Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru na kumsifu..
Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.. Baba wa Mbinguni,Mfalme wa Amani,Baba wa huruma,Mungu wa wajane,Baba wa yatima,Mponyaji wetu,Mlinzi wetu,Kimbilio letu.. Uhimidiwe Yahweh,Uabudiwe milele,Utukuzwe Baba wa Mbinguni, Usifiwe Mungu wetu,Unastahili sifa,Mwimbieni Mungu sifa,Mwimbieni.! Mwimbieni Mfalme wetu sifa Mwimbieni..! Mshangilieni, Mwimbieni Mungu sifa,simulieni matendo yake ya ajabu..! Uniwezeshe kusema, ee Bwana, Midomo yangu itangaze sifa zako..!Imbeni juu ya Utukufu wa jina lake, Mtoleeni sifa tukufu..! Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,wakiimba daima sifa zako..!!
Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?” Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?” Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu.. Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote.. Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha,na kujiachilia mikononi mwako Jehovah.. Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nzareti.. Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu.. Yahweh ukatupe neema ya ubunifu,maarifa katika vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende kama inavyokupendeza wewe Jehova tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu ukatupe neema ya uvumilivu,kusameheana, kuchukuliana,kuhurumiana,kusaidiana,kuelimishana kwa amani, Upendo ukadumu na kila mmoja akajue jukumu lake na kazi yake.. Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako watoto,wazazi wetu familia/ndugu na wote wanaotuzunguka.. Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu sisi na vyote tunavyovimiliki Baba wa Mbinguni ukatawale katika maisha yetu,ukatamalaki na kutuatamia,tuka nene yaliyo yako Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu.. Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kusimamia neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu.. Yahweh ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’” Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado).
Yahweh tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa ukawape tunaini,wagonjwa ukawaponye,wenye njaa Baba ukawatendee na kubariki kazi zao,mashamba na wakapate mahitaji ya kutosha na akiba... walio katika vifungo mbalimbali vya yule mwovu Baba ukawafungue na kuwaweka huru,ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweke huru..
Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!” Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, “Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?” Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!”
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu.. Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele.. Amina..!!
Wapendwa katika Bwana asanteni kwakuwa nami Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye.. Nawapenda.. |