1Ole wao wanaotunga sheria zisizo za haki,
watu wanaopitisha sheria za kukandamiza.
2Huwanyima maskini haki zao,
na kuwaibia maskini wa watu wangu maslahi yao.
Wajane wamekuwa nyara kwao;
yatima wamekuwa mawindo yao.
3Je, mtafanya nini siku ya adhabu,
siku dhoruba itakapowajieni kutoka mbali?
Mtamkimbilia nani kuomba msaada?
Mtakwenda wapi kuweka mali yenu?
4Litakalowabakia ni kujikunyata kati ya wafungwa
na kuangamia pamoja na wanaouawa vitani.
Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia,
bado ameunyosha mkono wake.
Onyo kwa mfalme wa Ashuru
5 10:5-34 Taz Isa 14:24-27; Nah 1:1--3:19; Sef 2:13-15
Ole wake Ashuru, fimbo ya hasira yangu,
yeye ashikaye kiboko cha hasira yangu!
6Nilimtuma kuliadhibu taifa ovu,
nilimwamuru kuwaadhibu watu niliowakasirikia,
kuwapora na kuteka nyara,
na kuwakanyaga chini kama tope njiani.
7Lakini Ashuru hakudhamiria hivyo,
yeye alikuwa na nia nyingine;
alikusudia kuharibu kabisa,
kuangamiza mataifa mengi iwezekanavyo.
8Maana alisema:
“Je, si kweli majemadari wangu ni wafalme?
9Je, si kweli kwamba Kalno nitautenda kama Karkemishi,
mji wa Hamathi kama mji wa Arpadi,
Samaria kama Damasko?
10Kama nimefaulu kuunyosha mkono wangu
dhidi ya falme zenye sanamu za miungu
kubwa kuliko sanamu za Yerusalemu na Samaria;
11je, nitashindwa kuutenda Yerusalemu na sanamu zake,
kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?”
12Wakati Mwenyezi-Mungu atakapomaliza kazi zake zote mlimani Siyoni na mjini Yerusalemu, atamwadhibu mfalme wa Ashuru, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake.
13Maana mfalme wa Ashuru alisema:
“Kwa nguvu zangu mwenyewe nimetenda hayo,
na kwa hekima yangu, maana mimi ni mwerevu!
Nimeondoa mipaka kati ya mataifa,
nikazipora hazina zao;
kama fahali nimewaporomosha walioketia viti vya enzi.
14Kama mtu anyoshaye mkono kwenye kiota,
ndivyo nilivyochukua mali yao;
kama mtu aokotavyo mayai yaliyoachwa kiotani,
ndivyo nilivyowaokota duniani kote,
wala hakuna mtu aliyeweza kupiga bawa,
au aliyefungua kinywa kunipigia kelele.”
Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:
15“Je, shoka litajigamba dhidi ya anayelitumia?
Msumeno waweza kujivuna dhidi ya mwenye kukata nao?
Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua anayeishika,
au mkongojo kumwinua mwenye kuutumia!”
16Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
atawaletea askari wao ugonjwa wa kuwakondesha,
na fahari yao itateketezwa kama kwa moto.
17Mungu aliye mwanga wa Israeli atakuwa kama moto,
Mtakatifu wa Israeli atakuwa mwali wa moto
ambao kwa siku moja utateketeza kila kitu:
Miiba yake na mbigili zake pamoja.
18Misitu yake ya fahari na mashamba yake mazuri,
Mwenyezi-Mungu atayaangamiza yote;
itakuwa kama mtu aliyemalizwa na ugonjwa.
19Miti itakayobaki msituni mwake itakuwa michache sana
hata mtoto mdogo ataweza kuihesabu.
Wachache watarudi
20Siku ile wazawa wa Yakobo watakaobaki, naam, Waisraeli watakaosalia hawatalitegemea tena taifa lililowaadhibu, bali watamtegemea kabisa Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. 21Wazawa wa Yakobo wachache watakaobaki watamrudia Mungu Mkuu. 2210:22 Taz Roma 9:27 Maana, hata kama sasa Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaorudi. Maangamizi yamepangwa yafanyike, nayo yatafanyika kwa haki tupu. 23Naam! Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atakamilisha kabisa katika nchi yote jambo aliloamua kutenda.
Mwenyezi-Mungu ataiadhibu Ashuru
24Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi watu wangu mnaokaa Siyoni msiwaogope Waashuru ambao wanawapiga kwa fimbo, wakiinua mikongojo yao dhidi yenu kama walivyofanya Wamisri. 25Maana bado kitambo, nayo hasira yangu itapita na ghadhabu yangu itawageukia Waashuru. 26Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi na nitawachapa kama nilivyowachapa Wamidiani kwenye jabali la Orebu. Nitanyosha fimbo yangu juu ya bahari kuwachapa kama nilivyowafanya Wamisri. 27Wakati huo, mzigo waliowabebesha nitauondoa na nira waliyowatia shingoni mwenu itavunjwa.”
Adui anakaribia
Adui amepanda kutoka Rimoni,
28amefika mjini Ayathi.
Amepitia huko Migroni,
mizigo yake ameiacha Mikmashi.
29Amekwisha pita kivukoni,
usiku huu analala Geba.
Watu wa Rama wanatetemeka kwa hofu,
wakazi wa Gibea, mji wa Shauli, wamekimbia.
30Pazeni sauti enyi watu wa Galimu!
Tegeni sikio enyi watu wa Laisha!
Jibuni enyi wenyeji wa Anathothi!
31Watu wa Madmena wako mbioni,
wakazi wa Gebimu wanakimbilia usalama.
32Leo hii, adui atatua Nobu,
atatikisa ngumi yake dhidi ya mlima Siyoni;
naam, atautikisia ngumi mji wa Yerusalemu.
33Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi
atakata matawi yake kwa ukatili;
miti mirefu itaangushwa chini,
walio juu wataaibishwa.
34Atakata vichaka vya msituni kwa shoka,
Lebanoni na mierezi yake maarufu itaanguka.
Isaya10;1-34
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.