Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 3 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 21......





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana....
Tumshukuru Mungu katika yote.....

Asante Mungu wetu  kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Jehovah,
Uhimidiwe Yahweh,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni...



Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.

 Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya
na kesho ni siku nyingine
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza 
kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah ukavitakase na kuvifunika ka Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tunaomba tukawe salama rohoni
Jehovah tunaomba ukatupe macho ya kuona na 
masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe
akili ya kutambua mema na mabaya
Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye chombo chema ee Baba wa Mbinguni nasi tukatumike
kama ianvyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi



Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako watoto wako
wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Yahweh ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu ukawaponye kimwli na kiroho pia
Baba wa mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,amani ikatawale,upendo ukadumu
ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masiki o ya kusiki sauti yako
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu tunaomba ukapokee sala/maombi yetu
Jehovah ukawajibu sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Nawapenda.




Mfalme Manase wa Yuda

(2Nya 33:1-20)

1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala Yuda, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano. 2Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kuiga mienendo miovu ya mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati watu wake, Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. 3Kwa maana alirekebisha mahali pa kuabudia miungu mingine palipoharibiwa na Hezekia baba yake; akajenga madhabahu za kuabudia Baali na kutengeneza sanamu ya Ashera, kama vile alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Isitoshe, Manase aliabudu na kutumikia vitu vyote vya mbinguni. 4Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa katika Yerusalemu.” 5Katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alijenga madhabahu ya kuabudia sayari. 6Pia alimtoa mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa. Alipiga ramli; alibashiri akishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha. 7Nayo sanamu ya Ashera aliyotengeneza akaiweka katika nyumba ambayo Mwenyezi-Mungu aliizungumzia mbele ya Daudi na mwanawe Solomoni: “Katika nyumba hii na mjini Yerusalemu niliouchagua ndiko mahali nitakapoabudiwa milele. 8Na iwapo Waisraeli watajali kutenda yote niliyowaamuru na kufuata Sheria zote mtumishi wangu Mose alizowapa, basi sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.” 9Lakini hawakusikia, naye Manase aliwafanya watende dhambi zaidi kuliko zile zilizofanywa na mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaharibu mbele ya Waisraeli.
10Ndipo Mwenyezi-Mungu alisema kupitia kwa watumishi wake manabii, 11“Kwa sababu mfalme amefanya mambo ya kuchukiza, mambo mabaya zaidi ya yale yaliyotendwa na Waamori waliomtangulia, amewafanya watu wa Yuda pia watende dhambi kwa kutumia sanamu zake; 12basi, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tazama nitaleta juu ya Yerusalemu na Yuda, msiba ambao hata yeyote atakayesikia atashtuka. 13Nitauadhibu Yerusalemu kama vile nilivyofanya Samaria, na mfalme Ahabu na wazawa wake. Nitafuta Yerusalemu kama mtu afutavyo sahani iliyosafishwa na kuiinamisha. 14Nitawaacha hao watu wa urithi wangu watakaosalia na kuwakabidhi kwa adui zao; watakuwa mawindo na mateka kwa adui zao wote. 15Nitawatendea hayo yote kwa sababu wameniasi na kunikasirisha tangu wazee wao walipotoka Misri mpaka leo.”
16Zaidi ya hayo, licha ya dhambi yake alipowakosesha watu wa Yuda wakafanya dhambi kwa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Manase aliwaua watu wengi wasiokuwa na hatia, damu ilijaa toka upande mmoja mpaka upande mwingine wa Yerusalemu.
17Matendo mengine ya Manase na yote aliyotenda, pamoja na dhambi zake zote, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 18Manase alifariki na kuzikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, katika Bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akatawala mahali pake.

Mfalme Amoni wa Yuda

(2Nya 33:21-25)

19Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu. Jina la mama yake ni Meshulemethi, binti Haruzi wa Yothba. 20Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya. 21Alifuata njia yote aliyoiendea baba yake na kutumikia sanamu ambazo baba yake alizitumikia na kuziabudu.
22Alimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hakushika njia ya Mwenyezi-Mungu.
23Baadaye watumishi wa Amoni walikula njama na kumwua katika ikulu yake. 24Lakini watu wa Yuda wakawaua wote waliomuua Amoni. Kisha watu hao wa Yuda wakamtawaza Yosia mwanawe mahali pake.
25Matendo mengine yote ya Amoni yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda. 26Amoni alizikwa kaburini katika bustani ya Uza; na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.


2Wafalme21;1-26


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Wednesday 2 May 2018

Maisha-Lifestyle;[Wanawake na imani]-Leo tunaye da'Rose wa Mbeyela


Hamjambo wapendwa/waungwana?
Mimi nipo vyema Mungu yu mwema....

Pichani; ni da'Rose wa Mbeyela mimi nimezoea kumuita [Dogo]
ni mke wa mtu na ni mama pia....

Kwenye "dawati langu leo" nimeguswa kumuweka na kumtambulisha kwako wewe usiyemfahamu
Na wanaomfahamu haijalishi umemjulia wapi,kwenye mitandao,umekuwa naye,umesoma naye vyovyote..
jee nini kinakufanya umsome/umfuatilie?

1.Kwangu mimi da'Rose ni mwandishi mzuri na mchambuzi mzuri wa anavyoviandika
hasa kwenye mambo ya kiimani...
Akiamua kuandika anaandika [Magazeti]kirefu ...
Ninavutiwa sana na magazeti yake hasa ya kiimani huwa ananibariki sana anavyolichambua Neno hata kama
ni mvivu wa kusoma lakini utatamani ujue mwisho wake ilikuwajee?
Hapo ndipo itabidi umalize kusoma tuu...
 kwa hili nampongeza sana na  namuombea sana. 
Mungu aendelee kumpa kibali cha kuendelea..
Siku hizi amekuwa mvivu,sijui ametingwa,sijui majukumu ,muda hautoshi au laa...
Ushauri wangu dada usijisahaulishe tunaomba urudi kwa Blog au unaweza kurudi kama VLOGGER
Kwanini jamani umepewa bure njoo utoe bure japo muda ni gharama pia....
Blog;http://beyou-rose.blogspot.co.uk/

facebook;https://www.facebook.com/rose.w.mbeyela
Instagram;https://www.instagram.com/rose_wa_mbeyela/

2.kwenye majukumu yake kama mke na mama pia ananivutia yeah anauzungu kidogo na uswahili kidogo
yupo makini  na anavijimisimamo vyake anavyoamini yeye mwenyewe na anaweza kusimama kama mke na kama
mama pia hasa wamama/wake wa ughaibuni nako kuna changamoto zake...
[Hapa ndani kunakitu tumemuiga/jifunza pia,-alisema wao wakienda kwenye sherehe za Wazungu huwa wanaandaa mboga kabisaa nyumbani wakirudi huko wanaangusha Nguna/Ugali hahahahhahahh...!!! hiki kitendo hapa ndani Baba watoto amekizingatia sana tangu amejua hivyo....hahahaha"swahili na waswahili"]

3.Uchapakazi;Nifamnyaji wa kazi na hachagui saana kazi za kibishoo na ni mtu wa kujivunia anachokifanya
Mbunifu[Mtundu]hupenda kujaribu na kujishughulisha..
Anajua kuzitafuta na anajua kuzitumia.....


oohh nami nikianza kuongea sitamaliza leo

kwa leo ngoja niishie hapa...


Nakutakia maisha mema dadake ,yenye baraka,amani,upendo ukadumu kati yetu

furaha pamoja na mume wako na watoto pia...
Mungu akakupe maisha marefu yenye kumpendeza yeye ukatimize ndoto zako na kazi uliyotumwa hapa duniani....
Migimingilove......


Picha na da'Rose[shukrani]

Asanteni kwa kunisoma,tukutane kwenye dawati langu lijalo sijui atakuwa nani labda ni wewe unayesoma hapa...

Mungu akitubariki tutakuwa na mahojiano/maongezi/video[sauti]si kuandika tuu...

Muwe na wakati mwema..
wenu; Da'Rachel siwa..

"Swahili Na Waswahili"Pamoja daima.

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 20......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu
na Nchi,Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,
Isaka na Yakobo..
Jehovah Jireh ..!Jehovah Nissi..!Jehovah Shammah,Jehovah Raah..!Jehovah Rapha..!
Jehovah Shalom..!Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu...



Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni ututakase na kutufunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba
ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni
Jehovah tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Yahweh tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na 
ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Upendo ukadumu kati yetu...
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke 
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti. Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.

Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
Wagonjwa,wenye njaa,walio katika magumu/majaribu mbalimbali,
waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,
waliokatika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,
waliojeruhiwa/umizwa rohoni,waliokwenda kinyume nawe/walipotea
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yao
Jehovah ukabariki mashamba/kazi zao
Mungu wetu ukawasamehe na kuwaokoa
Mungu wetu ukawaweke huru na haki ikatendeke..
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu na ukapokee sala/maombi yetu
Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana Wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
 kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.



Kuugua na kupona kwa mfalme Hezekia

(Isa 38:1-8,21-22; 2Nya 32:24-26)

1Wakati huo Hezekia aliugua sana karibu na kufa. Ndipo nabii Isaya, mwana wa Amozi alipomwendea na kumwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu; ‘Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.’”
2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu akisema, 3“Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.
4Lakini kabla Isaya hajapita ua wa katikati, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia, kusema, 5“Rudi ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wa Mwenyezi-Mungu: Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu yako Daudi, nimesikia ombi lako na nimeona machozi yako. Nitakuponya na baada ya siku tatu utakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 6Nitakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi.”
7Basi Isaya akasema, “Leteni andazi la tini mliweke kwenye jipu lake, ili apate kupona.” 8Hezekia akamwuliza Isaya, “Ni ishara gani ambayo itanionesha kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ataniponya na katika siku ya tatu nitaweza kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?”
9Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele au nyuma?”
10Hezekia akamjibu, “Ni rahisi zaidi kivuli kwenda mbele hatua kumi! Hebu kirudi nyuma hatua kumi.”
11Isaya akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akafanya kivuli kirudi hatua kumi kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi.

Wajumbe kutoka Babuloni

(Isa 39:1-8)

12Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani mfalme wa Babuloni alisikia kuwa Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, akamtumia ujumbe pamoja na zawadi. 13Basi, Hezekia akawakaribisha na kuwaonesha mali yake: Nyumba yake ya hazina, fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani na nyumba ya vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakukuwa chochote katika ikulu yake, au nchi yake ambacho hakuwaonesha. 14Ndipo nabii Isaya alipomwendea mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu, “Wamenijia kutoka nchi ya mbali.” 15Halafu akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”
16Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu: 17Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya baba zako mpaka wakati huu vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. 18Tena baadhi ya watoto wako wa kiume watapelekwa mateka, nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”
19Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu kama ulivyolisema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kwa nini isiwe hivyo, ikiwa kutakuwapo amani na ulinzi katika siku za utawala wangu.”

Mwisho wa enzi ya Hezekia

(2Nya 32:32-33)

20Matendo mengine ya Hezekia, ushujaa wake na maelezo juu ya jinsi alivyojenga bwawa na kuchimba mfereji wa kuleta maji mjini, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. 21Hezekia alifariki, naye Manase mwanawe akatawala mahali pake.




2Wafalme20;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 1 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 19......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye upendo,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote Alfa na Omega....

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Jehovah,
Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,matendo yako ni ya ajabu,
Matendo yako yanatisha,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!


Mji wa Gaza utahamwa, Ashkeloni utakuwa tupu. Wakazi wa Ashdodi watatimuliwa mchana, na wale wa Ekroni watang'olewa. Ole wenu wakazi wa nchi za pwani, watu mnaoishi huko Krete! Mwenyezi-Mungu ametamka dhidi yenu enyi wakazi wa Kanaani, nchi ya Filistia: Mimi nitawaangamiza asibaki hata mkazi mmoja! Nanyi nchi za pwani mtafanywa kuwa malisho; mtakuwa vibanda vya wachungaji na mazizi ya kondoo. Nchi ya pwani itamilikiwa na mabaki ya ukoo wa Yuda. Watachunga mifugo yao huko. Nyumba za mji wa Ashkeloni zitakuwa mahali pao pa kulala. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wao atawakumbuka na kuwarudishia hali yao njema.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbiguni ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa 
Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



“Nimeyasikia masuto ya Moabu na dhihaka za Waamoni; jinsi walivyowasuta watu wangu, na kujigamba kuiteka nchi yao. Kwa hiyo, niishivyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, mimi Mungu wa Israeli, Moabu itakuwa kama Sodoma na Amoni itakuwa kama Gomora. Nchi zake zitakuwa za viwavi na mashimo ya chumvi, zitakuwa ukiwa milele. Watu wangu watakaobaki wataziteka nyara, watu wa taifa langu waliosalia watazimiliki.” Hayo yatakuwa malipo ya kiburi chao, kwa sababu waliwadhihaki na kujigamba dhidi ya watu wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mwenyezi-Mungu atakuwa wa kutisha dhidi yao; miungu yote ya dunia ataikondesha. Mataifa yote duniani yatamsujudia; kila taifa katika mahali pake.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo
vimiliki,Mungu wetu tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni
Yahweh tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia
sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako 
siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Upendo ukadumu kati yetu
Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....


Nanyi watu wa Kushi pia mtauawa kwa upanga wake. Mwenyezi-Mungu atanyosha mkono wake kaskazini, na kuiangamiza nchi ya Ashuru. Ataufanya mji wa Ninewi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa. Makundi ya mifugo yatalala humo, kadhalika kila mnyama wa porini. Tai na yangeyange na korongo wataishi juu ya nguzo zake, bundi watalia kwenye madirisha yake, kunguru watalia kwenye vizingiti, maana nyumba zake za mierezi zitakuwa tupu. Je, huu ndio mji uliojivuna na kuishi kwa usalama, mji uliojisemea, “Ni mimi tu, hakuna mwingine!” Jinsi gani umekuwa mtupu na makao ya wanyama wa mwituni! Kila apitaye karibu atauzomea na kuudharau.

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye na kuwatendea kila mmoja
na mahitaji yake
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape neema ya kujiombea,
kufuata njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Yahweh ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu ukawape macho
ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako
Jehovah ukasikie kulia kwao Yahweh ukawafute machozi yao
Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako
tuliyoyanena na tusiyoyanena Baba wa Mbinguni unayajua
Ee Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Baba wa Mbinguni akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Mfalme aomba shauri kwa Isaya

(Isa 37:1-7)

1Mfalme Hezekia alipopata habari hizo, alirarua mavazi yake, akavaa gunia akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 2Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia. 3Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa. 4Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”
5Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya, 6aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi. 7Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”

Tisho jingine la Waashuru

8Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna. 9Halafu mfalme alipopata habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema, 10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru. 11Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka? 12Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza? 13Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’”
14Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu. 15Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu. 16Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai. 17Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao. 18Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu. 19Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.”

Ujumbe wa Isaya kwa mfalme

(Isa 37:21-38)

20Kisha Isaya, mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ‘Nimesikia ombi lako kwangu kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru:’ 21Hili ndilo neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kumhusu Senakeribu:
Anakudharau, anakubeza binti Siyoni,
anatikisa kichwa chake nyuma yako binti Yerusalemu.
22Je, uliyekuwa unamkashifu na kumdhihaki ni nani?
Nani umemwinulia sauti
na kumkodolea macho kwa kiburi?
Juu ya Mtakatifu wa Israeli!”
23Kwa kuwatuma wajumbe wako umemkashifu Bwana,
wewe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimekwea vilele vya milima
mpaka kilele cha Lebanoni.
Nimekata mierezi yake mirefu,
na misonobari mizurimizuri;
nimeingia mpaka ndani yake
na ndani ya misitu yake mikubwa.
24Nimechimba visima
na kunywa maji mageni
nilikausha mito yote ya Misri
kwa nyayo za miguu yangu.
25‘Je, hujasikia,
kwamba nilipanga jambo hili tangu awali?
Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.’
Nilikuweka uijenge miji yenye ngome
kwa rundo la magofu.
26Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,
wametishika na kufadhaika,
wamekuwa kama mimea ya shambani,
kama majani yasiyo na nguvu.
Kama majani yaotayo juu ya paa;
yakaukavyo kabla ya kukua.
27Najua kuketi kwako,
na kuamka kwako
nako kuingia kwako;
nayo mipango yako dhidi yangu.
28Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu
na nimeusikia ufidhuli wako,
nitatia ndoana yangu puani mwako,
na lijamu yangu kinywani mwako.
Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”
29Kisha Isaya akamwambia mfalme Hezekia, “Na hii ndio itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake. 30Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu. 31Maana kutakuwako watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika; maana Mwenyezi-Mungu amedhamiria kukamilisha hayo.
32“Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Waashuru: ‘Hataingia katika mji huu wala kuupiga mshale wala kuujia kwa ngao wala kuuzingira. 33Atarudi kwa njia ileile aliyoijia na wala hataingia katika mji huu,’ ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. 34‘Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuokoa mji huu.’”
35Basi, usiku huo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu laki moja. Kulipopambazuka watu wakaamka, hao wote walionekana wakiwa maiti. 36Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru aliondoka akaenda zake na kukaa Ninewi. 37Siku moja wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe akatawala badala yake.



2Wafalme19;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.