Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 3 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 12...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Hufikiria kununua shamba, kisha hulinunua, na kulima zabibu kwa faida ya jasho lake. Huwa tayari kufanya kazi kwa nguvu na kuiimarisha mikono yake.

Methali 31:16-17

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Hutambua kwamba shughuli zake zina faida; hufanya kazi hata usiku kwa mwanga wa taa yake. Husokota nyuzi kwa mikono yake mwenyewe, kwa vidole vyake mwenyewe husuka nguo zake.

Methali 31:18-19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Huufungua mkono wake kuwapa maskini, hunyosha mkono kuwasaidia fukara. Hawahofii watu wake ijapo baridi ya kipupwe, maana kila mmoja anazo nguo za kutosha.

Methali 31:20-21

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.




Yesu anapakwa marashi
(Mat 26:6-13; Marko 14:3-9)
1Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. 2Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. 3Basi, Maria alichukua nusu lita ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. 4Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, 5“Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari 300, wakapewa maskini?” 6Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. 7Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. 8Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.”
Njama za kumwua Lazaro
9Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu. 10Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, 11maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mat 21:1-11; Marko 11:1-11; Luka 19:28-40)
12Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. 13Taz Zab 118:25,26 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema:
“Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.
Abarikiwe mfalme wa Israeli.”
14Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
15“Usiogope mji wa Siyoni!
Tazama, Mfalme wako anakuja,
amepanda mwanapunda!”
16Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
17Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia. 18Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. 19Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”
Wagiriki kadhaa wanataka kumwona Yesu
20Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. 21Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.” 22Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. 23Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! 24Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. 25Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele. 26Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
Yesu anasema juu ya kifo chake
27“Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii. 28Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.”
29Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!” 30Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. 31Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. 32Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.” 33(Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani).
34 Taz Zab 110:4 Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?” 35Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. 36Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
Watu hawana imani
37Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. 38Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia:
“Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu?
Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?”
39Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena:
40“Mungu ameyapofusha macho yao,
amezipumbaza akili zao;
wasione kwa macho yao,
wasielewe kwa akili zao;
wala wasinigeukie, asema Bwana,
ili nipate kuwaponya.”
41Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
42Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. 43Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu.
Yesu alikuja kuuokoa ulimwengu

44Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. 45Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. 46Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. 47Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. 48Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. 49Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. 50Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.” 


Yohane12;1-50
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Wednesday 2 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 11...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Mke mwema kweli, apatikana wapi? Huyo ana thamani kuliko johari! Mumewe humwamini kwa moyo, kwake atapata faida daima.

Methali 31:10-11

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Kamwe hamtendei mumewe mabaya, bali humtendea mema maisha yake yote. Hutafuta sufu na kitani, na kufanya kazi kwa mikono yake kwa bidii.

Methali 31:12-13

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Yeye ni kama meli za biashara: Huleta chakula chake kutoka mbali. Huamka kabla ya mapambazuko, akaitayarishia jamaa yake chakula, na kuwagawia kazi watumishi wake.

Methali 31:14-15

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Kifo cha Lazaro

1Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. 2Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). 3Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!”
4Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.”
5Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. 6Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. 7Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!” 8Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?” 9Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. 10Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.” 11Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.” 12Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.” 13Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. 14Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa; 15lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.” 16Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!”
Yesu ni ufufuo na uhai
17Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. 18Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu, umbali upatao kilomita tatu. 19Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
20Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. 21Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! 22Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” 23Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.” 24Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.” 25Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; 26na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?” 27Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Mimi naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.”
Yesu analia machozi
28Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwambia faraghani, “Mwalimu yuko hapa, anakuita.” 29Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu. 30Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki. 31Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
32Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwambia, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!” 33Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni. 34Kisha akawauliza, “Mlimweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.” 35Yesu akalia machozi. 36Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!” 37Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?”
Yesu anamfufua Lazaro
38Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe. 39Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwisha anza kunuka; amekaa kaburini siku nne!” 40Yesu akamwambia, “Je, sikukuambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?” 41Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, “Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza. 42Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” 43Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro! Toka nje!” 44Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mkamwache aende zake.”
Njama ya kumwua Yesu
(Mat 26:1-5; Marko 14:1-2; Luka 22:1-2)
45Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu, wakamwamini. 46Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu. 47Kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza Kuu, wakasema, “Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. 48Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu hekalu letu na taifa letu!” 49Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akawaambia, “Nyinyi hamjui kitu! 50Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?” 51Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao; 52na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
53Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu. 54Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. 55Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo. 56Basi, wakawa wanamtafuta Yesu. Nao walipokusanyika pamoja hekaluni, wakaulizana, “Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?” 57Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.

Yohane11;1-57
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

Tuesday 1 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yohane 10...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Maneno ya mfalme Lemueli. Mawaidha aliyofundishwa na mama yake: Nikuambie nini mwanangu? Nikuambie nini mwanangu niliyekuzaa? Nikuambie nini wewe niliyekuomba kwa Mungu? Usimalize nguvu zako kwa wanawake, usiwape mali yako hao wanaoangamiza wafalme.

Methali 31:1-3

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Haifai ee Lemueli, haifai wafalme kunywa divai, wala wakuu kutamani vileo. Wakinywa watasahau maagizo ya sheria, na kuwanyima haki wenye taabu. Mpe kileo mtu anayekufa, wape divai wale wenye huzuni tele; wanywe na kusahau umaskini wao, wasikumbuke tena taabu yao.

Methali 31:4-7

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Lakini wewe, lazima useme kwa ajili ya wote walio bubu; na kutetea haki za wote wasiojiweza. Sema kwa ajili yao na kuamua kwa haki, linda haki za maskini na fukara.

Methali 31:8-9

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Mchungaji mwema
1“Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyanganyi. 2Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. 3Mngojamlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake, na kuwaongoza nje. 4Akisha watoa nje huwatangulia mbele, nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. 5Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake.” 6Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
Yesu mchungaji mwema
7Basi, akasema tena, “Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. 8Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyanganyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. 9Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. 10Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai – uhai kamili.
11“Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. 12Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwamwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. 13Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. 14Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, 15kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. 16Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
17“Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. 18Hakuna mtu anayeninyanganya uhai wangu; mimi nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye.”
19Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. 20Wengi wao wakasema, “Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?” 21Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?”
Yesu anakataliwa na Wayahudi
22Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. 23Naye Yesu akawa anatembea hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. 24Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, “Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiwe Kristo, basi, tuambie wazi.” 25Yesu akawajibu, “Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. 26Lakini nyinyi hamsadiki kwa sababu nyinyi si kondoo wangu. 27Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. 28Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. 29Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. 30Mimi na Baba, tu mmoja.”
31Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. 32Yesu akawaambia, “Nimewaonesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?” 33Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya kazi njema, ila kwa sababu ya kumkufuru Mungu! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.” 34Taz Zab 82:6 Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika sheria yenu: ‘Mimi nimesema, nyinyi ni miungu?’ 35Mungu aliwaita miungu wale waliopewa ujumbe wake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. 36Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: ‘Unakufuru,’ eti kwa sababu nilisema: ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ 37Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini. 38Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi, mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake.” 39Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.

40Yesu akaenda tena ngambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. 41Watu wengi walimwendea wakasema, “Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa.” 42Watu wengi mahali hapo wakamwamini. 


Yohane10;1-42

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe