Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza juu yenu?
Nani atasimama kuuliza habari zenu?
6Nyinyi mmenikataa mimi, nasema mimi Mwenyezi-Mungu;
nyinyi mmeniacha mkarudi nyuma.
Hivyo nimenyosha mkono kuwaangamiza,
kwa kuwa nimechoka kuwahurumia.
7Nimewapepeta kwa chombo cha kupuria,
katika kila mji nchini;
nimewaangamiza watu wangu,
kwa kuwaulia mbali watoto wao,
lakini hawakuacha njia zao.
8Wajane wao wamekuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Kina mama wa watoto walio vijana
nimewaletea mwangamizi mchana.
Nimesababisha uchungu na vitisho
viwapate kwa ghafla.
9Mama aliyesifika kuwa na watoto saba;
sasa ghafla hana kitu.
Ametoa pumzi yake ya mwisho,
jua lake limetua kukiwa bado mchana;
ameaibishwa na kufedheheshwa.
Na wale waliobaki hai nitawaacha
wauawe kwa upanga na maadui zao.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yeremia anamlalamikia Mungu
10Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa! Mimi nimekuwa mtu wa ubishi na ugomvi nchini pote! Sijapata kukopesha mtu wala kukopeshwa na mtu, lakini kila mtu ananiapiza. 11Haya basi, ee Mwenyezi-Mungu, acha laana hizo nizipate kama sijakutumikia vema na kama sikukusihi kwa ajili ya maadui zangu wakati walipokuwa katika taabu na shida! 12Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya mali yenu na hazina zenu zichukuliwe nyara tena bila kulipwa fidia yoyote kwa sababu ya dhambi zenu zote mlizotenda kila mahali nchini. 14Nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua kwa sababu hasira yangu imewaka moto ambao hautazimwa milele.”
15Nami nikasema: “Lakini wewe Mwenyezi-Mungu wajua;
unikumbuke na kuja kunisaidia.
Nilipizie kisasi watesi wangu.
Wewe u mvumilivu, usiniache niangamie;
kumbuka kuwa ninatukanwa kwa ajili yako.
16Mara maneno yako yalipofika, niliyameza;
nayo yakanifanya niwe na furaha,
yakawa utamu moyoni mwangu,
maana mimi najulikana kwa jina lako,
ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
17Sikuketi pamoja na wanaostarehe,
wala sikufurahi pamoja nao.
Niliketi peke yangu nimelemewa nguvu yako;
kwa maana ulinijaza hasira yako.
18Kwa nini mateso yangu hayaishi?
Mbona jeraha langu haliponi,
wala halitaki kutibiwa?
Ama kweli umenidanganya,
kama kijito cha maji ya kukaukakauka!”
19Mwenyezi-Mungu akajibu:
“Kama ukinirudia nitakurudishia hali ya kwanza,
nawe utanitumikia tena.
Kama ukisema maneno ya maana na sio ya upuuzi,
basi utakuwa msemaji wangu.
Watu watakuja kujumuika nawe,
wala sio wewe utakayekwenda kwao.
20Mbele ya watu hawa,
nitakufanya ukuta imara wa shaba.
Watapigana nawe,
lakini hawataweza kukushinda,
maana, mimi niko pamoja nawe,
kukuokoa na kukukomboa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21Nitakuokoa mikononi mwa watu waovu,
na kukukomboa makuchani mwa wakatili.”


Yeremia15;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: