Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!
Showing posts with label Kheri na Baraka. Show all posts
Showing posts with label Kheri na Baraka. Show all posts

Sunday 16 July 2017

Natumaini Jumapili Ilikuwa Njema/Inaendelea Vyema;Burudani-Mwamba Mwamba,Nanyinginezo - Chiri Msa Msa (Solly Mahlangu)

Shalom...! Wapendwa/Waungwana..
Habari za Jumapili?Nimatumaini yangu inaendelea vyema..
Hapa kwetu Mungu yu mwema sana Jumapili ilikuwa njema/inaendelea vyema kabisa..
Mungu ametubariki na kutupa kibali cha kwenda nyumbani mwa Bwana kushiriki Ibada na wapendwa wengine..
Vipi upande wako wewe umebarikiwa kuingia nyumbani mwa Bwana?Jumapili yako ilikuwaje/inaendeleaje?
Umepokea?Umebarikiwa?Umejifunza na kuyazingatia?
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..

Neno La Leo;1Wakorintho 2



Ujumbe juu ya Yesu aliyesulubiwa

1Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu. 2Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa. 3Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi. 4Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho. 5Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu.


Hekima ya Mungu

6Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea. 7Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu. 8Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangaliielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. 9Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona,
wala sikio kuyasikia,
mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni,
hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.”
10Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu. 11Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12Sasa, sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu.
13Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. 14Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. 15Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine. 16Maandiko yasema: “Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?” Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.






"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe Sana.

Sunday 18 June 2017

Natumaini Jumapili ilikuwa njema/inaendelea vyema;Happy Father's Day..Burudani-Phil Wickham - This Is Amazing Grace,At Your Name (Yahweh Yahweh)



Shalom wapendwa/waungwana;Nimatumaini yangu mnaendelea vyema na mmekuwa kuwa na wakati mzuri Jumapili hii..
Hapa kwetu leo kijua kimewaka haswaaa kama tupo Dar..
Tunamshukuru Mungu katika yote..

Niwatakie heri na baraka wa Baba wote.."Happy Father's Day" kwa wazazi/Baba wote wanaojua majukumu yao ..
Mungu aendelee kuwaongoza katika malezi ya watoto wenu na kwa watoto wengine wote..

Nimshukuru Baba wa watoto wangu kwa kuwa karibu na watoto wake na kujua/kutumikia majukumu yake..Mungu aendelee kumuongoza..
R.I.P. Baba yangu haupo nasi lakini kila leo tunakukumbuka katika yote..
ulipokuwa unatuasa/kutufundisha ,Kutushauri yooote tunayaona  sasa..
Ulipokuwa unasema wakati ule tulikuwa tunaona kama unaimba au unaongea sana[unatuzingua]
Maneno hayaozi...
Tunamshukuru Mungu kwa kila jambo yeye nimwema tuu..



Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. “Waheshimu Baba na mama yako,” hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, “Upate fanaka na kuishi miaka mingi duniani.” Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.


Wanangu, sikilizeni mwongozo wa baba yenu, tegeni sikio mpate kuwa na akili.

Siandiki mambo haya kwa ajili ya kuwaaibisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwafundisheni watoto wangu wapenzi. Maana hata kama mnao maelfu ya walezi katika maisha yenu ya Kikristo, baba yenu ni mmoja tu, kwani katika kuungana na Kristo mimi ndiye niliyewazaeni kwa kuihubiri Habari Njema. Kwa hiyo, nawasihi: Fuateni mfano wangu. Ndiyo maana nimemtuma Timotheo kwenu. Yeye ni mtoto wangu mpenzi na mwaminifu katika kuungana na Bwana. Atawakumbusheni njia ninayofuata katika kuungana na Kristo; njia ninayofundisha kila mahali katika makanisa yote.








"Swahili Na Waswahili"Pamoja Daima.

Sunday 28 May 2017

Natumaini Jumapili Ilikuwa Njema/inaendelea Vyema;Burudani-Miriam Lukindo Mauki - Hakuna Wa Kubadili Na Eunice Njeri - Nani Kama Wewe ..!!




Ni Nani kama wewe Nakuinua Mungu wangu Leo Nani kama wewe Nakupendaaa..!!
Miguuni pako Nakuinamia Bwana  Heshima na utukufu Baba nakupa Yesu..!!Nimekuja nikuinue Nimekuja nikupendeeh Miguuni pako Nakupendaaa..!!

Haleluyahh.! Mungu wetu  yu mwema sana. Haijalishi nini unapitia,Haijalishi umejikwaaje..!Inuka na uendelee na safari   hakuna mwingine tena kama Mungu..

Wapendwa/Waungwana Natumaini mlikuwa na Jumapili Njema/mnaendelea vyema na Jumapili hii..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwapa sawasawa na mapenzi yake..
Amina ooh Amina oohh Amina Mileleeeh..!!
1Mungu wenu asema:
“Wafarijini watu wangu,
nendeni mkawafariji.

Neno la Leo;Isaya 40:1-31 



Tumaini la kuponywa katika Yerusalemu
1Mungu wenu asema:
“Wafarijini watu wangu,
nendeni mkawafariji.
2Semeni na wenyeji wa Yerusalemu kwa upole,
waambieni kwamba utumwa wao umekwisha,
wamesamehewa uovu wao.
Mwenyezi-Mungu amewaadhibu maradufu
kwa sababu ya dhambi zao zote.”
3 40:3 Taz Mat 3:3; Marko 1:3; Yoh 1:23 Sauti ya mtu anaita jangwani:
“Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia,
nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu. 40:3-5 Taz Luka 3:4-6
4Kila bonde litasawazishwa,
kila mlima na kilima vitashushwa;
ardhi isiyo sawa itafanywa sawa,
mahali pa kuparuza patalainishwa.
5Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu utafunuliwa,
na watu wote pamoja watauona.
Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hayo.”
6 40:6-8 Taz Yak 1:10-11; 1Pet 1:24-25 Sikiliza! Kuna sauti inasema, “Tangaza!”
Nami nikauliza, “Nitangaze nini?”
Naye: “Tangaza: Binadamu wote ni kama majani;
uthabiti wao ni kama ua la shambani.
7Majani hunyauka na ua hufifia,
Mwenyezi-Mungu avumishapo upepo juu yake.
Hakika binadamu ni kama majani.
8Majani hunyauka na ua hufifia,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9Nenda juu ya mlima mrefu,
ewe Siyoni, ukatangaze habari njema.
Paza sauti yako kwa nguvu,
ewe Yerusalemu, ukatangaze habari njema.
paza sauti yako bila kuogopa.
Iambie miji ya Yuda:
“Mungu wenu anakuja.”
10 40:10 Taz Isa 62:11; Ufu 22:12 Bwana Mungu anakuja na nguvu,
kwa mkono wake anatawala.
Zawadi yake iko pamoja naye,
na tuzo lake analo.
11 40:11 Taz Eze 34:15; Yoh 10:11 Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
atawakusanya wanakondoo mikononi mwake,
atawabeba kifuani pake,
na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Bwana ameshakubali hakuna wakubadili..!!
 Ameshasema ndiyo Leo hakuna wa kubadili
Yeye ni Bwana wa Ma Bwana Hakuna wakubadili...!
Yeye ni Mwamba wa miamba hakuna wa Kubalidili..!!


Mungu wa Israeli hana kifani
12Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake,
kuzipima mbingu kwa mikono yake?
Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni;
kuipima milima kwa mizani
au vilima kwa kipimo cha uzani?
13 40:13 Taz Rom 11:34; 1Kor 2:16 Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu,
au kuwa mshauri wake na kumfunza?
14Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri,
ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi?
Nani aliyemfunza njia za haki?
Nani aliyemfundisha maarifa,
na kumwonesha namna ya kuwa na akili?
15Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo,
ni kama vumbi juu ya mizani.
Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini.
16Kuni zote za Lebanoni
na wanyama wake wote
havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake.
17Mataifa yote si kitu mbele yake;
kwake ni vitu duni kabisa na batili.
18 40:18-19 Taz Mate 17:29 Mtamlinganisha Mungu na nini basi,
au ni kitu gani cha kumfananisha naye?
19Je, anafanana na kinyago?
Hicho, fundi hukichonga,
mfua dhahabu akakipaka dhahabu,
na kukitengenezea minyororo ya fedha!
20Au ni sanamu ya mti mgumu?
Hiyo ni ukuni mtu anaochagua,
akamtafuta fundi stadi,
naye akamchongea sanamu imara!
21Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Je, hamkuambiwa tangu mwanzo?
Je, hamjafahamu mwanzo wa dunia?
22Dunia iliumbwa na huyo aketiye juu ya mbingu;
kutoka huko wakazi wa dunia ni kama panzi!
Yeye amezitandaza mbingu kama pazia,
na kuzikunjua kama hema la kuishi.
23Yeye huwaporomosha wakuu wenye nguvu,
watawala wa dunia huwafanya kuwa si kitu.
24Mara tu wanaposimikwa na kuanza kuota,
hata kabla hawajatoa mizizi kama miti udongoni,
Mwenyezi-Mungu akiwapulizia hunyauka,
kimbunga huwapeperusha kama makapi!
25Mungu Mtakatifu auliza hivi:
“Nani basi, mtakayemlinganisha nami?
Je, kuna mtu aliye kama mimi?”
26Inueni macho yenu juu mbinguni!
Je, ni nani aliyeziumba nyota hizo?
Ni yule aziongozaye kama jeshi lake,
anayeijua idadi yake yote,
aziitaye kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi,
hakuna hata moja inayokosekana.
27Enyi watu wa Israeli wazawa wa Yakobo,
kwa nini mnalalamika na kusema:
“Mwenyezi-Mungu hatujali sisi!
Mungu wetu hajali haki yetu!”
28Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu wa milele;
yeye ndiye Muumba wa kila kitu duniani.
Yeye hafifii kamwe wala kuishiwa nguvu.
Maarifa yake hayachunguziki.
29Yeye huwapa uwezo walio hafifu,
wanyonge huwapa nguvu.
30Hata vijana watafifia na kulegea;
naam, wataanguka kwa uchovu.
31Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu,
watapata nguvu mpya.
Watapanda juu kwa mabawa kama tai;
watakimbia bila kuchoka;
watatembea bila kulegea.







"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe Sana.

Sunday 9 April 2017

Nimatumaini Yangu Jumapili ilikuwa/inaendelea nyema;Burudani-UPENDO CHOIR. AZANIA FRONT KKKT CATHEDRAL CHURCH (TUKITEMBEA NURUNI ALBUM)

Wapendwa/Waungwana nimatumaini yangu mmekuwa na mnaendelea na Jumapili hii vizuri..hapa kwetu ni salama kabisa na leo kijua kimeonekana..
Mungu yu mwema na aendelee kuwabariki katika yote..Mkawe na wakati mwema..
Watoto hapa kwetu wapo likizo pia baadhi ya wazazi waliowahi kuomba likizo muwe na wakati mwema natumai mtakuwa na wakati mwema na watoto/familia..
Wanaondelea na kazi Mungu aendelee kuwaongoza katika kazi zenu...
Basi tukatumie Ulimi wetu vyema..Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tuwe na kiasi..

Nawapenda...
 Neno La Leo;Yakobo3:1-18

Ulimi
1Ndugu zangu, wengi wenu msiwe waalimu. Kama mjuavyo, sisi waalimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine. 2Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote. 3Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka. 4Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka. 5Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana.
Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa. 6Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe

7Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote – wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. 8Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. 9Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huhuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. 10Maneno ya kubariki na ya kulaani hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. 11Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? 12Ndugu zangu, je, mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

Hekima itokayo juu mbinguni
13Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aoneshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima. 14Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli. 15Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani. 16Maana popote palipo na wivu na ubinafsi, hapo pana fujo na kila aina ya uovu. 17Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki. 18Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.




Shukrani;Daniel Christopher

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday 26 March 2017

Natumaini Juma pili Ilikuwa/Inaendelea Vyema;Happy Mothers Day..Burudani-10,000 Reasons (Bless the Lord) ,I Give You My Heart | Hillsong ,I Need You More




Wapendwa/Waunngwana Natumaini mmekuwa/Mnendelea  na wakati mzuri Jumapili ya Leo....
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea katika yote yaliyo mema..Awape sawasawa na Mapenzi yake..
Hapa tulipo Leo tunasheherekea Siku Ya Mama.."Happy Mothers Day" Kwa Mama yangu Mpendwa na Nguzo yangu,
kwangu na Wamama wote..Mungu aendelee kuwabariki na kufurahia uzao wenu..!!
Mungu akawajaalie wote wanaotafuta watoto, watoto hao wakawe Baraka kwao na Jamii pia...
Mungu akabariki vizazi vyetu, watoto wetu wakamjue Mungu na wawe Baraka kwetu na Jamii pia..
Sifa na Utukufu ni kwako Mungu..

Neno La Leo;Waroma 8:18-39



Utukufu ujao
18Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. 20Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, 21maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. 22Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. 23Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. 24Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? 25Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.
26Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. 27Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
28Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. 29Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.
Upendo wa Mungu
31Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? 32Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? 33Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! 34Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! 35Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? 36Taz Zab 44:22Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha;
tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.”
37Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. 38Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; 39wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):










"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday 12 March 2017

Natumaini Jumapili inaendelea Vyema;"Wanawake ni Nguvu ya Jamii",[Hongera Wanawake]Burudani kwa Mwanamke,Emmy Kosgei_Mama,TAAI (we are moving forward )

Wapendwa /Waungwana Ni matumaini yangu jumapili inaendelea vyema,pia Wanawake mlisheherekea/Manaendelea kusheherekea Vyema siku Yenu..Pia naamini Wanaume mlikuwa/mko sambamba kuungana na Wanawake kwenye siku yao..
Mwanamke ni nani kwako wewe Mwanaume?
Jee wewe Mwanamke unajitambua na kujivunia kuwa Mwanamke?
Nini kikubwa hutakisahau chema/kibaya ulichokifanya kama Mwanamke ulipaswa kukifanya/kutokifanya?
Mungu aendelee kuwabariki na kuwaongoza katika majukumu yenu kama Wanawake.
Neno La Leo;Esta 2;1-23

Esta anateuliwa kuwa malkia

1Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake. 2Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja? 3Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi. 4Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo.
5Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. 6Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni.
7Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake.
8Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. 9Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie.
10Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. 11Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
12Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero. 13Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu. 14Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.
15Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye. 16Basi, Esta alipelekwa ikulu kwa mfalme katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Ahasuero, mwezi wa kumi uitwao Tebethi. 17Mfalme alipendezwa zaidi na Esta kuliko alivyopendezwa na wanawake wengine wote. Alipendwa sana kuliko wasichana wengine. Basi, mfalme akamvika taji ya kimalkia kichwani, akamfanya malkia badala ya Vashti. 18Kisha mfalme akaandaa karamu kubwa kwa heshima ya Esta, akawaalika viongozi na watumishi wote wa serikali yake. Pia, mfalme alitangaza msamaha wa kodi katika mikoa yote, akatoa zawadi nyingi kulingana na hadhi yake ya kifalme.










Mordekai aokoa maisha ya mfalme

19Wasichana walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi penye lango la mfalme. 20Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye.
21Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. 22Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. 23Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


Sunday 5 March 2017

Jumapili Indelee Vyema;Burudani-Mireille Basirwa - Tunashuka na nyingine..




Wapendwa/Waungwana nimatumaini yangu mmekuwa na siku njema,Basi Mungu andelee kuwabariki awalinde na kuwaokoa katika yote..Bwana akaonekane katika maisha yenu,Muendelee kupokea Neema ya Mungu
Roho mtakatifu akawaongoze katika yote..
.
Awape sawaswa na Mapenzi yake..


Mpendwa wetu Da'Mireille Basirwa alifiwa na mtoto wake hivi karibuni..Pole sana Mpendwa ,Tunamuomba Mungu aendelee kukufariji na kukupa Nguvu, Uvumilivu wakati wote..

Neno La Leo;Zaburi 34:1-22


Sifa kwa wema wa Mungu
(Zaburi ya Daudi alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki)
1Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
2Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,
wanyonge wasikie na kufurahi.
3Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,
sote pamoja tulisifu jina lake.
4Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,
na kuniondoa katika hofu zangu zote.
5Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;
nanyi hamtaaibishwa kamwe.
6Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,
na kumwokoa katika taabu zake zote.
7Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,
na kuwaokoa katika hatari.
8  Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.
Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
9Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;
maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.
10Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;
lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
11Njoni enyi vijana mkanisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.
12  Je, watamani kufurahia maisha,
kuishi maisha marefu na kufurahia mema?
13Basi, acha kusema mabaya,
na kuepa kusema uongo.
14Jiepushe na uovu, utende mema;
utafute amani na kuizingatia.
15Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,
na kusikiliza malalamiko yao;
16lakini huwapinga watu watendao maovu,
awafutilie mbali kutoka duniani.
17Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,
na kuwaokoa katika taabu zao zote.
18Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
19Mateso ya mwadilifu ni mengi,
lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.
20  Huvilinda viungo vya mwili wake wote,
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
21Ubaya huwaletea waovu kifo;
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
22Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.














"Swahili Na Waswahili"Pamoja.