Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 21 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 3...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


“Usimdhulumu jirani yako wala kumwibia. Mshahara wa mtu aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi. Usimlaani kiziwi wala kuweka kizuizi mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

Walawi 19:13-14

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

“Unapotoa hukumu uamue kwa haki; usimpendelee maskini wala kumwogopa mwenye cheo. Bali ni lazima kumwamua jirani kwa haki.

Walawi 19:15

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kamwe usipitepite ukiwachongea watu wa jamaa yako. Usiyatie maisha ya jirani yako katika hatari ya kifo kwa maneno yako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

Walawi 19:16

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



 Petro na Yohane wanamponya kiwete

1Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. 2Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. 3Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. 4Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” 5Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. 6Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” 7Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. 8Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. 9Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. 10Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
Hotuba ya Petro
11Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. 12Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea? 13Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa babu zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru. 14Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini nyinyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe. 15Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uhai. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo. 16Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.
17“Sasa ndugu zangu, mnafahamu kwamba nyinyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutokujua kwenu. 18Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke. 19Basi, tubuni, mkamrudie Mungu ili yeye afute dhambi zenu. 20Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu. 21Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani. 22Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu nyinyi wenyewe. 23Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.’ 24Manabii wote, kuanzia Samueli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi. 25Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: ‘Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.’ 26Basi, Mungu alimfufua mtumishi wake kwa faida yenu kwanza, akamtuma awaleteeni baraka kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake.”

Matendo3;1-26
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Friday 18 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 2...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa, naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake.

Walawi 19:7-8

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


“Utakapovuna mavuno ya nchi yako, usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba wala usirudi nyuma kukusanya mabaki. Msirudie kukusanya kila kitu katika shamba la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini; utawaachia maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Walawi 19:9-10



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


“Msiibe, msidanganye wala kuambiana uongo. Msiape uongo kwa jina langu hata kulikufuru jina la Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

Walawi 19:11-12

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Roho Mtakatifu anawashukia waumini
1Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja. 2Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. 3Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. 4Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.
5Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. 6Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? 8Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? 9Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, 10Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, 11Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.” 12Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?” 13Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”
Hotuba ya Petro
14Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. 15Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? 16Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana,
nitawamiminia binadamu wote Roho wangu.
Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike,
nitawamiminia Roho wangu siku zile,
nao watatoa unabii.
19Nitatenda miujiza juu angani,
na ishara chini duniani;
kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’
22“Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. 23Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. 24Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. 25Maana Daudi alisema juu yake hivi:
‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima;
yuko nami upande wangu wa kulia hata sitatikisika.
26Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi;
tena nilipiga vigelegele vya furaha.
Mwili wangu utakaa katika tumaini,
27maana hutaiacha roho yangu kuzimu,
wala kumruhusu mtakatifu wako aoze.
28Umenionesha njia za uhai,
umenijaza furaha kwa kuwako kwako!’
29“Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. 30Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. 31Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’ 32Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. 33Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia. 34Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema:
‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kulia,
35hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’
36“Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.”
37Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?” 38Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu. 39Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.”
40Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.” 41Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao 3,000 wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo. 42Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali.
Maisha ya kila siku ya wale waumini

43Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu. 44Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawiana. 45Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja. 46Waliendelea kukutana pamoja kila siku hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu. 47Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa. 


Matendo2;1-47
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Thursday 17 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Yohane,Leo Tunaanza Kitabu cha Matendo....1


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Yohane
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Matendo"
tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Iambie jumuiya yote ya watu wa Israeli hivi: Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Walawi 19:1-3

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Msizigeukie sanamu za miungu, wala msijitengenezee sanamu za kusubu za miungu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Walawi 19:4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


“Mnaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za amani, mtanitolea kama itakiwavyo ili mpate kukubaliwa. Sadaka hiyo ni lazima iliwe siku hiyohiyo inapotolewa au kesho yake. Chochote kinachobaki hadi siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto.

Walawi 19:5-6

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 1Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake 2mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3Kwa muda wa siku arubaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. 4Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. 5Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu anapaa mbinguni
6Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?” 7Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. 8Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.” 9Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.
10Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, 11wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.”
Mathia anachaguliwa ashike nafasi ya Yuda
(Mat. 27:3-10)
12Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka ule mlima uitwao Mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. 13Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.
15Siku moja baadaye, Petro alisimama kati ya wale ndugu waumini ambao walikuwa wamekusanyika, wote jumla watu 120, 16akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. 17Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu, maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.”
18Yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu, akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. 19Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba “Akel Dama,” maana yake, “Shamba la Damu.”) 20“Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi:
‘Makao yake yabaki mahame;
mtu yeyote asiishi ndani yake.’
Tena imeandikwa:
‘Mtu mwingine achukue nafasi yake ya huduma.’
21Basi, mtu mmoja miongoni mwa wale walioandamana nasi muda wote Bwana Yesu alipokuwa anasafiri pamoja nasi achaguliwe kujiunga nasi. 22Huyo anapaswa kuwa mmoja wa wale walioandamana nasi tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni. Huyo atashiriki pamoja nasi jukumu la kushuhudia ufufuo wake Yesu.”
23Hapo, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. 24Kisha wakasali: “Bwana, wewe unaijua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.” 26Wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.

Matendo1;1-26
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe